Jumla ya watoto 61 wamezaliwa siku ya krismasi

Dar es Salaam. Watoto 61 wamezaliwa katika hospitali nne jijini hapa wakati wa mkesha wa Sikukuu ya Krismasi, kati yao wa kiume wakiwa 36 na wa kike 25.


Takwimu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zimeeleza watoto tisa walizaliwa hospitalini hapo, kati yao wa kiume ni watano na wa kike wanne. Katika Hospitali ya Amana, walizaliwa watoto 28, wa kiume wakiwa 16 na wa kike 12, huku watano wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.

Hospitali ya Mwananyamala walizaliwa watoto 16 kati yao wa kiume wakiwa wanane na wa kike wanane, mtoto mmoja akizaliwa kwa njia ya upasuaji; huku watoto wanane, wa kike saba na wa kiume mmoja walizaliwa kwenye Hospitali ya Temeke.

Ofisa muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Amana, Theresia Akida alisema watoto waliozaliwa hospitalini hapo wana afya njema na wanaendelea vizuri.

Katika Hospitali ya Temeke, Ofisa Muuguzi Hamisa Shaabani, alisema kati ya watoto wanane waliozaliwa, kuna pacha. Alisema hali za watoto na wazazi zilikuwa njema na waliruhusiwa kutoka hospitalini.

Chapisha Maoni

0 Maoni