Ndege za bombardier zaanza safari Mwanza-Dar

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limezindua rasmi safari za ndege zake aina ya Bombardier Dash-8 Q 400 kati ya Dar es Salaam na Mwanza huku viongozi wa Serikali wakiwataka Watanzania kutanguliza uzalendo kwanza kwa kuthamini vitu vyao kukuza uchumi wa shirika hilo.


Uzinduzi huo ulifanyika juzi baada ya ndege hiyo kuwasili Mwanza kwa mara ya kwanza saa 10.45 jioni ikiwa na abiria zaidi ya 90 waliokuwa wamefuatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Leonard Chamriho na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella wajumbe wa bodi ya ATCL.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Chamriho alisema safari za ndege hizo kwenda Mwanza ni moja ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk. John Magufuli wakati wa kampeni na kwamba ATCL itaendelea kuimaraika ikiwa Watanzania watatanguliza uzalendo kwa kupanda ndege hiyo.

Alisema Serikali imetoa maelekezo kwa ATCL kuhakikisha inakuwa na ushindani na kampuni znyingine kwa kuweka bei nafuu inayoendana na kipato cha watanzania.

Chamriho alisema ununuzi wa ndege nyingine zilizoahidiwa kuongezwa itategemea ufanisi utakaokuwapo.

“Rais Magufuli amekusudia kurejesha heshima ya ATCL, sote tunajua kwamba Mwanza kuna vivutio vingine na ndiyo mkoa ambao unawarahisishia wageni kufika kwenye mbuga zetu za Serengeti.

“Tumefanya uchunguzi na kubaini wakazi wa Kanda ya Ziwa wana mwamko na usafiri angani, ndege zote zinazotoka huku na kwenda Dar es Salaam huwa zimejaza abiria.

“Huu ni uwekezaji sahihi nawaombeni bodi na menejimenti ya ATCL hakikisheni mnazingatia ushindani unaekwenda sambamba na utendaji wenye maadili mema, tunajua kuna changamoto zimejitokeza za kuchelewa.

“Zifanyieni kazi haraka, toeni vinywaji kwa abiria na kauli za ukarimu kupata wateja wengi.

“Naomba niseme kwamba baada ya wiki moja ndege hizo zitafanya safari kati ya Mwanza na Bukoba, Tabora na Kigoma na tutakuwa tunaongeza safari nyingine kulingana na mahitaji lakini kikubwa nasisitiza mapato yadhibitiwe yasipotee kupitia mikono ya wachache,”alisema.

Chapisha Maoni

0 Maoni