MTOTO wa Mbunge wa Mbarali, Haroon Mulla (CCM), ametiwa nguvuni kwa
tuhuma za kukutwa na meno ya tembo pamoja na nyama ya pori kinyume cha
sheria.
Tukio hilo lilitokea jana wilayani Mbarali ambapo mtoto wa mbunge huyo
alikamatwa na shehena ya meno ya tembo pamoja na nyama hiyo ambayo
haijajulikana kiasi chake.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya vyombo vya dola mkoani hapa,
kilimbia MTANZANIA kuwa baada ya tukio hilo maofisa wa Serikali pamoja
na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) walimtia mbaroni mtu
huyo ambapo hadi tunakwenda mitamboni walikuwa wakiendelea na mahojiano
kwa lengo la kubaini mtandao wa ujangili anaoshirikiana nao.
“Ukitaka kufahamu nani mmiliki halali wa biashara hiyo baba au mtoto,
tungependa Serikali ifuatilie silaha alizokutwa nazo mtuhumiwa, kwani
hapo ndiyo ukweli utajulikana, Serikali imekuwa ikiingia hasara
kutokana na kuuawa kwa tembo, hivyo ni vema suala hili likachunguzwa kwa
kina,” alisema mtoa habari wetu.
Chanzo hicho kilisema kuwa familia hiyo imekuwa ikihusishwa na tuhuma za
ujangili pamoja na kufanya biashara ya meno ya tembo kwa miaka mingi.
Kutokana na taarifa hiyo MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya, Dhahiri Kidavashari, ambaye alikiri kukamatwa kwa watu hao, huku
akisema walikamatwa na askari wa Tanapa.
“Mtuhumiwa bado yupo kwenye mikono ya Tanapa hivyo kwa sasa siwezi
kuzungumzia suala hili. Kwani operesheni hii inaendeshwa na Tanapa
wenyewe.
“…na huyo mtu yupo mikononi mwao mimi siwezi kulizungumzia ila
watakapomfikisha kwetu, ndiyo nitatolea taarifa kwa sasa sina uwezo
nalo,” alisema Kamanda Kidavashari.
Kutokana na hali hiyo MTANZANI ilipomtafuta Meneja Mawasiliano wa
Tanapa, Pascal Shelutete ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo akiri
kukamatwa kwa mtoto huyo wa mbunge na kueleza kuwa wanaendelea na
uchunguzi.
“Ni kweli tunamshikilia mtuhumiwa na tunaendelea naye na uchunguzi na ukikamilika tutatoa taarifa kwa umma,” alisema.
MTANZANIA lilipomtafuta mbunge huyo ili kuzungumzia taarifa za mtoto
wake kuhusishwa na mtandao wa ujangili, hakuweza kupatikana kutokanana
simu yake ya mkononi kuita bila kupokewa.
“Mheshimiwa salaam, kuna taarifa za mtoto wako kukamatwa kwa tuhuma za
ujangili wilayani Mbarali, je ni kweli?,” ulieleza ujumbe huo ambao
hakuujibu hadi tunakwenda mitamboni. Hata hivyo hivyo jitihada za
kumpata mbunge huyo zinaendelea.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA