Lusekelo 'Mzee wa Upako' afunguka baada ya kashfa

Siku moja baada ya Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo kudaiwa kumfanyia fujo jirani yake, mchungaji huyo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako ameibuka kanisani kwake na kusema msemo wake wa kawaida kuwa, ‘watashindana lakini hawatashinda.’


Pia alisema kuwa alitaka kusema jambo, lakini hatazungumza kama wengi walivyodhani.

Lusekelo aliyasema hayo jana jioni katika ibada ya Ijumaa kanisani kwake, Ubungo Kibangu ambako mwandishi wa Mwananchi alihudhuria.

“Nimeyaona magazeti hapa, ooh Mzee wa Upako, ooh Mzee wa Upako, sisemi. Sasa leo yupo hapa, na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini hawatashinda. Hii ni kama kumpiga chura teke,” alisema huku akishangiliwa na waumini wake.

Kabla ya kuzungumza, Lusekelo aliingia kanisani akiimba wimbo wa kuabudu ‘Niguse Tena’ huku waumini wote wakiwa wamesimama.

Akiwa amevalia shati jeupe la kitenge na suruali nyeusi huku kanisa likiwa limezingirwa na walinzi kila kona, mchungaji huyo aliingia na kusimama madhabahuni kisha kuwasalimu waumini: “Nawasalimu katika jina la Bwana.”

Baada ya salamu hiyo, alianza kuimba wimbo mwingine na waumini hao wakaanza kuimba pamoja naye huku wakipita mmoja mmoja mbele kumtuza fedha.

Wimbo ulipoisha, waumini waliketi na Lusekelo alianza kuhubiri kwa kufungua Biblia katika kitabu cha 2 Timotheo 4.

Katikati ya mahubiri hayo, alidokeza na kusema kuna watu walikuwa wanasubiri kuona Mzee wa Upako hayupo na wanataka aseme, lakini hatasema chochote.

“Kuna kitu nilikuwa nataka nikiseme, lakini sitakisema ili waendelee kusema haohao waliokuwa wanasema. Sisemi chochote. Hao waliosema wakawaulize wenyewe,” alisema bila kufafanua zaidi.

Ingawa alisema hatasema chochote, mahubiri yake yalionekana kama kujibu mapigo.

“Imani yangu ndiyo ilikuwa mwisho, kwa sababu maadui watakuwa wengi lakini watajikuta wanapiga risasi kule, kumbe adui yupo huku… vita ni kutulia,” alisema.

“Adui yako hataacha kuwa adui yako. Jiepushe sana na watu hao. Lakini mimi ninaamini Mungu atawalipa sawa na amri yake wakati ukifika.”

Aliendelea na kusema wanadamu wamekengeuka na kuziacha njia za uzima na kuzigeukia njia zao wenyewe.

“Wakati wote watu watakataa kusikia ule ukweli, Ogopa sana anayekataa kukusikiliza, watakapozigeukia njia zao wenyewe, wakiacha kusikia ukweli, jua kuna tatizo, akiacha kukusikiliza ni hatari sana jua kuna rushwa. Ukiona anaacha kukusikiliza kaa tayari” alisema.

Mchungaji huyo aliendelea kuhubiri na kusema ni marufuku kumuhukumu mtu kabla ya kumsikiliza.

“Hao ndiyo marafiki wanafiki.Nao wakajiepusha wasisikie yaliyo kweli na watageukia hadithi za uongo. Uongo ukisemwa sana hubadilika na kuwa ni kweli.

“Wale wazee wa Israel walitunga uongo, na wakatoa fedha uongo usambazwe, ule uongo mpaka leo bado unaitafuna Israel.” alisema Mzee wa Upako.

Kabla ya Lusekelo kuingia kanisani, mchungaji mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana alisimama madhabahuni na kusema mwaka huu mwanzoni Mchungaji aliziombea bahasha na kuubariki kuwa mwaka wa kucheka. “Kuna watu wanaotaka kuuharibu, lakini hawatafanikiwa.”

“Zimebaki siku 40 kabla ya kumaliza mwaka wa kucheka, lakini kuna watu lazima muwe nao makini wanaweza kusababisha mwaka wa kucheka usiishe vizuri.” alisema

Mahojiano ya Mwananchi na Mzee wa Upako Jumanne wiki hii

Awali katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani kwake Kawe Jumanne wiki hii, Lusekelo alisifu uamuzi wa Serikali ya Rais John Magufuli kwa kuzuia shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni kwa kuwa hali ya kisiasa Zanzibar si nzuri na kwamba uamuzi huo unanusuru amani ya nchi.

Mzee wa Upako alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Jumanne kabla ya taarifa zake za hivi karibuni kuwa amegombana na jirani yake.

Hata hivyo, Lusekelo amesema shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria ni muhimu kurushwa moja kwa moja, lakini ni hatari kwa usalama iwapo kitatumiwa vibaya.

Serikali ilitangaza Januari mwaka huu kuwa kituo cha televisheni cha Shirika la Utangaza la Taifa (TBC) hakitakuwa kikirusha shughuli zote za Bunge kutokana na gharama za matangazo hayo kuwa kubwa.

Waziri wa Habari, Nape Nnauye alisema wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo bungeni kuwa badala yake shughuli hizo zitarekodiwa na kurushwa usiku na kwamba vituo vingine binafsi vinaruhusiwa kurusha moja kwa moja.

Hata hivyo, vituo binafsi pia vilizuiwa na sasa hata wapigapicha za televisheni hawaruhusiwi kuingia na kamera ndani ya ukumbi wa Bunge.

Sababu ya Waziri Nape aliyotoa wakati huo, ilipishana na kauli ya Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa aliyoitoa wakati akizungumza na Watanzania waishio nchini Uingereza ambako alisema kurusha Bunge moja kwa moja ni kwenda kinyume na kaulimbiu ya Rais Magufuli ya “Hapa Kazi Tu” kwa kuwa anataka watu wafanye kazi badala ya kuangalia matangazo ya televisheni wakati wote.

Katika mahojiano hayo, Mzee wa Upako alisema ni muhimu kuwa na Bunge Live, lakini kutokana na hali ya kisaiasa ya Zanzibar na sababu za kiusalama ni bora lisionyeshwe.

“Hali ya Zanzibar kisiasa si nzuri kwa hiyo ukiacha uhuru wa kila mtu aseme anachojisikia, ni hatari kwa taifa hili. Mali kubwa tuliyonayo katika nchi hii ni amani na utulivu. Wanasiasa si watu wazuri sana (kwa kuwa) wapo tayari kufanya lolote ili wapate madaraka au wasalie madarakani,” alisema.

Alisema si vyema ukawaacha watu kuzungumza kuhusu maandamano na mikutano ya kisiasa bungeni na Bunge lipo ‘live’ wakati unajua hali iliyopo Zanzibar. Na unapozungumzia uongozi wa Rais, lazima ujue kwamba ana dhamana ya kusimamia ulinzi na usalama.

“Ukisema uanze kusemasema tu kila kitu, utahatarisha amani ya Taifa hili kwa kuwa mtu anaweza kusema neno dogo tu nchi ikalipuka. Hivyo Serikali kuchukua uamuzi wa kuchuja nini kinasemwa ni muhimu sana kiusalama,” alisema Mzee wa upako.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka jana kwa mara ya kwanza wapinzani walipata kura nyingi, hivyo ni dhahiri kwamba hao watu wanakubalika.

Alisema kwa maana hiyo endapo wapinzani wakiruhusiwa kuingia barabarani kuandamana inawezekana wakasababisha maafa.

“Endapo wataingia (wataandamana) wapinzani 20,000 tu halafu wakakataa kutoka unafanyeje? Ukisema uue watu 300 inakuwa ni nchi tena? Tayari vita,” alisema mchungaji huyo.

Kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, Mchungaji Lusekelo alisema kinachomkwamisha katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kupata uongozi wa Zanzibar ni hoja yake ya Serikali tatu kwa kuwa inaiweka nchi njia panda katika masuala ya amani na usalama.

“Kwa mfano kama kweli Sharif alishinda, tatizo si kushinda, tatizo ni usalama wa nchi. Unapozungumza Serikali tatu unatuhakikishiaje kuwa nchi yetu itakuwa salama? Au unatuhakikishiaje kwamba tutakuwa wamoja?” alihoji.

“Hakutakuwa na Tanganyika na Zanzibar? Akishindwa kutuhakikishia, bora mambo yabaki hivi hivi kwa kuwa amani ni muhimu kuliko madaraka.”

Alisema amani ya nchi si kitu cha kuchezea wala kujaribisha kwa kuwa nguvu ya ngumi haipimwi kwenye mwili wa mtu.

Kadhalika alisema siasa za Zanzibar zimetawaliwa na ubaguzi baina ya wakazi wa Unguja na Pemba tofauti na hali ilivyo Tanzania Bara.

“Ni kama Kenya ambako ukabila umetawala,” alisema.

“Ni vigumu sana Mpemba akawa CCM na hata akienda CCM ujue kanunuliwa tu na ukimchunguza vizuri utakuta si Mpemba, na ndiyo maana siku zote, CCM itashinda Unguja na CUF itashinda Pemba, piga ua.”

Kuhusu suala la Katiba Mpya

Mzee wa Upako alisema tatizo la Watanzania si Katiba Mpya, bali maisha mazuri, huduma nzuri za afya, ulinzi na usalama na kuona rasilimali za nchi zinawanufaisha.

“Suala la Katiba Mpya ni hitaji la kisiasa si la wananchi. Wapinzani wanadhani ikipatikana Katiba Mpya, wataweza kushika dola na chama tawala wanadhani watapokonywa dola, lakini wananchi wao wanataka maendeleo,” alisema mchungaji huyo.

Chapisha Maoni

0 Maoni