Waziri mkuu atoa katazo walimu kuishi mbali na shule

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza walimu wanaoishi mbali na shule wakati shule zao zina majengo wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.

Amesema haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.
Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.
“Nimeambiwa kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,” amesisitiza.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.

Chapisha Maoni

0 Maoni