Vijana wenye msimamo mkali wa USARF (Mlimani) walitimkia wapi?


Ndugu zangu,
Born Again Pagan kama anavyopendwa kuitwa ni mmoja wa Wanazuoni waliokuwepo pale Chuo Kikuu Dar es Salamm enzi hizo. BAP- Born Again Pagan, ambaye ni mwanachama wa miaka mingi wa mtandao wa Mjengwablog ana kumbukumbu nyingi za wakati huo. Alisoma Chuo Kikuu akiwa na watu wa aina a Yoweri Museveni. 

Kwenye simulizi aliyopata kusimulia kwenye mtandao wa Mjengwablog, BAP  anawazungumzia Vijana wa msimamo mkali walipohitimu Machi, 1970. Kwamba  walitawanyika na walitokea Tanzania, Uganda, Kenya na hata Guinea.
Yoweri Kaguta Museveni alikwenda kufanyakazi Ikulu ya Uganda chini ya Rais Milton Obote. Na wakati Idi Amin anampindua Rais Obote, Museveni alirudi Tanzania kufundisha hapo Chuo cha Ushirika Moshi na hapo badaye kuanzisha chama chake cha ukombozi wa Uganda, Front for National Salvation (FRONASA) na wenzake waliokuwa nao hapo Mlimani.
Salim Msoma alikwenda kufundisha Elimu ya Siasa hapo Business College. Hirji alipelekwa kufanya kazi ya Afisa wa Wilaya, Sumbawanga. Kwa wakati huo kupelekwa Sumbawanga, tena wilayani, huenda kuna kitu alimkorofisha Julius Nyerere.

Hirji huyu ameonekana majuzi kwenye kongamano la kumuenzi  Fidel Castro pale Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Wanaharakati wengine wa enzi hizo waliokuwepo kwenye tukio hilo ni  pamoja na Salim Msoma, Issa Shivji na Jenerali Ulimwengu.
Henry Mapolu  alikwenda kufanya kazi Kiwanda cha Urafiki. Ali Mchumo alikwenda kuwa mwana-sheria wa Jeshi la Kujenga Taifa. Huyu Ali Mchumo kuna mahali huwa nakutana naye. Hata majuzi tu nilimwona. Napanga kufanya mazungumzo naye ya kina juu ya wakati wao pale Mlimani.
Charles Kileo alijiunga na TANU hadi kuwa Mkuu wa Mkoa Mtwara. Emily Ndonde  alijiunga na Ikulu.
Simulizi itaendelea...

Chapisha Maoni

0 Maoni