Imetayarishwa na OTHMAN MASOUD OTHMAN
Nimefarajika sana kuona kwamba Wazanzibari wengi wamepata muamko mkubwa
kuhusiana na maslahi ya Zanzibar katika suala la kisiwa cha Latham
(Fungu Mbaraka). Hii ni faraja kwa vile Tanganyika wameonyesha nia ya
wazi, ya dhahiri na ovu katika kukichukua kwa nguvu kisiwa hichi kutoka
katika milki ya Zanzibar. Baada ya mwishoni mwa mwaka 2013 kuona kwamba
Tanganyika wamefika kutumia hata nguvu ya vyombo vya ulinzi kudai kuwa
kisiwa hichi ni cha Tanganyika na baada ya kuona baadhi ya
wataalamu wao
wanajenga hoja dhaifu kuwa kisiwa hichi ni cha Tanganyika, mimi binafsi
nilifanya utafiti wa kina juu ya umiliki wa Zanzibar kwa kisiwa hichi
na kuuwasilisha utafiti huo Serikalini. Baada ya Serikali kuridhika nao
ndipo Makamu wa Pili wa Rais alipomuandikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
juu ya msimamo wa Zanzibar katika umiliki wa kisiwa hicho. Hatimaye,
Waziri Mkuu naye akajibu kuwa kwa kumbukumbu zao, ambazo hakuziwasilisha
hata moja, kisiwa hicho ni cha Tanganyika.
Nimeona ni vyema niwasambazie MUHTASARI wa taarifa ya utafiti niliofanya
na ambao ndio uliowasilishwa kwa Mizengo Pinda. Naamini taarifa hii
itasaidia kuanika uovu wa Tanganyika kwa Zanzibar katika umiliki wa
kisiwa hicho. Aidha, utaweka bayana udhaifu wa baadhi ya viongozi wa
Zanzibar katika kusimamia maslahi ya Zanzibar.
1. UTANGULIZI
Kisiwa cha Latham au kwa jina jengine Fungu Mbaraka (au Fungu Kizimkazi)
kipo usawa wa kijiografia wa 6’ 54’ 5 S na 39’ 55’ 45’ E (Angalia
ramani katika ukurasa wa 2). Masafa kutoka Rasi ya Kizimkazi hadi katika
Kisiwa hichi ni maili 36 (kilomita 57.9) na masafa kutoka kusini mwa
Dar es salaam ni maili 37 (kilomita 59.5). Aidha, masafa ya karibu
kabisa baina ya kisiwa hicho na Tanzania Bara (sehemu za Kimbiji) ni
maili 23 na nusu. Kisiwa hichi kina urefu wa yadi 350 sawa na mita 320
na upana wa yadi 180 sawa na mita 164.5(kwa vipimo vya mwaka 1898).
Inaaminika kwamba kisiwa cha Latham kiliitwa jina hilo kutokana na meli
ya kiingereza iliyokuwa ikiitwa Latham ambayo ilitia nanga katika kisiwa
hicho mwaka 1758. Aidha, kinajulikana kwa jina la Fungu Mbaraka
kutokana na Bwana Ahmed Mbaraka ambaye alipewa ruhusa na Sultani kuzamia
katika mabaki ya meli iliyozama jirani na kisiwa hicho na akapata fedha
nyingi zilizomuwezesha kupata utajiri na kununua ardhi kubwa sehemu ya
Nyamanzi. Kisiwa hichi kina mnyanyuko wa futi 10 kutoka usawa wa bahari
na kinakaliwa na ndege tu hali iliyopelekea kuwa maarufu kwa samadi ya
ndege (guano) ambayo watu na makampuni kadhaa wamewahi kuomba kukitumia
au hata kwenda kukichukua bila ya ruhusa. Rasilimali hiyo ya samadi
nyingi ya ndege ni miongoni mwa mambo yaliyokipa umaarufu sana kisiwa
hichi hapo siku za nyuma.
2. HISTORIA YA UMILIKI
Kabla ya mikataba baina ya Waingereza na Wajerumani; ule wa 1886, 1888
na ule wa Heligoland wa mwaka 1890, kisiwa hicho kilikuwa chini ya
mamlaka ya Zanzibar bila ya ubishi wala utatanishi wowote. Mikataba hiyo
miwili ndiyo iliyozusha utatanishi kuhusu umiliki wa Zanzibar juu ya
kisiwa hicho. Sababu za utatanishi huo ni kama zifuatazo:
Ibara ya 1 ya Mkataba wa mwaka 1886, iliyatambua mamlaka ya Sultani wa
Zanzibar juu ya visiwa vya Zanzibar na Pemba na visiwa vidogo vidogo
ndani ya mzunguko wa meli 12. Kwa vile kisiwa cha Latham kipo umbali wa
maili 36, inafsirika kuwa hakikuwezi kuingia katika makubaliano ya ibara
hiyo ya 1 ya mkataba wa 1886;
b) Sababu ya pili ni kuwa kwa mujibu wa ibara ya XI ya Mkataba wa
Heligoland wa 1890, Ujerumani ilikubali kuyatambua mamlaka ya Sultani
juu ya visiwa vya Zanzibar na Pemba na mamlaka nyenginezo zilizobaki.
Ibara hiyo haikuweka wazi kama kisiwa cha Latham kilikuwa miongoni mwa
mamlaka hizo nyenginezo au la;
c) Sababu ya tatu ambayo iliongeza utatanishi ni kuwa mikataba yote
haikutoa mamlaka bayana kwa Wajerumani wala Waingereza juu ya kisiwa cha
Latham.
Hata hivyo, pamoja na utatanishi huo wa kimikataba, hakukuwahi kutokea
ubishani wowote au hoja yoyote juu uhalali wa umiliki wa Zanzibar kwa
kisiwa cha Latham k
ati ya mwaka 1886 hadi 1898.
3. UBISHANI JUU YA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM
Hoja ya nani mmiliki halali wa kisiwa cha Latham ilizuka mwaka 1898
baada ya kampuni moja iitwayo Messr Dawson & Company ya 9 & 10
Pancras Lane, Queen Victoria Street, London ilipoiandikia Wizara ya
Mambo ya Nje ya Uingereza kuulizia nani mmiliki halali wa kisiwa cha
Latham kati ya Ujerumani na Zanzibar. Baada ya kupata suala hilo, tarehe
19 August, 1898, Wizara ya Mambo ya Nje ilimuandikia Waziri Kiongozi wa
Sultani (First Minister) kutaka ufafanuzi wa jambo hilo. Balozi Mdogo
na Wakala wa Uingereza aliyekuwepo Zanzibar Sir Arthur H. Hardinge
alijibu barua hiyo tarehe 4 Oktoba, 1898. Katika barua yake alitoa
ufafanuzi juu ya kisiwa hicho na msimamo wa kisheria unaotokana na
mikataba ya 1886 na ule wa 1890. Hatimaye alihitimisha kwa kusema kuwa
kwa vyovyote vile kisiwa hicho hakiwezi kuwa cha Ujerumani. Hata hivyo,
alieleza pia utatanishi wa kisheria uliopo juu ya umiliki wa Zanzibar
pia.
Baada ya kujibu barua hiyo, Sir Arthur Hardinge mnamo tarehe 15 Oktoba,
1898 alimuandikia barua Sir Lloyd Mathews ambaye alikuwa Waziri Kiongozi
wa Sultani kutoa ufafanuzi zaidi na ushauri wake juu ya kisiwa cha
Latham. Katika barua yake alieleza kuwa chini ya mikataba yote miwili
kisiwa hicho hakiko chini ya mamlaka ya Ujerumani wala Uingereza. Aidha,
mikataba hiyo haikuweka bayana kuwa kiko chini ya mamlaka ya Sultani.
Hivyo, alishauri kuwa kisheria kisiwa hicho si ardhi ya mtu (no man’s
land). Kwa sababu hiyo na kwa sababu Zanzibar ndiyo yenye uhusiano wa
karibu zaidi na kisiwa hicho, alimshauri Sir Lloyd Mathews aende katika
kisiwa hicho haraka iwezekanavyo na akaweke bendera ya Zanzibar ili
kukichukua na kukitangaza rasmi kuwa ni kisiwa cha Zanzibar.
4. KISIWA CHA LATHAM KUTANGAZWA RASMI KUWA CHA ZANZIBAR
Mbali ya ushauri huo wa Sir Arthur Hardinge, ambao unaonyesha ulipelekwa
pia kwa Sultani, tarehe 17 Oktoba, 1898, Sir Lloyd Mathews alipokea
maelekezo kutoka kwa Sultani kuwa aende katika kisiwa cha Latham ili
akapachike bendera ya Zanzibar na kukitangaza rasmi kisiwa hicho kuwa
kiko chini ya mamlaka ya Zanzibar.
Kufuatia maelekezo hayo, Lloyd Mathews aliondoka Zanzibar tarehe 18
Oktoba, 1898 kwa kutumia boti ya SS Barawa. Alifuatana na Captain Arthur
Agnew, Port Officer wa Zanzibar na Dr. Alfred Andrew Spurrier, Medical
Officer, wafanyakazi wa boti hiyo na vibarua wengine kadhaa. Saa 12
asubuhi ya tarehe 19 Oktoba, 1898 bendera ya Zanzibar ilipandishwa
ikifuatiwa na saluti ya mizinga 21. Aidha, nyumba ya chuma ilijengwa na
bao kubwa la Tangazo lililosomeka “LATHAM ISLAND, FUNGU KIZIMKAZI UNDER
ZANZIBAR SOVEREIGNTY” na pembeni ya ubao huo wa Tangazo maneno ya
kiarabu yaliandikwa ambayo yakisomeka kama ifuatavyo “ Seyyid Hamoud byn
Mohamed byn Said wa Zanzibar”. Ofisa mmoja aitwaye Captain Baw na
wasaidizi wawili waliteuliwa kuwa wasimamizi wa kisiwa hicho.
Sir Lloyd Mathews alirejea Zanzibar na akaandika taarifa rasmi
kumpelekea Sultani, Waziri Kiongozi na Wizara ya Mambo ya Nje ya
Uingereza.
5. MADAI YA UJERUMANI JUU YA KISIWA CHA LATHAM
Kwa mara ya mwanzo kabisa Ujerumani ilizusha madai ya umiliki wa kisiwa
cha Latham mnamo mwaka 1910. Madai hayo hata hivyo yalianzia mwaka 1909.
Mnamo tarehe 23 Juni, 1909 Sir Edward Clarke alimuandikia Gavana wa
Ujerumani wa Tanganyika akimueleza kuwa kuna taarifa kuwa wapo raia wa
Uingereza wanaoishi kusini mwa Tanganyika ambao wanakwenda kuchukua
samadi ya ndege (guano) bila ya ruhusa ya Serikali ya Zanzibar. Alimtaka
Gavana asitishe vitendo hivyo mara moja. Tarehe 6 Disemba, 1910, Gavana
wa Tanganyika aliandika Waraka kwa Serikali ya Zanzibar akidai kuwa
Ujerumani ndiyo yenye mamlaka juu ya kisiwa cha Latham. Katika kujenga
hoja hiyo, Waraka huo ulinukuu zaidi vifungu vya mikataba baina ya
Wajerumani na Waingereza ambayo ilitambua mamlaka ya Zanzibar. Kwa
tafsiri ya mikataba hiyo alidai kuwa Zanzibar haina mamlaka juu ya
kisiwa hicho.
Mnamo tarehe 13 April, 1911 Sir Edward Grey alijibu Waraka huo kwa
kuandika Waraka wa majibu kumpelekea Herr Von Kuhlmann wa Ofisi ya
Gavana wa Tanganyika.
Katika majibu yake Sir Edward Grey alieleza hoja zifuatazo:
a) Kwamba kisiwa cha Latham kiliwekwa rasmi kuwa sehemu ya Zanzibar
kuanzia tarehe 19 Oktoba, 1898 na akafafanua kwa urefu juu ya kazi ya
uwekaji wa bendera ya Zanzibar kulikofanywa na Sir Lloyd Mathews;
b) Alikumbusha kwa urefu mawasiliano yaliyofanywa katika mwaka 1900
baina ya Serikali ya Uingereza na nchi kadhaa ikiwemo Ujerumani juu ya
pendekezo ya kujenga minara ya kuongozea meli katika eneo la Zanzibar
kikiwemo kisiwa cha Latham, Pemba Kaskazini na Chumbe. Alieleza kuwa
Ujerumani ilikuwa moja ya nchi zilizotoa maoni kuhusu pendekezo hilo
lakini haikuwahi kudai
wala kuonyesha dalili ya kuwa Latham ni sehemu ya mamlaka ya Ujerumani
wala kupinga mamlaka ya Zanzibar juu ya kisiwa cha Latham;
c) Alifanya uchambuzi wa mikataba hiyo na kuhitimisha kwa kueleza kuwa
hakuna mkataba wowote kati ya hiyo ambayo imetoa mamlaka ya wazi kwa
Ujerumani au Uingereza juu ya kisiwa cha Latham. Alimalizia kwa
kuishauri Ujerumani kama ina hamu ya kukimiliki kisiwa cha Latham
iwasiliane na Serikali ya Zanzibar ambayo inaweza kuzungumza juu ya
suala hilo.
Serikali ya Ujerumani haikuwahi hata mara moja kujibu Waraka huo wa Sir
Edward Grey na wala haikuwahi kuwasiliana na Serikali ya Zanzibar juu ya
kisiwa hicho. Hatimaye iliwekewa kumbukumbu rasmi kuwa suala la hoja ya
Ujerumani juu ya umiliki wa kisiwa cha Latham limefungwa rasmi.
6. SUALA LA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM BAADA YA UJERUMANI KUONDOKA TANGANYIKA
Wakati wa utawala wa Uingereza katika Tanganyika suala la umiliki wa
kisiwa cha Latham halikuwahi kujitokeza. Badala yake, utawala wa
Uingereza uliendelea kusisitiza kuwa kisiwa hicho ni mali ya Zanzibar.
Mtu mmoja aitwaye Mc Elderry aliiandikia barua Serikali ya Tanganyika
akiomba ruhusa ya kuchukua samadi ya ndege kutoka katika kisiwa cha
Latham. Mnamo tarehe 16 Novemba, 1934 Sekretariat ya Serikali ya
Tanganyika ilimuandikia barua Bw. Mc Elderry kujibu maombi yake. Katika
barua hiyo ya majibu Sekretariat ilieleza kuwa kisiwa cha Latham
hakikuwahi kuwa chini ya mamlaka ya Ujerumani. Aidha, katika
kuthibitisha hilo, ilielezwa kuwa hata katika ramani ya Reich’s
Kolonialamt iliyochapishwa Berlin mwaka 1908 haikuonyesha kuwa Latham ni
sehemu ya mamlaka ya Ujerumani.
HATUA ZA KIUTAWALA NA KISHERIA ZA SERIKALI YA ZANZIBAR JUU YA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Serikali ya Zanzibar iliendelea kukitumia na
kukiendesha kisiwa cha Latham kwa shughuli mbali mbali. Miongoni mwa
shughuli hizo ni utafiti wa ndege, kupanda miti, utafiti juu ya kima cha
samadi ya ndege (guano) kama inatosheleza kibiashara au la.
Mbali ya shughuli hizo, viongozi kadhaa, akiwemo Sultani na British
Resident walitembelea kisiwa cha Latham na taarifa za safari zao
zimewekewa kumbukumbu. Mfano mzuri ni ziara ya British Resident ya
tarehe 9 March, 1951.
Mnamo mwaka 1959, Serikali ya Zanzibar ilikitangaza kisiwa cha Latham
kuwa ni hifadhi ya ndege (bird sanctuary) kupitia Tangazo Namba 56 la
1959 kama linavyoonekana hapa chini. Kwa mujibu wa kumbukumbu tulizoweza
kuzitafiti, Tangazo hili bado halijafutwa au kurekebishwa na hivyo,
kisheria, kisiwa hicho bado ni hifadhi ya ndege ya Zanzibar.
8. HITIMISHO
Ni dhahiri kwamba kwa kumbukumbu za kisheria na za kiutawala ziliopo na
ushahidi juu namna kisiwa cha Latham kimekuwa kikitumika, kusimamiwa na
kuendeshwa, kisiwa hicho cha Latham kipo chini ya mamlaka ya Zanzibar
tokea tarehe 19 Oktoba, 1898.
Aidha, Zanzibar imekuwa inakitumia na kukisimamia kisiwa hicho kiutawala
kwa miaka yote hiyo mfululizo bila ya kuwepo madai wala haki ya mamlaka
nyengine. Hivyo, kisheria kisiwa hicho ni sehemu ya Zanzibar na kwamba
Zanzibar ina mamlaka halali juu ya kisiwa hicho tokea tarehe 19 October
1898.
OTHMAN MASOUD OTHMAN
ADVOCATE & NOTARY PUBLIC
Źanzibar
+255777411175
+255784515184
Click to expand...
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA