Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema amefurahishwa na uamuzi wa Kanisa Katoliki
na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wa kutafuta viwanja Dodoma ili
wajenge ofisi za makao yao makuu pamoja na makazi ya viongozi wao wakuu.
Alitoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Oktoba 27, 2016) wakati akizungumza na Askofu
Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Katoliki la Dodoma pamoja na Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC), Bw. Peter
Maduki ofisini kwake mtaa wa Railway, mjini Dodoma.
“Sina shaka juu ya maombi yenu ya kupatiwa viwanja kwa ajili ya ujenzi
wa makao makuu pamoja na makazi ya viongozi wakuu. Sasa hivi Master Plan
ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi inapitiwa upya ili izingatie
mahitaji ya msingi sababu zamani ilikuwa haijapangwa kwa mazingira ya
sasa ya ujio wa Serikali,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema wiki tatu zilizopita alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ili atafute makampuni yenye uwezo wa
kupima viwanja kwa haraka. “Hii itatusaidia kutambua tuna eneo kiasi
gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana
na mahitaji yake,” ameongeza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyashukuru makanisa kwa huduma za kijamii
zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama ambavyo
ameshuhudia katika baadhi ya maeneo alikopita hapa nchini.
Pia amewakubalia ombi lao la kuwa na kikao cha pamoja baina ya watendaji
wa Serikali na makanisa ambacho kitajadili namna ya kuimarisha ubia
katika utoaji wa huduma za kijamii hususan za afya na elimu.
Mapema, Baba Askofu Mkuu Kinyaiya alimweleza Waziri Mkuu kwamba
wanahitaji eneo la kujenga ofisi za makao makuu na makazi kwa ajili ya
kanisa hilo pamoja na makanisa yaliyo chini ya CCT ambayo kwa pamoja
yanaunda Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC). Alisema
wanahitaji eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi wa Baba
Mtakatifu.
Alisema walipowasilisha maombi yao CDA, waliahidiwa kupatiwa eneo la makazi tu lakini bado wanahitaji eneo la ofisi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Maduki alisema katika sekta ya
afya hadi kufikia Juni 2016, makanisa yalikuwa yanamiliki na kuendesha
hospitali 102, vituo vya afya 102 na zahanati 696. “Kati ya hospitali
102, mbili ni za rufaa za kanda na 38 ni za hospitali teule za
Halmashauri za Wilaya na hospitali nyingine 62 zinatoa huduma
halmashauri mbalimbali,” alisema.
Alisema karibu asilimia 38 ya hospitali hapa nchini zinamilikiwa na
makanisa na nyingi ziko maeneo ya vijijini. Pia alisema kuna chuo kikuu
kimoja, vyuo vikuu vishiriki vitatu, na vyuo vya mafunzo ya kati 62
ambavyo vinatoa kozi za uuguzi, maabara na ufamasia.
Kuhusu
sekta ya elimu, Bw. Maduki alisema makanisa yanatoa elimu kuanzia elimu
ya awali hadi chuo kikuu na kwamba hadi kufikia Juni, 2016, makanisa
yalikuwa na shuke za msingi 161, za sekondari 369, na vyuo vya ufundi
stadi 126. “Pia tuna vyuo vya ualimu 14, vyuo vikuu tisa, vyuo vikuu
vishiriki 17 na vituo vya vyuo vikuu saba,” alisema
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA