Serikali imesema inaandaa utaratibu wa kuhakiki vyeti vya taaluma vinavyotolewa na vyuo vya elimu ya juu vya ndani na nje ya nchi.
Wakati hayo yakielezwa, watumishi wa umma 14,409 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi huku 1,907 wakiwa hawajawasilisha vyeti kwa ajili ya kuhakikiwa licha ya Serikali kutoa muda wa kutosha kwa watumishi hao kuwasilisha vyeti vyao Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa ajili ya uhakiki.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurean Ndumbaro wakati akipokea taarifa ya sita na ya mwisho ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde.
Taarifa iliyotolewa jana na kitengo cha mawasiliano Ofisi ya Rais Utumishi, inaeleza kuwa mbali na Serikali kuandaa utaratibu huo, watumishi waliosoma vyuo vya nje ya nchi, watapaswa kuviwasilisha Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili vihakikiwe kujiridhisha uhalali na wake.
Katika taarifa hiyo, Dk Msonde amebainisha kuwa uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma ni vya ufaulu wa kidato cha nne, sita na ualimu.
Alisema katika awamu ya sita watumishi 5,696 wamehakikiwa vyeti vyao, kati ya hao 5,404 sawa na asilimia 94.82 wamebainika kuwa na vyeti halali na watumishi 295 sawa na asilimia 5.518 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi.
Alisema watumishi wa umma 511,789 wamehakikiwa katika awamu zote sita za uhakiki, kati ya hao watumishi 494,554 sawa na asilimia 96.71 vyeti vyao vimebainika kuwa ni halali, 14,409 sawa na asilimia 2.82 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi na watumishi 1,907 hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya uhakiki.
Katika taarifa hiyo, Dk Msonde alisema ofisi yake imebaini watumishi 71 majina yao halisi waliyoajiriwa nayo ni tofauti na majina katika vyeti walivyotumia kujipatia ajira katika utumishi wa umma.
Amebainisha kuwa ofisi yake ilichukua hatua ya kuwahoji wahusika ambao walitoa sababu mbalimbali zilizosababisha utofauti wa majina yao ikiwamo kubadili dini na kusema hilo liko nje ya uwezo wa taasisi yake na ameliwasilisha kwa katibu mkuu utumishi kwa ajili ya hatua stahiki.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Dk Ndumbaro, alisema anaamini waajiri wameshawaondoa katika orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali watumishi wote waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tano ya uhakiki, isipokuwa waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi katika awamu ya sita iliyotolewa jana.
Kuhusu watumishi 1,907 ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa wametenda kosa kwa kutotekeleza maagizo halali.
kuhusu watumishi 71 ambao majina yao halisi ni tofauti na yaliyopo katika vyeti vyao, katibu mkuu huyo alisema suala hilo litafanyiwa uchunguzi na kutoa taarifa itakayotoa maoni na ushauri wa hatua za kuchukuliwa.
Watumishi 295 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi katika uhakiki wa awamu ya sita iwapo hawataridhika na matokeo ya uhakiki wanapewa fursa ya kukata rufaa hadi Machi 31, mwaka huu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA