Mfanyabaishara Ndama Hussein maarufu kama mtoto wa Ng’ombe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka sita ikiwamo kughushi na kutakatisha Dola za Kimarekani 540,390 (sawa na Sh, bilioni 1.181). Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa akisaidiana na Wakili wa Serikali Leonard Challo.
Msigwa alidai kuwa Februari 20, mwaka 2014, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa na lengo la kudanganya alighushi nyaraka za kusafirisha madini akionyesha kwamba Kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited imepewa kibali cha kusafirisha boksi nne za vipande wa dhahabu zenye uzito wa kilo 207 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 8.2 kwa Kampuni yenye makazi yake nchini Austaria inajulikana kama Trade TJL DTYL Limited huku akijua nyaraka hizo za uongo.
Katika shtaka la pili, Machi 6, mwaka 2014, jijini Dar es Salaam akiwa na nia ya kudanganya, aliandaa nyaraka za uongo kuonyesha kwamba hati ya kuondolea mizigo kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa za tarehe hiyo, akiwa na lengo la kuonyesha kwamba vipande vya dhahabu vyenye uzito wa kilo 207 kutoka Jamhuri ya Congo, kuwa zinasafirishwa na Kampuni ya Muru Platnum kwenda Austraria.
Msigwa alidai katika shtaka la tatu, Februari 20, mwaka 2014 jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kudanganya alighushi nyaraka zikionyesha kuwa ni fomu ya tamko la kodi akionyesha Kampuni ya Muru Platnum imelipa Dola za Kimarekani 331,200 kama kodi ya kuingiza mzigo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kilo 207 ya vipande vya dhahabu vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 8,280,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku akijua ni uongo.
Katika shtaka nne, Februari 20, mwaka 2014 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa na nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka zauongo za kuonyesha kuwa ni za bima kutoka Kampuni ya Phoenix Ltd za terehe hiyo, akilenga kuonyesha kwamba Kampuni ya Muru Platnum imekatia bima boksi nne za vipande vya dhahabu zenye uzito wa kilo 207 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 8,280,000 huku akijua ni uongo.
Katika shtaka la tano na sita, kati ya Februari 26 na Machi 3, mwaka 2014 jijini Dar es Salaam, alijipatia kwa njia ya uongo na kutakatisha Dola za Kimarekani, 540,390 (sawa na Sh. Bilioni 1.181) kutoka Kampuni ya Trade TJL DTYL Limited kwa madai kuwa angesambaza na kusafirisha nje ya nchi kilo 207 za vipande vya dhahabu vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 8,280,000 lakini hakufanya hivyo.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alitakatisha fedha hizo zilizopatikana kwa njia ya jinai kwa kuelekeza kiasi hicho cha fedha kuingizwa katika akaunti iliyopo benki ya Stanbic yenye jina la Kampuni ya Muru Platnum na baadaye alizitoa zote na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi huku akijua zimepatikana kwa njia ya udanganyifu.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na uliomba mahakama tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Nongwa alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 13, mwaka huu.
Mshtakiwa alirudhishwa mahabusu kwa sababu mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA