SERA YA ELIMU NA MADHARA YA SIASA KATIKA UTEKELEZAJI

Katika makala iliyopita juu ya siasa za Tanzania na hatima ya maendeleo ya taifa, nilizungumza kuhusu sera mbalimbali na madhara ya siasa kwenye utekelezaji wa sera, ambapo nilianza na sera ya elimu ya mwaka 2014. Nilizungumza kipengele kidogo kabisa cha elimu ya awali ambacho kimeainishwa katika sera ya elimu na mafunzo ya ufundi. Nilizungumzia mazingira gani ambayo mtoto anatakiwa kutengenezewa ili kumwezesha kushika kile anachofundishwa kulingana na umri wake. Ikumbukwe pia, kwenye sera, umri uliowekwa kuwa ni umri wa mtoto kupata elimu ya awali ambayo ni ya lazima ni miaka 3-5, na ni umri ambao kisaikolojia ni umri wa makuzi ya awali ya mtoto yaani, Early childhood stage, hatua ambayo leo nitaizungumzia kinagaubaga pamoja na umuhimu wake katika uzalishaji rasilimali watu, moja ya kiolezo muhimu kabisa katika
mazingira ya mtoto aliye katika hatua ya elimu ya awali.
Makuzi ya awali ya mtoto yanaanzia miaka 2-5, umri ambao ndani yake ni umri wa elimu ya awali iliyoainishwa kwenye tamko la sera ya mwaka 2014. Sifa kubwa ya umri huu ni kwamba, mtoto hukua zaidi misuli mikubwa, kuliko midogo, misuli ambayo humfanya kila kazi anayoifanya, aifanye kwa nguvu nyingi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mtoto mwenye umri wa miaka 2-5 huwa ana uwezo mkubwa sana wa kutumia misuli mikubwa katika kufanya kazi, misuli kama ya mikono, miguu na ya mabega. Katika kipindi hiki, mwendo wa ukuaji wa misuli midogo kama ya viganjani huwa ni ndogo sana, na kutokana na udogo wa mwendo wa kukua kwa misuli hii, mtoto aliye katika umri huu huwa na uwezo mdogo sana wa kufanya kazi ndogo kama kudhibiti mwandiko kwenye daftari. Hapa ndipo wataalamu wa saikolojia hushauri mtaala wa elimu uwe wenye mlengo wa kazi tu (activity oriented curriculum) ambapo hii humsaidia mtoto kuendeleza makuzi ya kawaida ya mwili ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa misuli yote. Mmoja kati ya wanasaikolojia wanaoshauri hili ni Maria Montensori katika kitabi chake cha Absorbent Mind.
Hali kwenye shule zetu ikoje?
Katika umri kama huu, kwanza kuanzia mavazi ya mtoto huwa ni tofauti kabisa na mavazi ya watoto wengine kama watoto walio katika madaraja ya mbele. Mfano, kaptura ya mtoto wa umri huu kitaalamu inatakiwa kuwa na lastic kiunoni, na si belt. Je, wajua ni kwa nini? Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mtoto wa umri huu, kama nilivyosema awali, huwa na uwezo wa misuli mikubwa kuliko misuli midogo, yaani more large muscles than fine muscles. Maana yake nini? Mfano, ni rahisi zaidi kwa mtoto wa umri huu kuvuta kaptura yake na kukojoa, kuliko kufungua zip na belt, kwa maana, kufungua belt na zip huhitaji misuli midogo, wakati kuvuta kaptura hutumia misuli mikubwa.
Maana yake nini kwa watoto walioko kwenye shule ya awali?
Nimefanya uchunguzi yakinifu na kugundua kwamba, watoto katika shule nyingi za awali wanafundishwa kuandika tarakimu na hata baadhi ya herufi, kitu ambacho ni sawa na kuandika 0 kwenye maji. Kwa nini? Kitendo cha kuandika huhitaji misuli midogo ya mtoto, misuli ambayo katika umri huu huwa haiku vizuri, hivyo ni vigumu kwa mtoto ku-control kiganja chake na kuandika herufi au tarakimu kwenye daftari ambalo walimu wanawahitaji watoto kuandika. Kama haitoshi, kuna shule zingine ambazo zinasisitiza mtoto awe na daftari la mistari mikubwa na midogo, ili kwenye hiyo mistari midogo ndimo mtoto anatakiwa kuunda herufi yake, nasema hili kamwe ni vigumu kufanikiwa. Msisitizo: katika umri tajwa wa mtoto kuanza elimu ya awali kwa lengo la kumtengenezea msingi wa madaraja mengine, mtaala haujaangalia vizuri saikolojia ya mtoto na hivyo, si rahisi kutengeneza msingi wa kuandika kwa mtoto mwenye umri uliotajwa kwenye sera.
USHAURI.
ü  Mtaaala wa elimu ya awali unatakiwa uwe na mlengo wa kuendeleza makuzi ya awali ya mtoto na si kuandika, maana si umri sahihi wa mtoto kujua kuandika kwa umri wake, na;
ü  Mtaala ujumuishe zaidi kazi za mwili (physical activities) ili kuijenga saikolojia ya mtoto katika umri huu.
Usikose kufuatilia makala zangu ambazo zinachambua sera ya elimu na mafunzo ya ufundi na mitaala yake kwa ujumla.
Wasiliana na mimi kwa nambari 0759 947 397 au nitumie ujumbe kwa barua pepe anwani jumahussein59@yahoo.com
Soma makala kwenye blog yangu ili tufahamishane mengi.

Chapisha Maoni

0 Maoni