Jamhuri yamkatia rufani Rugemalira


UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayomkabili mfanyabiashara James Rugemalira na mwenzake ya kutakatisha fedha, umeiomba Mahakama ya Rufani Tanzania kutupilia mbali maombi matatu ikiwamo kubadili taarifa ya kusudio lake la kukata rufani.


Kadhalika, Rugemalira ameiomba mahakama kumruhusu kumwongeza mfanyabiashara Harbinder Sethi kama mtu muhimu kwenye kesi hiyo na ombi la tatu ni kumpa dhamana wakati anasubiri kusikilizwa maombi yake.

Pingamizi hilo la awali la Jamhuri lilisikilizwa katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Mwenyekiti Bernard Luanda, akisaidiana na Batwell Mmila na Gerard Ndika.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na jopo la Mawakili wa Serikali Wakuu, Dk. Zainabu Mango, akisaidiana na Peter Maugo, Tumaini Kweka na Wakili wa Serikali Elizabeth Mkunde.

Dk. Mango alidai kuwa upande wa Jamhuri unapinga maombi ya Rugemalira kwa kuwa vifungu alivyotumia havionyeshi kama vinahusu kesi za madai, jinai au mtu aliyekutwa na hatia.

Alidai kuwa vifungu alivyotumia vimeshindwa kuielekeza mahakama nini mshtakiwa anaomba na kwamba vimejumuishwa bila kufafanua kila kifungu matakwa yake dhidi ya maombi yake.

"Watukufu majaji, kama mshtakiwa aliona kuna haja ya kuungana na mshtakiwa Sethi katika rufani ama maombi haya alitakiwa kuunganisha Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa, ili wawasilishe maombi yaliyoko mbele yenu kwa pamoja..." alidai Dk. Mango wakati akiwasilisha hoja za pingamizi la awali.

Upande huo wa Jamhuri uliomba mahakana kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa hayana mashiko kisheria.

Hata hivyo, Rugemalira ambaye ana mawakili wanane wanaomtetea katika kesi hiyo, aliiomba mahakama kusimama na kujibu hoja za Jamhuri yeye mwenyewe na kuomba mawakili hao kukaa kando, Jopo hilo liliridhia maombi ya mshtakiwa na alidai kuwa pingamizi la Jamhuri haliko sahihi.

"Watukufu majaji, pingamizi la awali la Jamhuri halina mashiko kisheria... Hoja zao hazina ufafanuzi mahakama itupilie mbali," alidai mshtakiwa huyo.

"Maombi yangu yako sahihi kisheria na mahakama hii ina mamlaka; naomba yasikilizwe." Jaji Luanda baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alisema mahakama yake itazijulisha tarehe ya kutoa uamuzi.

Katika kesi ya msingi, Rugemalira na mfanyabiashara  Sethi wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. bilioni 309.

Kesi hiyo inasikilizwa usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na itatajwa tena Machi 16 na washtakiwa wanaendelea kukaa mahabusu.

Chapisha Maoni

0 Maoni