Rais Magufuli atoa kibali kuendeleza Msikiti


Uongozi wa Waislamu Mkoani Rukwa umepokea kwa furaha mchango wa Milioni 5.7 uliotolewa na uongozi wa serikali ya Mkoa huo ukiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo katika kikao cha maridhiano juu ya ujenzi wa msikiti uliosimama kwa muda.

Fedha hizo zilizochangwa zilijumuisha ahadi, fedha taslimu pamoja na vifaa vya ujenzi vilivyotolewa kwa umoja wa viongozi wa serikali kuonesha mshikamano uliopo kati ya serikali na wananchi bila ya kujali itikadi, dini wala rangi huku Mhe. Wangabo akichangia milioni 1.5.

Kabla ya maridhiano hayo Mhe. Wangabo alitoa salamu za Rais Dkt. John Pombe Magufuli juu ya kuendeleza msikiti huo na kunukuu kuwa Rais ametoa kibali cha kuuendeleza msikiti huo na yupo tayari kuweka jiwe la msingi ama kuuzindua msikiti huo.

"Mhe. Rais ameniagiza niseme yafuatayo kuwa ametoa kibali cha kuendelea kujenga msikiti huu hadi umalizike, ameyafikiria mambo mengi sana mpaka kuja kufikia maamuzi haya, ili yalete mustakabali wa maridhiano, amani, utulivu, mshikamano, maelewano na umoja ili Rukwa yetu iweze kusonga mbele kama kitu kimoja. Pia amesema kuwa yupo tayari kuweka jiwe la msingi ama la kuzindua msikiti huu", amesema Wangabo.


Pamoja na hayo, Wangabo ameendelea kwa kusema "nauomba uongozi wa uislamu mkoa kuendelea kushirikiana na kudumisha amani na kuhakikisha wanajenga Rukwa moja isiyoyumbishwa na tofauti yoyote kwani ushirikiano huo umekuwa wa muda mrefu hivyo nisingependa pawepo na tofauti".


Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa na kumtaka kamishna wa ardhi nyanda za juu kusini kufanya haraka kupitisha kibali ili msikiti huo upatiwe hati.

Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa mkoa wa Rukwa Rashid Akilimali amesifu maamuzi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kukubali ombi lake la kutaka kuja kuweka jiwe la msingi ama kuuzindua msikiti huo na kuwa waislamu wataendelea kuungana nae na kumuombea amalize vipindi vyake salama.

Chapisha Maoni

0 Maoni