Ofisi ya CAG yatilia shaka ulaji wa sh. mil.775 kila eka NSSF



Kufuatia taarifa hiyo, wabunge kupitia Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) walikuja juu na kuubana uongozi wa NSSF, wakitaka maelezo ya kina kuhusiana na suala hilo walilodai lina harufu ya ufisadi.

Wakati ikipitia taarifa ya CAG, kamati hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Naghenjwa Kaboyoka, ilibaini kuwa katika mradi wa NSSF kuendeleza mji wa kisasa wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ambao shirika hilo limeingia ubia na taasisi nyingine, thamani ya kiwanja kimoja iliyowekwa ni Sh. milioni 800 wakati thamani halisi ni Sh. milioni 25, hivyo kuwapo na malipo ya ziada ya Sh. milioni 775 kwa kila kiwanja.

PAC ilifichua ulaji huo wakati ikiibana NSSF kwa kutaka ufafanuzi kuhusu hoja mbalimbali za ukaguzi zilizoainishwa na CAG katika mwaka wa fedha 2014/15.

Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka, alisema kuwa watalieleza Bunge kuhusu harufu ya ufisadi katika mradi huo wa NSSF katika kuendeleza mji wa Kigamboni.

Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige (CCM), alidai mradi huo umegubikwa na 'uchafu' kutokana na kile kilichofanyika .

Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim Ali (CCM), alisema kuna taarifa kwamba mbia, ambaye ni kampuni ya Azimio Housing Estates, kuwa anataka kukopa tena wakati kuna fedha za uwekezaji hazijaingizwa kwenye mradi.

Ali alidai pia kuwa, kuna mgongano wa maslahi kutokana na kampuni hiyo kuonekana ikipewa kazi nyingi na NSSF.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, alisema taarifa zao zinaonyesha mbia huyo yupo tayari kuingiza fedha kwenye uwekezaji huo lakini anataka akope, hivyo kuna uwezekano wa NSSF kupoteza Sh. bilioni 270 ambazo zimeingizwa kwenye uwekezaji huo kama isipokuwa makini kuangalia namna ya kuzirudisha.

Katika ripoti ya CAG ya 2014/15, inaelezwa kuwa NSSF iliingia ubia na kampuni hiyo na kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Builders Limited.

Ilielezwa kuwa katika mkataba huo wa mradi wa Kigamboni, Azimio Housing Estates inatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni lakini baada ya tathmini, PAC imebaini zipo ekari 3,503 tu.

Katika ubia huo, NSSF inamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estates inamiliki asilimia 55 ya hisa na jumla ya gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 653.44.

Aidha, inaelezwa kuwa utaratibu wa uchangiaji mtaji ni NSSF kutoa fedha kwa asilimia 45 ya gharama za mradi na Azimio kutoa fedha zenye thamani ya asilimia 35 ya gharama za mradi pamoja na ardhi ambayo itathaminishwa kuwa asilimia 20 ya gharama za mradi.

Hata hivyo, wajumbe wa PAC walishangazwa na uthamini uliofanywa kwenye ardhi wakieleza kuwa gharama imeonekana ni kubwa kuliko gharama halisi.

Ripoti ya CAG inaeleza kuwa katika makubaliano ya usitishwaji, kiasi cha Sh. bilioni 43.9 ilicholipwa Azimio na shirika ni sehemu ya ada ya ushauri ambayo inabadilishwa kuwa mkopo utakaorejeshwa na kampuni kupitia sehemu ya mauzo ya nyumba katika mradi wa Dege ndani ya miaka mitatu, kwa riba ya asilimia tatu kwa mwaka.

Akijibu hoja za wabunge, Mkurugenzi wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara, alisema utekelezaji wa mradi wa Dege ulisimama tangu Februari mwaka huu kutokana na mwekezaji kutokuwa na fedha huku NSSF tayari ikiwa imeshaingiza Sh. bilioni 270.

Hata hivyo, alisema kuna ukaguzi maalumu unafanyika kwenye miradi yote ya NSSF ukiwamo huo wa Kigamboni.

