JPM atoa msaada kwa wazee wasiojiweza Kigoma

RAIS John Magufuli amekabidhi msaada wa vyakula mbalimbali na juisi kwa kituo cha wazee wasiojiweza (SILABU) cha mjini Kigoma ikiwa ni kutoa mkono wa sikukuu kwa watu wasiojiweza.
Msaada huo umekabidhiwa kwa wazee hao kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Emmanuel Maganga.Alisema msaada huo umetolewa kuwawezesha wazee hao kusherehekea sikukuu ya Krismasi sawa na watu wengine wenye uwezo.
Miongoni mwa vyakula vilivyokabidhiwa ni pamoja na kilo 90 za mchele, mafuta ya kula ndoo tatu na mbuzi mmoja kwa ajili ya kitoweo.
Maganga naye alitoa katoni tano za juisi na miche 24 ya sabuni. Mwenyekiti wa kambi hiyo, Hamisi Sabuni amemshukuru Rais Magufuli kwa msaada huo, akisema tangu aingie madarakani ameonesha dhamira ya dhati ya kuwajali watu wasiojiweza na wenye kipato duni.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mfawidhi wa Mkoa Kigoma, Heradius Mushi alisema pamoja na serikali kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia chakula kituoni hapo, bado kiasi cha fedha kinachotolewa hakikidhi mahitaji na kuomba wahisani zaidi wajitokeze si tu nyakati za sikukuu, bali mara kwa mara.

Chapisha Maoni

0 Maoni