Mbeya. Muuguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya anayedaiwa kumkamshifu
Junes Elias, mkazi wa Mbozi mkoani Songwe na Rais John Magufuli
ametambuliwa.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Gloria Mbwille alisema muuguzi huyo
ametambuliwa na kwamba tume imeundwa kuchunguza tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, alikataa kuzungumzia zaidi kuhusu muuguzi huyo wala kumtaja
jina akisema taarifa zaidi zitatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos
Makalla baada ya tume kukamilisha uchunguzi huo. Juzi mchana, Junes
alimueleza Makalla kwamba alifika hospitalini hapo Novemba 22 asubuhi
akitokea wilayani Mbozi.
Alisema baada alifuata taratibu za kufungua kadi kwa gharama ya Sh5,000
kwa ajili ya kutaka matibabu ya mtoto wake, Joyce Asifiwe (9), lakini
alikashfiwa kwenye dirisha la dawa akiambiwa ataisoma namba kwa
kumchagua Rais Magufuli.
Alisema baada ya kumuona daktari aliandikiwa dawa za kwenda kuchukua kwenye dirisha ambako ndiko alikotolewa maneno ya kashfa.
“Kwenye dirisha hilo nilimkuta muuguzi mmoja ambaye aliniambia kwamba
dawa zote zinauzwa. Hapa hakuna dawa za bure, si mlimchagua Magufuli,
sasa mtaisoma namba,’’ alisema akidai kumnukuu aliyemtaja kuwa ni
muuguzi.
Baada ya kumsikiliza malalamiko hayo, Makalla aliagiza mganga mkuu
aitwe, lakini ilielezwa alikuwa safarini, hivyo kaimu wake, Dk Ismail
Macha alifika.
Makalla alimueleza Dk Macha kwa kifupi yaliyojiri kutoka kwa mlalamikaji
huyo na kumtaka waongozane hadi hospitalini na kuwaita wauguzi
waliokuwa zamu Novemba 22 dirisha la dawa ili amtambue mhusika na
achukuliwe hatua jambo ambalo limefanyika.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA