MTOTO anayesadikiwa kuwa na umri kati ya miaka 15-17 amefunga Mtaa wa
Mecco, Kata ya Nyakato wilayani Nyamagana, Mwanza kwa kupiga risasi
hewani na kusababisha taharuki kubwa kwa wafanyabiashara na Wananchi.
Tukio la kijana huyo ‘kufunga mtaa’ limetokea usiku wa jana saa 1:45
katika Mtaa wa Mecco stendi, baada ya (kijana) huyo kutaka kupora katika
duka moja linalouza mtungi ya gesi na vifaa vingine.
Hata hivyo, katika mapambano ya wawili hao, kijana huyo alianza kupiga
kelele zilizosikika, ‘niachieni, niachie’ huku mfannyakazi wa duka hilo
akiomba omba msaada kwa watu waliokuwa karibu na duka hilo.
Baada ya watu kufika huku mfanyakazi wa duka hilo, akiita ‘mwizi mwizi,’ watu walifika na kumshika kijana huyo.
Kijana huyo aliwaponyoka na kutoa silaha iliyokuwa kwenye begi na kupiga
risasi moja hewani kuwatawanya watu waliokuwa eneo hilo.
Pia baada ya kijana huyo kupiga risasi hiyo, gari ndogo nyeupe ilifika
na kumchukua na kutokomea kusikojulikana, kitendo hicho kilisababisha
wananchi wa eneo hilo kupigwa butwaa.
Daud Machota, mmoja wa Wananchi wa eneo hilo amesema kuwa, vitendo vya
uhalifu katika eneo hilo vimeanza kutishia amani kwani kumesababisha
watu wengi kulala mapema.
“Kwanza mimi ninachoshangaa inakuaje mtoto mdogo wa miaka 15 – 17
anashika silaha na kupiga risasi hewani, labda hawa watoto wanaweza
wakawa wamefunzwa mafunzo ya kigaidi, haiwezekani kwa umri wake kufanya
hivyo,” amesema Machota.
Machota amesema kuwa, kijana huyo alifanikiwa kuchukua kiasi cha Sh. 40,
000 kwenye duka hilo, huku akidai kwamba uhalifu huo unasababishwa na
ugumu wa maisha unaonekana kuwagusa watu wengi.
Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza na Naibu Kamishna wa
Polisi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akidai kuwa, askari
walikuta katika eneo la tukio begi na shati moja.
“Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika uhalifu huo, tunaendelea na uchunguzi
kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo, ilipigwa risasi moja hewani,”
amesema Msangi.
Vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha za moto katika kipindi cha hivi
karibuni, vimeshamiri jijini humo na kusababisha wananchi na
wafanyabiashara wa maduka, kuishi kwa hofu.
Tarehe 31 Novemba mwaka huu matukio mawili ya uhalifu wa kutumia silaha
za moto yalifanyika kwa wakati tofauti na kusababisha watu wawili
kujeruhiwa na kuporwa fedha kiasi cha Sh. 1.2 Milioni katika Mgahawa wa
The Dinners.
Kashamiri kwa matukio hayo kumesababisha baadhi ya watu jijini humo
kulaumu vyombo vya usalama kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.


0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA