TAARIFA YA UFAFANUZI KWA UMMA KUHUSU TAARIFA ILIYOSAMBAZWA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII YA KUDHALILISHWA KWA MWALIMU WA SEKONDARI YA SHILALO TAREHE 17 OKTOBA,2016.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Eliurd Mwaiteleke anapenda kuwataarifu Wananchi wote na Umma kwa ujumla kuhusu taarifa iliyosambazwa kwenye Mitandao ya Kijamii tarehe 17 0ktoba,2016 kuhusiana na kitendo cha Udhalilishaji wa Mwalimu mmoja katika Shule ya Sekondari Shilalo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi
.

Hivyo,kutokana na taarifa hiyo ilizosambazwa kwenye mitandao ya Kijamii yenye kichwa cha habari,”MKURUGENZI MISUNGWI AMWAMURU MWALIMU APIGE DEKI MBELE YA WANAFUNZI”ambayo ilieleza kuwa Mkurugenzi huyo alimuamrisha Mwalimu kudeki darasa huku wanafunzi wake wakimshuhudia ambapo wanafunzi hao wa kidato cha nne walikuwa wakijisomea kwa ajili ya maandalizi ya Mitihani,kwa mujibu wa taarifa rasmi kuhusiana na hali Halisi katika tukio hilo taarifa iliyotolewa ya kwamba alimuamrisha kudeki darasa si ya kweli kutokana na sababu na mambo yafuatayo:-

i/. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi alianza Ziara ya kikazi tarehe 4 oktoba,2016 katika Kata ya Mondo kwa lengo la kutoa Mwelekeo wa shughuli za Serikali ya awamu ya tano kwa Watendaji wa Kata na Vijiji na Wataalam wote wa Ngazi ya kata na vijiji pamoja na mambo mengine ikiwa ni kukagua utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo vijijini iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2013/2014- mwaka 2015/2016 pia aliambatanana na baadhi ya Wataalamu wa Idara na Vitengo mbalimbali vya Halmashauri,ambapo alifanya kikao cha ndani pamoja na Uongozi wa Kata na kutembelea katika taasisi za Elimu, Maji, barabara, Kilimo, Mapato na Afya ambazo ni Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Zahanati na Vituo vya Afya.

Kwa Mantiki hiyo, katika ziara hiyo alibaini baadhi ya Mafanikio makubwa yaliyoko kwenye miradi mbalimbali iliyopo vijijini na kupongeza juhudi zilizofanyika pamoja na hayo aliona Changamoto na kasoro katika baadhi ya Miradi na maeneo ya Kiutendaji kwa baadhi ya Watumishi wa umma ambao hawawajibiki ipasavyo na kutozingatia maadili ya Utumishi wa umma

Mfano: 
Usafi wa Mazingira ya ndani na nje ya eneo la Taasisi, Madarasa, Vyoo na Mazingira, Kufanya kazi kwa bidii na Weledi,Kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni na Miongozo ya kazi.

Alitoa maelekezo ya jumla kwa Viongozi wa ngazi ya Kata kuwasimamia watendaji na Watumishi wote walioko chini yao ili kuleta tija na matokeo yanayonekana kwa muda mfupi,wa kati na mrefu na utoaji wa taarifa kwa wakati na kushauri mapema Miradi ambayo haitekelezwi kwa kiwango na ubora kulingana na thamani ya fedha

Mfano: 
Baadhi ya Majengo ya Nyumba katika Zahanati ya kijiji na shule ya Msingi Ntulya yameanza kubomoka na kuhatarisha maisha ya watu.

ii/. Katika Kata ya Shilalo alifanya Ziara tarehe 5 oktoba, 2016 na kutembelea na kukagua miradi na shughuli za Maendeleo katika maeneo ya Shule za Msingi 6, Sekondari ya Shilalo, Ujenzi wa Ofisi ya kata, Ujenzi wa Zahanati 3, Ujenzi wa Masjala ya Ardhi 2, Lambo la kunyweshea Mifugo na Uhamasishaji wa Michango ya CHF kwa jamii.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo aliwapongeza Viongozi na Wataalamu wa kata na vijiji kwa mafanikio hayo na kuwasihi waendelee na kasi hiyo ya maendeleo kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu pamoja na kuongeza bidii katika ukusanyaji wa Mapato kwa kutumia njia ya mashine za Kielektroniki.

iii/. Baadhi ya mambo yaliyobainika na kutolewa taarifa na watendaji na wataalamu wa kata hiyo katika kuboresha na kuimarisha utendaji kazi ni pamoja na Serikali kuongeza idadi ya wataalamu katka sekta ya Elimu na Afya na Vitendea kazi ikiwemo Usafiri, na kutoa fedha za kukamilisha miradi iliyoko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

iv/. Mkurugenzi Mtendaji Wilaya pamoja na Wataalamu kutoka wilayani na Wataalamu wa ngazi ya kata na vijiji walibaini na kushuhudia baadhi ya Changamoto mbalimbali zikiwemo, Uchafu wa Mazingira ya nje na ndani ya Madarasa 5 na Vyoo vya Walimu na wanafunzi katika Shule ya Sekondari Shilalo, hali ambayo haikuwafurahisha timu yote ilifika Shuleni hapo, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya alitoa Maelekezo kwa Walimu wote waliokuwepo kutimiza wajibu wao wa kuwasimamia kikamilifu wanafunzi kufanya Usafi na kutunza Mazingira ikiwemo usafi wa madarasa,vyoo na ofisi zao na kusisitiza Mwalimu wa darasa na wa Zamu kuwajibika katika majukumu yao kwa kuwasimamia wanafunzi kufanya usafi kwa ujumla kila siku pamoja na kudeki Madarasa yao angalau mara 2 kwa wiki na kupanda miti kupanda katika mazingira ya shule.

v/. Vile vile timu katika ukaguzi wake, ilibaini shule ya Msingi Mwamboku ikiwa na mazingira yenye uchafu uliokithiri hususan upande wa vyoo vya wanafunzi, hali ambayo wajumbe wote wa ziara waliona na kufedheheshwa na hali ya mazingira hayo hatarishi ya wanafunzi kujisaidia juu ya sakafu na nje ya jengo la choo, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya aligundua kuwa baadhi ya watendaji wanafanya kazi kwa mazoea na uzembe wa hali ya juu, kitendo ambacho kinaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa kama kichocho na kipindupindu.

