Arusha.
Sakata la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka fedha katika akaunti
maalumu kwenye benki za biashara limechukua sura mpya baada ya Gavana wa
Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kusema si kosa kisheria.
Profesa Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRA iliyovunjwa na
Rais John Magufuli Jumapili iliyopita, alisema mjini hapa jana kuwa
hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum isipokuwa hilo
suala lilikuwa na hali nyingine.
Japokuwa Profesa Ndulu hakutaka kufafanua zaidi kwa maelezo
lilichomekewa tu katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea hali
ya uchumi, alisema hali hiyo ndiyo suala lililozungumzwa na siyo kusema
“fixed deposit account” ni mbaya.
“Kwani amesema fixed account zote ni mbaya, pamoja na za watu binafsi?
Ndo hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa hiyo nilikuwa tayari,”
alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa
habari walipotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka
fedha kwenye akaunti maalum tena benki binafsi.
Kauli hii ya Profesa Ndullu imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli
kueleza kilichochangia kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa Mwenyekiti
wa Bodi, Bernard Mchomvu na pia kuivunja bodi yake iliyokuwa na wajumbe
tisa. Kati ya wajumbe hao tisa, watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na
wanne ni wa kuteuliwa.
Wajumbe wanaoingia kwenye Bodi kwa mujibu wa sheria ni Gavana wa BoT,
Profesa Beno Ndullu; Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata; Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Doto James; Katibu Mkuu Wizara
ya Fedha Zanzibar, Khamis Mussa Khamis; na Katibu Mkuu Mipango. Bodi
hiyo ilivunjwa Jumapili iliyopita.
Rais Magufuli alisema juzi kuwa Bodi ya TRA iliyokuwa na watendaji hao
wakuu wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha
uamuzi wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za
binafsi.
“Juzi hapa tumekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya
matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit
account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela
nikazichukua na bodi kwaheri,” alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni
rasmi kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
yaliyofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambako jumla ya Vijana 4038
walihitimu shahada mbalimbali
Ukwasi wa mabenki
Katika hatua nyingine Profesa Ndullu amesema ukwasi wa fedha katika
mabenki umeshuka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma hatua inayotatiza
utoaji wa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mara baada ya kufungwa mkutano
wa 18 wa taasisi za fedha uliofanyika kwa siku mbili jijini hapa alisema
hali hiyo inafanyiwa kazi na wadau wa taasisi hizo ili kuja na mbinu
kufanya kuwa endelevu kwani uchumi unategemea uwekezaji unaotegemea
mikopo ya muda mrefu.
Profesa Ndulu alisema BoT itahakikisha inaziwezesha benki kuendelea na
jukumu lao la kutoa mikopo pia kuwa wabunifu wa kutafuta pesa kwa ajli
ya amana badala ya kutegemea Serikali pekee.
“Benki zinaweza kukusanya amana kwa kiwango kikubwa lakini kama
nilivyosema jana (juzi) kuwa katika kila Sh60 kati ya Sh100 zipo kwenye
mikono ya watu badala ya kuwekwa akiba benki hivyo ni muhimu zikawekwa
mbinu ya kuzipata kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji kuzitumia kwenye
uzalishaji,” alisema.
Alisema katika kufanikisha mpango huo lazima kuvutia mitaji kutoka nje
kwani hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kupiga hatua kwa kutegemea
fedha za maendeleo na uwekezaji zitokane na mapato ya ndani pekee
akitolea mfano wa nchi China kuwa ni mfano uchumi wake kutegemea mitaji
inayotoka nje ya nchi hiyo.
Katika hatua nyingine Profesa Ndullu alisema amekubaliana na wadau wa
sekta ya fedha kuongeza nguvu katika kutoa mikopo na kuboresha mifumo ya
taarifa kwa wale wanaotaka mikopo kwa ajili ya kilimo katika mnyororo
mzima wa thamani kuanzia uzalishaji hadi kufika kwenye soko.
Profesa Ndulu alisema Tanzania imekaa vizuri kijiografia kufanya
biashara na nchi zisizo na bahari zikiwemo Malawi, Uganda, DRC na Zambia
katika kuwezesha sekta ya fedha kusaidia eneo la usafirishaji, bandari
kufanya kazi na huduma kutolewa inavyotakiwa.
Mwenyekiti wa wenye mabenki ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB,
Dk Charles Kimei amesema waendeshaji wa mabenki wamenufaika na kuelewa
mikakati na fursa za Serikali ambayo itawawezesha wao kutoa fedha kwa
wafanyabishara.
Alisema wao kama CRDB wameweza kukusanya amana za Sh500 bilioni
zinazokopeshwa kwa wafanyabiashara katika kipindi cha miaka miwili
iliyopita na kufungua matawi madogo madogo 100 nchi nzima ambayo ni siyo
gharama kubwa.
Dk Kimei alisema serikali inapobanwa kifedha kutokana na kutegemea
mashirika ya umma inawapa fursa sekta binafsi kupanua wigo wao kuwafikia
wananchi wengi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA