Nawaomba radhi sana wananchi wa Singida, sikuweza kuwepo Namfua baada ya waandaaji kuahirisha tamasha, ipo siku tutakutana.
Nimekwishasema mara nyingi kwamba, hata mimi, kama ilivyo binadamu
wengine huwa nina siku mbaya na nzuri katika maisha yangu, kwa sababu
kwa watu wengi tafsiri ya maisha bora ni kuwa na gari, nyumba, kazi,
fedha nk. Ni rahisi kudhani kwamba ninaishi maisha ya furaha kila siku,
si kweli, kuna siku natokwa na machozi kama binadamu mwingine, naomba
nikushirikishe sasa siku yangu ya Novemba 19, 2016, siku ya Jumamosi
iliyopita, ili upate uhalisia wa maisha.
Usingizi ulikata saa tisa na nusu usiku, nikaanza kuyapitia maisha yangu
na changamoto ninazokutana nazo, mambo ninayoyafanya lakini pia
kufanyiwa na watu. Mawazo yangu haya yananifikisha kwenye uhusiano wangu
na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa muda mrefu sana nimekuwa kada
wake, mara kadhaa nikijitoa mhanga mimi mwenyewe kukitetea na
kukipigania nikiamini ndiyo chama pekee kinachoweza kuwaletea Watanzania
mabadiliko ya kweli.
Naipenda CCM, nakiamini chama hiki hata kama kuna baadhi ya watendaji
ndani yake natofautiana na jinsi wanavyofanya mambo kiasi cha kuathiri
hatma ya chama hiki kama taasisi, wapenzi, mashabiki na wanachama wake.
Pamoja na kuwa mfanyabiashara nimewahi kuacha kazi zangu na kuzunguka
karibu nusu ya nchi yetu nikipiga kampeni na Rais Jakaya Mrisho Kikwete,
lakini kwa sababu mtu yeyote anayeonesha mapenzi kwa CCM hasa akiwa
mfanyabiashara hutafsiriwa anajipendekeza au mwoga, pengine hivyo ndivyo
ninavyoitwa, lakini kwangu mimi ambacho hunisukuma kufanya mambo haya
ni mapenzi na imani niliyonayo kwa CCM kama taasisi na zilivyo sera
zake.
Kama nilivyosema hapo awali, tatizo langu kubwa huwa ni watendaji wa
CCM, ambao wakati mwingine hufanya mambo ambayo huathiri mapenzi yangu
kwa taasisi yenyewe, hali hii imewavunja moyo watu wengi sana waliokuwa
na mapenzi pamoja na imani kubwa kwa CCM.
Yesu ni mwokozi wangu, daima nitazungumza ukweli, hata kama
utanigharimu! Nakumbuka huko nyuma nimewahi kuzungumza ukweli kuhusu CCM
kwenye ukurasa huu, baadhi ya viongozi wa juu hawakufurahishwa na
nilichokiandika, Katibu Mkuu Kinana nikiongea naye ofisi kwake
aliniambia “Eric wewe ni kijana wa hapa, siku nyingine ukiwa na suala la
kuzungumza tueleze sisi moja kwa moja, usilipeleke barabarani!”
Nilikubaliana naye na sikuwa tayari kabisa kusema maneno yaliyotokana na
mawazo yangu ya usiku gazetini tena, kwani nilimuahidi nisingefanya
hivyo, lakini nifanye nini, nisemee wapi? Kama katibu mkuu wangu
nampigia simu kila siku hapokei? Namuandikia ujumbe kwa njia ya WhatsApp
na unaonekana umesomwa lakini hanijibu, tafsiri yangu ni ya haraka ni
kwamba ananidharau ingawa mimi namuheshimu kama baba na kiongozi wangu,
angalau angekuwa anapokea simu hata kunipa tu matumaini, nisingefikia
hatua ya kuzungumza hapa.
Kuanzia usingizi ulipokata saa tisa na nusu usiku, nilifikiria mambo mengi sana juu ya namna ambavyo baadhi
ya watendaji wa CCM wamekuwa wakinifanyia pamoja na kujitoa kwangu kote
kwa chama hicho, moyo unaniuma mno kwani sistahili hata kidogo
kufanyiwa mambo ambayo leo natendewa na chama ambacho mimi binafsi
naamini nimejitoa kiasi kikubwa mno kukitumikia kwa akili, muda na mwili
wangu.
Inahitaji usiwe mtu mwenye hofu au uliyekata tamaa kufungua mdomo na kuzungumza nitakayoyasema leo,
ndugu zangu, Watanzania wenzangu, moyoni mwangu pamejaa uchungu mwingi
mno, acha niseme labda nitakuwa mwepesi! Sijui kitakachonipata, Mungu
anajua, mimi ni msema kweli, nionavyo mimi ni bora kuzungumza ukweli
ukapata matatizo kuliko ubaki hai ukiendeleza unafiki, NASHINDWA.
Mawazo haya juu ya CCM yananitoa machozi mke wangu akiwa usingizini
kando yangu, sitaki kumuamsha, sitaki kumshirikisha kinachoendelea, mimi
ni mtoto wa kiume mambo mengine natakiwa kukabiliana nayo mwenyewe, kwa
muda mrefu naendelea kuwaza nikiwapitia viongozi mbalimbali wa CCM
kuanzia mwenyekiti mstaafu, mwenyekiti aliyeko madarakani, katibu mkuu
na mweka hazina.
“Mama!” saa kumi na mbili na dakika kumi namuamsha mke wangu.
“Bee!”
“Tulikubaliana kwenda hospitali Muhimbili kusalimia mgonjwa.”
“Kweli.”
“Mzima lakini?”
“Naendelea vizuri, wewe?”
“Mimi mzima, nina mafua tu kidogo!” nilimjibu hivyo kwa sababu sikutaka agundue kilichokuwa kimetokea.
Kawaida ya wanawake ni kujiandaa taratibu sana, mpaka tunaondoka kwenda
Muhimbili tayari ilikuwa ni saa moja asubuhi, tumechelewa muda wa kuona
wagonjwa. Mbele ya Jengo la Mwaisela, alipolazwa mgonjwa ambaye ni
mkamwana wa mama mmoja aitwaye Mama Swai, ambaye tulikuwa tukiabudu naye
Kanisa la Word Alive kabla hatujahamia Victory Christian Center,
tunakutana na mlinzi mkali kama pilipili.
“Muda wa kuona wagonjwa umekwisha.”
“Tusaidie kaka” nambembeleza kwa muda, hatimaye akionekana kunionea
huruma, anasema “basi aende mmoja tu, tena mwanamke, maana hii wodi ni
ya wanawake.”
“Mama nenda basi wewe!”
Mke wangu anaondoka na kuniacha nimesimama peke yangu nje ya wodi,
mawazo yananirejesha tena kwa CCM baada ya kubaki peke yangu, najiuliza
ni kitu gani nimekikosea chama hicho mpaka kunitendea mambo
wanayonitendea! Roho inaniuma, nasikia huzuni kubwa moyoni mwangu, niko
chini kabisa kiroho leo, sina furaha hata kidogo, mawazo ya CCM na mambo
wanayonitendea, wakati mimi nilishafanya mema mengi kwao yamenivuruga.
Dakika ishirini baadaye mke wangu anatokeza kutoka wodini, alikuwa
amepewa muda mfupi sana, pamoja tunaongozana mpaka kwenye gari,
namfungulia mlango, anaketi nami nakaa kwenye usukani na kuanza
kuendesha kuelekea ofisini, anawahi kazini kwake kwa sababu leo ana
sherehe ya watu waliokodisha hoteli.
Njiani nasikia wimbo wa vijana kutoka Kenya waitwao Sauti Sol, uitwao
‘Kuliko Jana’ nilishawahi kuusikia wimbo huo kabla, lakini leo
unaonekana kuwa wimbo mpya kabisa kwangu, maneno yake yananigusa sana
moyo, namshikirisha Vene kwenye wimbo huo, anaonekana kama hanielewi au
ninachokiongea hakimgusi, bila shaka anawaza sherehe inayofanyika
hotelini kwake.
“Hawa vijana wanaimba sana, natamani siku moja niwaalike hapa Dar es
Salaam, nifanye tamasha kubwa la vijana kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu,
bure! Nifundishe vijana wa taifa hili uzalendo na kupenda nchi yao.”
Natamka maneno hayo ingawa moyoni mwangu kuna uchungu mwingi;
Bwana ni mwokozi wangu,
Tena ni kiongozi wangu,
Ananipenda leo kuliko jana!
Baraka zake hazikwishi si kama binadamu habadiliki,
Ananipenda leo kuliko jana,
Kuliko jana, kuliko jana,
Yesu nipende leo kuliko jana,
Kuliko jana, kuliko jana,
Yesu nipende leo kuliko jana,
Nakuomba Mungu uwasamehe
Wangalijua jinsi unavyonipenda
Mimi wasingenisema
Na maadui wangu nawaombea
Maisha marefu wazidi kuniona ukinibariki
Ujue binadamu ni watu wa ajabu sana
Walimkana Yesu mara tatu kabla jogoo kuwika…
Safari inaendelea, wimbo uliokuwa ukipigwa redioni umefika mwisho, kwa
kutumia simu yangu nilitafuta ‘You tube’ kisha kuuchagua wimbo huo ambao
unaendelea kupiga mpaka namfikisha mke wangu ofisini kwake, kila
unapokwisha naurudia tena, unanizidishia uchungu moyoni, namshusha mke
wangu na kuendesha tena kuelekea ofisini kwangu.
