Mahakama
Kuu imewapa siku saba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake kujibu
madai ya chama hicho.
Msajili, Lipumba na wenzake walipewa muda huo jana na Jaji Sekieti
Kihiyo kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa
CUF mahakamani hapo.
Katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, bodi ya wadhamini CUF inaiomba
mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa
Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.
Pia, wanaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kufanya kazi nje ya
mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake na pia itoe
amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama
hicho.
Mbali na Msajili na Profesa Lipumba, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wanachama wengine tisa
waliosimamishwa uanachama wa chama hicho, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara
ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua (Tabora), Magdalena Sakaya.
Kesi hiyo ilitajwa jana mahakamani hapo kwa mara ya kwanza tangu
ilipofunguliwa Oktoba 19, mwaka huu na mahakama ikataka wadaiwa
kuwasilisha majibu ya madai hayo ya CUF, Novemba 17, mwaka huu.
Pia, Mahakama ilielekeza upande wa Maalim Seif kuwasilisha majibu ya
hoja za wadaiwa Novemba 23 na ikapanga kesi hiyo itajwe tena Novemba 24,
kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Wadai katika kesi hiyo wanawakilishwa na mawakili Juma Nassoro na
Halfani Daim wakati Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wanawakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Obadia Kameya na
Lipumba na wenzake wakiwakilishwa na Mashaka Ngole.
Katika hati ya Kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Maalim Seif anadai
kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia utendaji wa
ndani wa Vyama vya Siasa.
Anadai kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya nchi haimpi mamlaka
Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa chombo cha rufaa wala kurejea mambo ya
utawala ndani ya chama cha siasa.
Badala yake anadai mamlaka hayo yako kwa vyombo vya juu vya chama na
Mahakama na kwamba jukumu la Msajili ni kusajili vyama na kuweka
kumbukumbu za vyama hivyo.
CUF kimekuwa na mgogoro wa kiuongozi baada ya Profesa Lipumba kuandika
barua ya kutengua uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu ambao Msajili
alikubaliana naye na alikiandikia barua chama kuendelea kumtambua
mwenyekiti huyo. Hata hivyo, CUF ilimfukuza uanachama Lipumba.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA