Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed
Shein ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar kupitia Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kusimamisha utoaji wa mikopo ya elimu ya
juu, hadi hapo serikali itakapojiridhisha na utaratibu mzima wa utoaji
wa mikopo hiyo. Blogu ya Hussein Juma imeinasa!!
“Hatutatoa mikopo mwaka huu mpaka hapo tutakapokamilisha kazi ambayo
tumeanza kuifanya ya kupitia upya utaratibu wa utoaji mikopo hiyo ili
kuhakikisha inatolewa kulingana na mahitaji ya sasa ya nchi na kwa
wanaostahili,” amesema Dkt. Shein.
Akizungumza katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofaulu
daraja la kwanza katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2015
na Kidato cha Sita mwaka 2016, Dkt. Shein amesema kuwa katika utaratibu
wa sasa wapo waliodanganya kupata mikopo na ambao wamekopeshwa lakini
wamekuwa wagumu kurejesha mikopo hiyo.
Katika hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Usii Gavu, jumla ya
wanafunzi 119 waliomaliza kidato cha nne na wengine 50 waliomaliza
kidato cha sita, walipewa zawadi kwa kupata daraja la kwanza katika
mitihani yao ya taifa.
“Wako waliokejeli matokeo yenu, lakini ukweli ni huo mko 50 wa kidato
cha tano mliopata daraja la kwanza na wengine 119 mliofaulu daraja la
kwanza mtihani wa kidato cha nne,” amesema Dkt. Shein na kuhoji msingi
wa kukebehi matokeo hayo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA