NADHARIA YA UTUMBUAJI MAJIIPU, MBONA HAYA HAYAJATUMBULIWA?

Leo hii chombo cha habari kikipitisha siku hakijataja habari za kutumbua majipu, basi hicho chombo kipo nchi nyingine na si Tanzania. H.E JPM utasikia leo yupo Muhimbili, majipu mawili yatumbuliwa, basi siku hiyohiyo utasikia Mwigulu naye yupo Butcher anatumbua majipu,  wakati huohuo pia Kigwangala naye keshafunga geti
hospitalini kuzuia wafanyakazi wachelewaji, Bashe naye anatumbua jipu kule hospitali nyingine...yaani full majipu.

Wafanya kazi hewa nao wanachukua sura mpya kila leo, wakati huo Kilango naye kwa kufikri bado yupo kwenye utawala wa kutabasamu anaficha majipu, huku napo mfanyakazi wa serikali yupo Ujapani kwa miaka 13 anapiga kitabu, sijui anasoma nini, huku nako Makonda anasainisha mkataba wa makubaliano juu ya watendaji kuajibika wanapogundulika  kuwa wamelea wafanya kazi hewa, yaani ni vurugu tupu.

Sijayasikia haya, kwamba mkurugenzi wa TANROADS atumbuliwa kwa kujenga barabara iliyo chini ya kiwango. Sijasikia kabisa juu kesi za barabara ambazo Mhe. mwenyewe ndiko alikotoka, sasa sijui nisemeje hapa, napata kigugumizi pia kama alivyopata Mhe. yule wakati wa kumuachisha kazi mama Tiba.

Sijasikia pia Chenge atumbuliwa kwa ubadhilifu wa fedha za umma kwa muavuli wa zawadi toka kwa Rugemalila. Hapa napo najiuliza sana, ni lini Chenge naye ataingia kwenye orodha ya waliotumbuliwa kwa ujasiri wa JPM? Naendelea kusubiri, ikumbukwe pia kwa sasa ni mwenyekiti wa Bunge, sijui ndiyo kawekwa pale  ili atumie elimu yake toka Havard ili kuifanya sheria iwe na kutu kwa mabosi wale...mimi na wewe hatujui.

Natamani pia kusikia jipu kubwa latumbuliwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma kwenda Marekani kufanya upasuaji wa ajabuajabu wakati Mwananyamala, Bugando na Muhimbili tunao wataalamu lukuki wa kufanya hiyo kazi, tena wazawa wa kwetu, yaani sijui ni lini hilii jipu litaiva, au labda haliguswi kwa sababu ni laini, sijui!

Namani pia kusikia jipu latumbuliwa lililoshiriki kumpiga Mzee Warioba wakati wa kukabidhi rasimu ya katiba mpya, nalo hili jipu sijui halijaiva, au kwa sababu Mzee naye alikaa kimya ili mwanae apate mkate, sijui.

Tetesi za kuaminika pia ni kwamba, aliyekuwa Gavana wa benki kuu Daudi Balali kumbe hajafa na hadi leo yupo tu huko kwenye mtaa wa kistaarabu, sasa hili jipu lililohusika na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) sijui nalo halijaiva, maana Chacha Wangwe alipofungua mdomo kusema kuwa kamuona Balali, hatujui naye alikufaje, sasa sijui hili limeiva, au bado ni kaupele tu.

TUMBUA MAJIPU, ILA HAYA NAHISI YASISAHAULIKE...

Chapisha Maoni

0 Maoni