Aidha, Mkurugenzi huyo alichukua hatua ya kumvua Madaraka ya Ualimu mkuu aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, na kuagiza abaki na nafasi ya Ualimu wa kawaida shuleni hapo.

vi/. Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya katika Majumuisho ya ziara aliwapa maelekezo ya jumla, na kuwataka wataalamu wote kuwa Waadilifu, kuwajibika na kufanya kazi kwa uzalendo.

Pia alisisitiza Maafisa watendaji wote Kata na vijiji kuhakikisha wanafanya usafi wa mazingira ya maeneo ya Taasisi zao na kusimamia wananchi katika kutekeleza Agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, John Pombe Magufuli la kufanya usafi kwenye maeneo yote, pamoja na Mkakati wa Mkoa na Wilaya uliowekwa wa kufanya usafi wa mazingira kwa kila Jumamos ya kila mwisho wa Mwezi.

vii/. Hivyo pamoja na maelekezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kwa wataalamu ngazi ya kata na vijiji kusisitiza uwajibikaji, vile vile Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu wakuu wameagizwa kutekeleza vyema majukumu yao ya kila siku na kuzingatia mpango kazi, kwa barua yenye kumb Na.MZA/MDC.F.10/63/13 ya tarehe 12/10/2016,iliyosainiwa na Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Misungwi.

Kutokana na sababu na maelezo hayo, yenye mantiki, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Misungwi katika ziara hiyo ya kikazi ameweza kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na miongozo ya Serikali inayosisitiza viongozi katika Maeneo yao kutembelea na kukagua shughuli zote za Mendeleo ikiwemo miradi mbalimbali na kutoa maelekezo na maagizo.

Pamoja na hayo, ziara yake inaendelea ambapo amepanga kutembelea kata 2 kila wiki na kukamilisha kata zote 27 za Wilaya ya Misungwi ifikapo mwezi Disemba, 2016.

Katika mwendelezo wa ziara hiyo tarehe 18 oktoba,2016 amefanya ziara katika kata ya Gulumungu na kutembelea Taasisi zote ndani ya kata na kubaini mabadiliko makubwa katika baadhi ya maelekezo na maagizo aliyoyatoa kwa kata alizotembelea awali ikiwemo na suala la usafi wa mazingira hususan katika usafi wa vyumba vya madarasa,vyoo na mazingira kwa ujumla pamoja na watumishi kuanza kubadilika kwa kuonyesha matokeo ya muda mfupi na hakusita kutoa pongezi kwa watendaji waliofanya vizuri na kwa ubunifu, na kuagiza Mwalimu mmoja wa shule ya Msingi Lukanga mwenye ubunifu katika sanaa ya uchongaji na uchoraji kuhamishiwa katika shule maalum ya Mitindo.

Kwa matukio zaidi ya picha Bofya chini.

View attachment 420587 
Picha inayoonyesha jengo la choo katika shule ya msingi Lukanga,Kata ya Gulumungu.Ikionyesha hali halisi ya usafi wa vyoo ulivyo kwa sasa baada ya kupokea maelekezo ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Misungwi.

sa.jpg

Jengo la choo cha shule ya msingi, Mwamboku likionyesha hali isiyoridhisha katika usafi wa mazingira na rafiki kwa matumizi ya wanafunzi ndani na nje.

Hali hiyo ilibainika baada ya ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Misungwi na kutoa maelekezo kwa shule zote kuzingatia usafi wa mazingira.Aidha alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha anawapima wanafunzi endapo wameambukizwa Magonjwa ya kuambukiza kama kichocho na Mengineyo na kutoa taarifa za kitabibu.

saw.jpg

Picha ya jengo la nyumba ya Mganga Mfawidhi katika zahanati ya kijiji cha Ntulya ikionyesha nyufa zilizokwisha jitokeza ikiwa ni miaka 2 tangu ifunguliwe na Mheshimiwa Rais wa awamu ya nne Dkt, Jakaya Kikwete mwaka 2013.

Hali inayoonyesha namna ya baadhi ya watendaji wasioweza kusimamia utekelezaji wa miradi na kutokuwa wazalendo kwa Taifa.

saww.jpg

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Misungwi, Eliud Mwaiteleke akitoa maelekezo ya kiutendaji kwa wataalamu wa Kata ya Shilalo katika kikao cha ndani kabla ya ukaguzi wa shughuli na Miradi ya Maendeleo kwenye taasisi za Kata hiyo. Walioketi kutoka kushoto ni Afisa mtendaji wa Kata, Mheshimiwa Diwani wa Kata ya hiyo Mayila Maguha, Kulia Mchumi Sylvia Rwehabura, akifuatiwa na Mwakilishi wa Mganga Mkuu Wilaya.

Picha zote na Thomas Lutego Misungwi.

Imetolewa na:

Thomas Lutego

Kaimu Afisa Habari na Mawasiliano (W)

MISUNGWI

18 Oktoba,2016

Chapisha Maoni

0 Maoni