Mawazo ni mengi, kichwa kimevurugika, Mariam, msaidizi wangu anaingia na
kunitayarishia chai, nakunywa lakini haipandi. Baadaye anaondoa vyombo
na kuniacha peke yangu, muda mfupi baadaye aliingia mzee Mbizo, sijui
kama alinielewa kwa hali aliyonikuta nayo, nilikuwa kwenye siku yangu
mbaya, niko chini sakafuni nawaza, baada ya salamu tu tofauti na siku
nyingine zote ambazo mimi na yeye huongea mambo machache, anaaga na
kuondoka.
Nabaki peke yangu nikiendelea kufikiria, naikumbuka siku ya mwisho
nilipofika ofisi ndogo ya CCM pale Lumumba, ambako nilikwenda
nikitarajia kulipwa fedha zangu ninazodai kwa kazi niliyoifanya (kwa leo
sitataja ni kiasi gani) kama nilivyokuwa nimeahidiwa baada ya kuwa
nimesubiri mwaka mmoja na miezi sita, hapo katikati nikiwa nimelipwa
fedha kidogokidogo sana.
Tofauti na matarajio kwamba siku hiyo ningelipwa fedha zote, nikalipwa kiduchu tena! Nikiwa
ndani ya ofisi ya mweka hazina wa chama, mama Zakia Meghji, yeye ni
shahidi, kama nasema uongo au ukweli anajua, machozi yalinitoka! Hali
yangu kibiashara ni mbaya, fedha nyingi ziko mikononi mwa CCM na nina
madeni makubwa ninayodaiwa, baadhi ya wadai wanataka kupiga mnada mali
zangu! Chama Cha Mapinduzi kimeniingiza kwenye matatizo makubwa.
Nakumbuka alichokifanya mama huyu ni kunipa chupa ndogo ya maji ya
Kilimanjaro na kuniambia “Kunywa maji mwanangu, upunguze uchungu!”
nikayapokea na kuyanywa, niliondoka ofisini hapo nikiahidiwa kwamba
ningelipwa muda si mrefu, lakini haikuwa hivyo, siku zinazidi kusonga na
hali inazidi kuwa mbaya na hakuna anayeonekana kujali.
Kwenye saa 5: 00 asubuhi hivi, naamua kuachana na mawazo hayo kwani
maisha bado yanaendelea na kuamua kwenda kuungana na wenzangu kwenye
kikao cha asubuhi kujadili maendeleo ya Gazeti la Ijumaa Wikienda ili
nifute kilichokuwa kikiendelea kichwani, nafanikiwa kufanya kikao hicho
bila mtu yeyote kugundua kilichokuwa kikiendelea akilini mwangu na
baadaye narejea ofisini ambako naendelea kuusikiliza Wimbo wa Sauti Sol
huku nikizidi kuhuzunika.
Muda mfupi baadaye anaingia Davina Lema, msimamizi wa kampuni yetu ya
Blue Mark Real Estate ambayo inajishughulisha na upangishaji wa nyumba,
tunaongea naye kuhusu biashara na namna ya kufanya biashara katika
kipindi hiki kigumu, nampenda Davina, alianza kazi hii akiwa hajui
chochote lakini sasa amemudu kazi, baada ya mazungumzo hayo ndiyo naanza
kumweleza kidogo kuhusu maisha na namna ambavyo mtu unaweza ukatenda
wema lakini ukalipwa ubaya.
Sikuweza kuzungumza hadi mwisho, machozi yananitoka mbele ya mfanyakazi
wangu, si jambo jema lakini sikuwa na jinsi, siandiki haya ili nionewe
huruma la hasha! Nawaeleza muone baadhi ya siku zangu ambavyo huwa
zinakuwa, mtu asinione napita barabarani akadhani maisha yangu ni keki
kila siku, kuna mateso na maumivu makubwa nyuma yake!
Alichofanya Davina ni kunitafutia tishu za kufutia machozi kisha
kuondoka baada ya meneja wetu mkuu, Abdallah Mrisho kuingia na kunikuta
katika hali mbaya niliyokuwa nayo, akaketi chini na kuanza kunidadisi ni
kwa nini nilikuwa nalia! Kwikwi ilikuwa imenishika sikuweza kuongea,
kuna jitu lilikuwa kooni ambalo nahisi ni hasira.
“Braza inaniuma sana, nimejitahidi maishani mwangu kuwa mtu mwema,
nikikusanya senti tanotano kwa njia halali mpaka kufika hapa nilipo,
mimi ni tofauti sana na wanasiasa ambao wanaweza kutia saini mkataba
mmoja tu wa kifisadi wakaingiza bilioni ishirini au watoto wa viongozi
wanaoweza kutumia majina ya wazazi wao kujipatia mikataba minono ya
kuwatajirisha, kaka unajua mimi nadunduliza kila siku nikijinyima na
kuishi maisha ya kawaida ili niwaachie watoto wangu urithi, leo hii
nahisi kabisa nataka kunyang’anywa haki yangu niliyoitesekea kwa muda
mrefu, inaniuma!
Kwa mwili huu nilikuwa na uwezo wa kushika bunduki na kuingia benki
kuchukua fedha au kwenda Brazil kupakia mzigo mkubwa wa heroin au
Cocaine na kuleta hapa nyumbani kuja kuharibu watoto wa watu akili,
sikutaka kufanya hayo yote kwa sababu sitaki kufanya dhambi au kupata
fedha ambazo baadaye nitajilaumu, nimechagua kufanya biashara halali
kuanzia gazeti la shilingi mia moja mpaka leo shilingi elfu moja, kwa
nini sasa kikundi fulani cha watu kininyime haki yangu? Sitakubali, ni
bora nife kuliko kubaki hai wakati haki yangu inataka kuchukuliwa na
wanaoona kwamba wana nguvu na hawawezi kufanywa chochote.”
Wakati nayasema maneno hayo yote nilikuwa nikilia kwa uchungu mno,
meneja mkuu alijaribu kunituliza lakini alishindwa, roho ilikuwa
ikiniuma sana, mimi mtoto wa maskini, niliyetoka chini kimaisha
nikapambana mpaka hapa nilipo, unidhulumu kiasi kikubwa cha fedha namna
hiyo? (nitakitaja hivi karibuni). Hapana, ni bora kufa au kupigania haki
mpaka tone la mwisho, huko ndiko kunaitwa kuwa mwanaume.
Baadaye nilitulia, tukazungumza na braza Mrisho kwa muda mrefu akinisihi
nitulie wala nisichukue hatua yeyote, yeye akiamini haikuwa rahisi
kudhulumiwa wakati tulikuwa na mikataba! Jambo moja ambalo hakulifahamu
ni kwamba dhamana tulizoweka kwa waliotukopesha fedha zingeweza kuuzwa,
hata kama baadaye tungelipwa na CCM ingekuwa haina maana kubwa, wazungu
wana msemo usemao “Justice delayed is justice denied” yaani haki
iliyocheleweshwa ni sawa na haki ambayo haikutolewa, wakati wa kulipwa
na CCM ni sasa ili tuepuke kuuziwa dhamana zetu.
Alipoondoka meneja mkuu ofisini kwangu, aliingia Nyemo Chilongani, mmoja
wa vijana wachapakazi ofisini kwangu ambaye husimamia ukurasa wangu wa
Facebook, aliongozana na wasichana wawili ambao aliwatambulisha kwangu
kama mashabiki wa ukurasa wangu ambao walikuja ofisini kununua vitabu na
walitaka niwasainie vitabu vyao na pia tupige picha pamoja.
Wasichana hawa walikuwa ni Zainabu na Dina kutokea Kigamboni, mara moja
nilibadilisha muonekano wangu kama vile kilikuwa hakijatokea kitu,
tukaanza kuongea mambo mbalimbali kuhusu maisha, nikiwaeleza umuhimu wa
kuthamini vipaji maishani, ambavyo kila mmoja wetu anavyo, “Mtu anaweza
kufeli darasani kama nilivyokuwa nikifeli mimi, lakini kipaji kikamuinua
na kumfanya awe mtu mwenye mafanikio!”
Mwisho wa mazungumzo yetu nilipiga nao picha na kwa kweli walifurahi
kukutana nami ambaye ujio wao na mazungumzo tuliyoyafanya ulisaidia sana
kubadilisha akili yangu na kunipa uwezo wa kuketi chini na kuandika
haya unayoyasoma leo.
Hivyo ndivyo siku yangu ya Novemba 19, 2016, ilivyoanza, nifuatilie wiki
ijayo nipate kukueleza kwa undani kilichotokea mpaka nikajikuta katika
haya niliyoyaandika leo.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA