Kwa masiku kadhaa Sheikh Khalifa amekuwa akisikika na kauli yake ya
kumtuhumu Rais Magufuli kuwajaza Wakristo wengi kwenye nafasi zake za
uteuzi.
Aidha Sheikh huyo aliongezea kwa kusema kuwa licha ya uwepo wa suala
hili la udini Rais Magufuli ameweka wazi upendeleo wake wa kikanda
ambapo watu wa kanda ya Ziwa wameonekana kung’ara kwa kuteuliwa katika
nafasi za uongozi kwa wingi zaidi kuliko watu wa kanda yoyote hapa
nchini.
Akizungumzia suala hilo na waandishi wa gazeti la Mizani la November 11,
2016 Sheikh Khalifa Khamis alieleza kuwa katika nafasi 10
walizotumbuliwa Waislam ni nafasi 1 tu ndiyo aliyopewa Muislam.
Sheikh Khalifa alizidi kufafanua kuwa Wenyeviti wa bodi mbalimbali
walioteuliwa na Rais Magufuli 18 ni Wakristo na 1 tu ndiyo Muislam.
Makatibu Tawala wa Wilaya Wakristo ni 81% huku Waislam wakiambulia 19% tu. Wakuu wa wilaya Wakristo ni 71% na Waislam ni 21%.
Makatibu Tawala wa mikoa 137 ni Wakristo na 16 tu ndiyo Waislam.
Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya na majiji Wakristo ni 185 na
Waislam ni 36 tu.
Kitu pekee anachopaswa kutambua Sheikh Khalifa Khamis ni kwamba Rais
Magufuli hateui mtu kwa kuangalia dini bali anaangalia taaluma na uwezo
wa kuongoza.
Kukiwa na kitengo kinachohitaji uwakilishi wa dini hapo ndo tunapaswa
kuangalia usawa wa uwakilishi wa kidini. Pia anapaswa kutambua kuwa
Tanzania haina Wakristo na Waislam tu, kuna watu wa dini tofauti tofauti
na wasio na dini pia, je hao amewaweka kwenye kipengele gani?
Hizi ni njama tu za kutaka kumrudisha nyuma Rais wetu kipenzi cha
Watanzania wengi. Watanzania tunahitaji MAENDELEO na AMANI tu, mambo ya
dini tunayaacha kwenye nyumba za ibada. Tunapofika kwenye sekta za umma
hatusemi tena mambo ya dini zetu, bali kauli yetu huwa ni moja tu nayo
ni HAPA KAZI TU.
Ni jambo la kusikitisha sana kuona kiongozi mkubwa wa dini akitoa tuhuma za uongo na uzushi kwa Kiongozi Mkuu wa wa nchi yetu.
Sheikh Khalifa anakiuka misingi ya imara ya taifa letu iliyowekwa na
baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere ya kupiga vita udini na ukabila.
Udini na ukabila ni mbegu mbaya sana ambayo siyo tu haifai kupandwa
kwenye ardhi yetu bali haipaswi hata kutunzwa majumbani mwetu, isije mea
hata kwa bahati mbaya.
Mataifa mengi yameshuhudia machafuko na mauaji ya kutisha kwa udini na
ukabila. Hakuna hata Mtanzania mmoja anayetamani kuona mfano wa mauaji
ya Kimbari ya Rwanda au vita ya Biafra Nigeria ikitokea hapa kwetu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA