SIASA ZA TANZANIA NA SERA MBALIMBALI, MADHARA YA SIASA KATIKA SERA.

Leo ningependa kuendelea na uchambuzi wangu wa siasa za Tanzania na hatima ya maendeleo ya nchi kama ilivyo ada ya ukurasa huu wa blog. Kikubwa ambacho ningependa leo kuchangia katika ukurasa huu ni juu ya sera mbalimbali za maendeleo na madhara ya siasa katika utekelezaji wa sera hizo. Pamoja na hilo, ningependa pia ndugu msomaji wangu wa makala hii utambue kuwa, siasa ni kila kitu katika maisha ya kila siku kama
nilivyosema kwenye mada yangu ya wiki iliyopita. Bila shaka utakumbuka vizuri niliongea masuala anuai yanayogusa utawala na masuala anuai ya kimaendeleo. Songa na mimi katika mada hii.
Kwanza kabisa nitumie fursa hii kuwashukuru wachangiaji wangu ambao pia wamenitia moyo kwa dhati kabisa katika kuendeleza uchambuzi wa masuala haya ambayo pia yanalenga mustakabali wa maisha yetu kama watanzania kwa ujumla wetu.
Sera ambayo ningependa kuanza nayo ni sera ya elimu ambayo imekuwa ikipigiwa kelele kila siku na wadau mbalimbali wa masuala ya elimu na hivyo kukosa muafaka halisi wa namna gani sera hii iwezeshwe kuwa yenye tija katika maisha ya watanzania walio wengi na imwandae pia mtanzania katika soko la ushindani la ajira Afrika na ulimwenguni kote. Pembeni yangu ninayo sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambayo imebainisha mambo mbalimbali ya msingi kabisa yenye lengo la kupiga hatua katika kile ambacho watunga sera wanaamini kuwa ni mtumbwi wa kuwasukuma watanzania kuelekea katika nchi yenye uchumi wa kati.
Kabla sijaenda mbali, nipende tu kuwakumbusha pia, sera yetu inaamini katika mfumo wa 2+7+4+2+3+, yaani, miaka miwili katika shule ya awali, ama chekechea, miaka saba ya elimu ya msingi, miaka mine ya shule ya upili (secondary), miaka miwili ya shule ya upili mwendelezo (Advanced secondary) na miaka mitatu na zaidi katika elimu ya chuo, kama ulivyoainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya ufundi Ukurasa wa 21.
Nini Tamko la serikali kwa elimu ya awali?
Nimeona tuanzie na matamko ya serikali katika mfumo huu ambao kimsingi mlengo mahsusi wa elimu yetu. Tamko la serikali kwenye elimy ya awali (chekechea) ni kama lifuatalo;
“Serikali itaweka utaratibu wa elimu ya awali kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitatu hadi mitano kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja” (T.I.E, 2014)
Kwa kawaida sera ya elimu ya awali kufanywa kuwa ya lazima ni jambo la msingi, lakini hofu yangu ni kwamba, je, ni mazingira gani ambayo mtoto atawekewa ili kumtengenezea uwezo na uelewa pamoja na kumjengea msingi imara wa kitaaluma ili aweze kuendela vema na viwango vingine zaidi vitakavyofuatia?
Tafsiri yangu ya msingi ni kwamba, je serikali imeandaa nini maalumu kwa watoto wanaoanza na shule hii ya awali ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na vitu? Umri uliotajwa kiukweli kabisa na kifalsafa ni halisi kwa mtoto kujifunza vitu vyepesi vyepesi hasa kwa njia ya michezo, kama alivyowahi kueleza mwanafalsafa Jacques Rossoeau, ambapo anaamini kwamba, katika hali ya kawaida na umri wa kuanzia miaka 0-5, mtoto anatakiwa ajifunze vitu vya kawaida kwa njia ya michezo na kuimba ambayo itamjengea uelewa. Swali hapa ni je, mazingira ya michezo kwa mtoto, serikali imejipangaje, ikiwa ni pamoja na bembea mashuleni maalumu kwa ajili ya hiyo michezo, au tu kwa kucheza chini na kuchimbachimba ndo serikali imejidhatiti kutoa kwa watoto hawa?
Ushauri wangu, dhana ya Elimu bure ianzie kwenye elimu ya awali, elimu ambayo huwa ni msingi wa mengine yote yanayofuatia baada ya hapo na ambayo mtoto hufanya kama chanzo cha maarifa mengine.
Lakini pia, serikali ione utaratibu wa kuanzisha elimu amaalumu kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu:rasilimali ambayo itakuwa maalumu kwa ajili ya watoto. Hii ni kutokana kuwa, kwa rasilimali ambazo zinatoka vyuoni moja kwa moja naamini hazina uelewa halisi wa malezi kwa watoto wenye umri mdogo kama huu uliowekwa na serikali. Hivyo basi, ni vema kwa nia ya dhati kabisa serikali itabaini ni sehemu gani mahsusi kwa ajili ya kuzalisha rasilimali watu ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha na kuanzisha msingi imara katika taaluma ya mtoto.
Itaendelea…

Chapisha Maoni

0 Maoni