“Tukitoka kwenye ubia huu, tunaweza kupoteza fedha hizo… tupo makini kuhakikisha mwekezaji huyo (Azimio) anarejesha fedha hizo,” alisema Mkurugenzi huyo.

Prof. Kahyarara alikiri Azimio kupeleka barua kwa NSSF ikitaka kukopa na ilikataliwa kupewa mkopo huo kwa sababu inadaiwa na haiwezi kukopeshwa tena.

Alisema sehemu kubwa ya ardhi imenunuliwa na NSSF kwa bei kubwa tofauti na uhalisia na kuna uchunguzi unafanywa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) huku akisema hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi wale wote waliohusika na mkataba wa mradi huo.

UTATA MIKOPO SACCOS
Katika hatua nyingine, PAC imemuagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu wa mikopo yote iliyotolewa na NSSF baada ya kubaini kuwa Saccos ya Bumbuli Development Corporation imepatiwa mkopo usio wa kawaida wa Sh. bilioni 2.4 ndani ya mwaka mmoja.

Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka, alisema juzi kuwa kamati yake ilishtushwa na kumuagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu wa fedha za Saccos ya Bumbuli.

Alisema suala la Saccos ya Bumbuli kupatiwa kiasi hicho kikubwa cha fedha, limewashtua wajumbe wa kamati hiyo na kujiuliza imekuwaje ipate fedha nyingi katika kipindi hicho kifupi huku ikipewa tena fedha nyingine na kufanya deni kufikia Sh. bilioni 2.4 ndani ya mwaka mmoja.

“CAG afanye ukaguzi kwenye Saccos maana haijulikani kama fedha walizopewa awali zimerudishwa au la,” alisema Mwenyekiti huyo.

Kaboyoka aliongeza kuwa maelekezo mengine yatatolewa bungeni kwa mujibu wa Kanuni ya 117(10) katika kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, inayoipa mamlaka kamati hiyo kuwasilisha taarifa bungeni kuhusu hesabu za serikali.

Awali, wakati wakichangia mapitio ya hesabu za NSSF, wajumbe wa kamati hiyo walionyesha kushtushwa na jinsi Saccos hiyo ilivyopewa mabilioni ya shilingi kwa zaidi ya mara moja ndani ya muda huo mfupi.

Mbunge wa Viti maalumu, Tunza Malapo (Chadema), alihoji kama NSSF imefanya uhakiki na kujiridhisha juu ya uwapo wa Saccos hiyo ya Bumbuli.

Mbunge wa Kilindi, Omar Kigua (CCM), alihoji vigezo vilivyotumika mpaka Saccos moja kupewa mkopo mara tatu ndani ya mwaka mmoja.

Alisema NSSF imetoa mikopo kwa Saccos tisa, kwa kiasi kinachozidi asilimia 50 ya thamani ya mali za Saccoss, husika kinyume cha sera ya kukopesha ya shirika na limeomba kiasi ambacho hakikustahili kutolewa.

Katika ripoti ya CAG, mbali na Bumbuli, Saccos zingine zilizopatiwa fedha nyingi kinyume cha utaratibu ni Korongo Amcos Saccos, UMMA Saccos, SBC Saccos Ltd, Hekima Saccos, Ukombozi Saccos Ltd, Uzinza Saccos Ltd, Harbour Saccos na Umoja Saccos.

Akizungumzia suala hilo la Saccos, Mkurugenzi wa NSSF, Prof. Kahyarara, alisema ukaguzi wa awali uliofanywa, umebaini ni kweli kuna Saccos zilikuwa hazionekani huku kwenye vitabu zikiorodheshwa kuwa zimekopeshwa.

Aidha, alisema kuna wadaiwa wengine wamejitokeza na kupeleka fedha wenyewe, na ambao awali walikuwa hawajulikani.

Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Prof. Samwel Wangwe, alisema hivi sasa bodi imesimamisha mikopo kwa Saccos hadi uchunguzi ukamilike na baada ya hapo utawekwa utaratibu mpya wa utoaji mikopo.
 

Chapisha Maoni

0 Maoni