Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameingia katika mapambano ya wazi na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako kwa kumpa maagizo, ambayo ameyakataa.
Makonda amemwagiza Waziri Prof. Ndalichako asiwasikilize wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Al-Muntazir iliyopo jijini Dar es Salaam, lakini kinyume chake, Prof. Ndalichako ameunda Kamati ya kuchunguza malalamiko ya wazazi yaliyodumu kwa miaka mitatu sasa.
Uongozi wa shule hii umekuwa na ‘kiburi’ cha ajabu kwa kutotii maagizo ya Serikali kupitia barua zaidi ya sita walizoandikiwa kutokana na ‘jeuri’ ya fedha, hali inayowafanya wazazi kuendelea kuumizwa kwa kutozwa ada na faini kubwa kinyume na maelekezo ya Serikali.
Wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatoza ada ya Sh milioni 1.3 kwa kozi ya Uhandisi kwa mwaka, shule binafsi ya msingi ya Al-Muntazir imeongeza ada kwa kiwango cha asilimia 10-15, kwa mujibu wa waraka wao wa malipo. Ada ya mwaka huu imepanda hadi Sh 2,480,000 kutoka Sh 1,980,000 ya mwaka jana.
Zipo shule nyingine nyingi jijini Dar es Salaam zilizokiuka waraka huu wa Serikali kwa kupandisha ada kutoka wastani wa Sh 600,000 kwa muhula na kufikia Sh 800,000. Shule nyingi za binafsi zina mihula mitatu kwa mwaka.
Baadhi ya wazazi wanaamini kuwa shule hii inakuwa na ‘kiburi’ kutokana na kuwa wamiliki wa shule hii au wajumbe wa Bodi ya Shule ni watu wazito waliowahi kushika nyadhifa kubwa serikalini au wanaoendelea kushikilia nyadhifa hizo.
Kati ya wajumbe wa Bodi wa shule hiyo ni pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo na mfanyabiashara maarufu nchini Azim Dawji, kama alivyowataja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda.
Makonda alivyoanzisha mgogoro
Makonda amejiingiza matatani baada ya kutembelea shule hiyo hivi karibuni katika shughuli ya kukabidhiwa madawati na kutamka maeneo yaliyosumbua mioyo ya wazazi waliohoji kama Makonda ni mtumishi wa umma au amejigeuza mpiga debe wa wavunja sheria, aliposema:
“Kama mwanao anapata elimu bora ni vema kuiombea shule hiyo, kama mwanao anapata elimu bora na unataka shule iharibikiwe, una matatizo ya akili.
“Ninataka hao wazazi wafuate taratibu zote, sio kukurupuka kwenda kushtaki wizara ya elimu… sasa ukiona inafikia hatua shule imefikisha miaka 40, bado ukaona kuna watu wanataka kuiangusha, huyo ni adui namba moja.
“Niwaambie wazazi kama una malalamiko peleka kwa menejimenti ya shule, peleka kwa afisa elimu wa wilaya, ikishindikana nenda kwa afisa elimu wa mkoa… nisingependa wazazi wawe na kiherere cha kuruka ngazi kwenda wizarani. Kama wangekuwa Katavi, wangeweza?
“Ninawaomba mawaziri msiwasikilize watu wanaoruka ngazi kuja wizarani, kisa tu ni karibu sana, nauli Sh 400… msife moyo. Kubalini kusemwasemwa, maana pia hayo ni matangazo, maana kama msingesemwa hata mimi nisingewajua.”
Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema ni kweli kumekuwapo tatizo kwa baadhi ya wazazi na uongozi wa shule kuhusu masuala kadhaa, likiwemo la ongezeko la ada.
“Pale wanao mgogoro wao ambao sitaki kuuingilia… ila kwa hakika wazazi hao wanatakiwa kufuata taratibu, wasiruke ngazi na kwenda kwa waziri, kama wangekuwa Katavi wangeweza kwenda kwa waziri?”
Wakati Makonda akiyasema hayo, baadhi ya wazazi wamelithibitishia JAMHURI kuwa ngazi zote alizozitaja Makonda wamezipitia bila msaada na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imetoa maagizo kupitia barua yenye Kumb. Na. FA.49/6401D/28 ya Machi 21, 2016 ikisema baadhi ya wazazi wamewasilisha malalamiko ofisini kwake juu ya ada na faini inayotozwa kwa wazazi wanaoshindwa kulipa ada ndani ya siku saba.
Barua hiyo iliyosainiwa na R. E. Mapunda kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwaelekeza wamiliki wa shule hiyo kuwa: “Ongezeko la ada linakwenda kinyume na katazo la kuongeza ada kwa shule zisizo za Serikali kwa mwaka wa masomo 2016, ambalo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambayo sasa ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.” Aliwapa siku 7 kutekeleza maagizo yake. Makonda anasema wazazi hawajapitia ofisini kwake!
Waziri Prof. Ndalichako asikiliza wananchi
Akizungumza na JAMHURI, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amesema amekuwa akiyasikia yanayoendelea baina ya wazazi na uongozi wa shule ya Al-Muntazir.
Katika kulinda heshima ya Serikali isidhalilishwe na wenye shule binafsi, Prof. Ndalichako anasema, ofisi yake imekuwa inawasiliana na uongozi wa shule hiyo, huku kukiwa na mlolongo wa mawasiliano ya barua kwa muda mrefu na kwamba anatafuta namna ya kumaliza mgogoro huo baada ya kufahamu chibuko halisi.
“Nimemuagiza Katibu Mkuu, aunde Timu ya Wataalamu ambao watapitia mgogoro huu kwa kina na kunishauri…ili baadaye nichukue hatua ambazo zitakuwa suluhisho kwa mgogoro huo,” anasema Prof. Ndalichako.
Walivyoshughulikia mgogoro
Shule za Al-Muntazir zimeendelea kupuuza agizo la serikali la ada elekezi, badala yake menejimenti ya shule hizo imeendelea kupanga ada ya masomo kama inavyotaka, hali inayoleta mkanganyiko kwa baadhi ya wazazi. Wanamiliki shule za awali, msingi na sekondari.
Shule hizo ambazo zina wanafunzi kuanzia madarasa ya awali mpaka kidato cha sita, zimekuwa zikiongeza ada na kukaidi agizo la serikali, hata baada ya Kamishna wa Elimu kuingilia kati na kuwataka wasitishe mpango huo mara moja.
Kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Elimu yenye Kumb. Na. PA.275/295/64/26 ya Mei 9, mwaka huu, iliutaka uongozi wa shule hiyo kutoa maelezo ndani ya siku saba juu ya kwa nini wameongeza ada bila kupata kibali kutoka kwenye ofisi ya Kamishna huyo.
Prof. Eustella Bhalalusesa ambaye alikuwa Kamishna wa Elimu katika kipindi hicho, aliandika barua akinukuu baru yake nyingine yenye Kumb. Na. SYCB/312/371/01/50 ya Aprili mwaka huu, ambayo iliutaka uongozi wa shule hiyo kusitisha ongezeko la ada na gharama nyingine za uendeshaji kwa wazazi kwa mwaka 2016.
“Aidha wazazi ambao walikwishalipa ada ya muhula wa kwanza kwa viwango vilivyowekwa mwaka 2016, walipe pungufu kwa muhula wa pili ili kiwango kisizidi kile kilichotozwa mwaka 2015 na kuacha kutoza faini kwa wazazi ambao wamechelewa kulipa ada.
“Hata hivyo, mpaka sasa hujatekeleza agizo hilo, hali ambayo imesababisha kuendelea kwa malalamiko miongoni mwa wazazi,” inasomeka sehemu ya barua ya Prof. Bhalalusesa.
Barua kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam iliyotajwa hapo juu, iliyosainiwa na R.E. Mapunda kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam ilinakiliwa kwa Kamishna wa Elimu na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ikisema, ongezeko la ada linakwenda kinyume na katazo la kuongeza ada kwa shule zisizo za serikali kwa mwaka wa masomo 2016.
“Wamiliki wote wa shule zisizo za serikali wanaagizwa kutoongeza gharama za uendeshaji shule zikiwemo ada kwa mwaka wa masomo unaoanza Januari 2016, mpaka watakapopata maeleko kutoka kwa Kamishna wa Elimu,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Mapunda ananukuu waraka wa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambayo sasa ni Wizara ya Eimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Mbali na kauli ya Kamishna wa Elimu, kuhusu katazo la serikali la ongezeko la ada, shule hizo zimeendelea na msimamo wake, huku baadhi ya wazazi wakiamua kulifikisha suala hilo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi.
Katika barua yao yenye Kumb. Na. UMJ/WAZ/MTZ/012, wazazi hao wanamweleza Katibu Mkuu Kiongozi mlolongo wa hatua ambazo zimechukuliwa na serikali, huku shule zikiwa hazizitambui na badala yake zimeendelea kushikilia msimamo wake wa ongezeko la ada.
Al-Muntazir wazungumza
Akizungumza na JAMHURI, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Abdulwahid Zacharia, anakiri kwamba kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wazazi kuhusu ada, huku akisema wazazi hao wamekuwa hawapeleki malalamiko yao kwa viongozi husika.
“Wizara ya Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, walituandikia barua kutaka tusitoze ada zaidi, badala yake tuendelee na ile ya mwaka jana, pamoja na suala la kuwalipisha faini wazazi wanapozidisha muda wa kulipa ada.
“[Pia] Wizara ilituandikia barua ikitutaka tusimamishe usajili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza pamoja na wale wa kidato cha tano, ila sasa wameturuhusu huku wakitoa miongozo mbalimbali na kuelezea sehemu ambazo tunahitaji kuboresha,” anasema Zacharia.
Anasema, uamuzi huo wa wizara kuwaruhusu waendelee kusajili wanafunzi ulitolewa Julai, mwaka huu na shule ya Al-Muntazir wakaendelea na usajili. Zacharia anasema waliendelea na usajili wa wanafunzi wa kidato cha tano mpaka Agosti, huku wakiendelea na usajili wa kidato cha kwanza mpaka Oktoba, mwaka huu.
“Wizara ya Elimu, ilituma timu ya watalamu wake hapa kukagua… walituelezea kuhusu mapungufu yetu, moja ikiwa ni kutokuwa na Bodi ya Shule, jingine ni suala la kuwatoza wazazi faini pamoja na suala la kutoongeza ada,” anasema Zacharia.
Amesema Bodi ya Shule imeundwa, faini ya kuchelewesha ada imeondolewa na mwaka huu hawajaongeza ada, ingawa nyaraka za shule kwa wazazi ambazo JAMHURI linazo, zinabainisha kuwa mwaka huu wametoa maagizo ya kuongeza ada.
Uongozi wa shule unawalaumu baadhi ya wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha suala la ada linashughulikiwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa maafisa wa shule ya Al-Muntazir, Suleiman Salim, anasema, “Baadhi ya wazazi wanaoshughulikia suala hili hawana lengo zuri na shule… Kwa nini wamekuwa wakificha majina yao? Wamekuwa wanaleta barua ambazo hazina majina ya walioandika.”
Suleiman, akazidi kuwatuhumu baadhi ya wazazi hao kuwa wamejipa kazi ya upolisi huku wakishindwa kuelewa kwamba wizara inavyo vyombo vyake vya kuchunguza kuhusu madai waliyoyasema.
“Hawajawahi kukutana na uongozi wa shule na kuelezea masikitiko yao. Kama wanaogopa pengine kufahamika kwa kuhofia watoto wao kufukuzwa shule, wala jambo hilo haliwezekani maana kuna mlolongo wa taratibu ili kufikia uamuzi huo,” anasema Suleiman.
Akizungumza kuhusu ada elekezi zilizotolewa na wizara, Zacharia anakiri kwamba waliona tangazo kwenye magazeti, huku akisema hawakuwahi kupelekewa waraka wowote kutoka wizarani ambao unazuia ongezeko la ada.
Hata baada ya kuulizwa na JAMHURI, kwamba kwa nini hawakufuatilia wizarani baada ya kuona tangazo, Zacharia anasema; “Utafuatilia mambo mangapi na magazeti yanaandika kila siku. Mimi nafahamu serikali huwasiliana nasi kwa barua na sio magazeti.”
Kuhusu barua ambazo shule imekuwa ikiandikiwa na Serikali, akasema kwa dharau na mkato: “Tumekuwa tukiwajibu.”
Mtaala wa dini usiokubalika
Mwaka jana baadhi ya wazazi waliwasilisha malalamiko yao kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wakidai kuwa mtaala wa somo la dini unaofundishwa katika shule hiyo kwa kulazimisha wanafunzi wote bila kujali madhehebu au dini zao unakiuka maadili ya Kitanzania na kiimani.
“Hawa wamiliki wa shule za Al-Muntazir tulilalamika kwa waziri kuwa wanafundisha watoto wetu katika mtaala kuwa ikiwa mkewe yupo kwenye hedhi, basi dini yao inaruhusu mume kumwingilia mkewe kinyume na maumbile. Waziri alishika mdomo, akabaki kinywa wazi.
Alifanya uchunguzi na kubaini hilo, kisha akawaandikia barua ya kuwazuia aina hii ya mafundisho,” anasema mmoja wa wazazi. Zaidi ya wazazi 50 wamekutana na JAMHURI na kulalamikia mambo kadhaa kwa shule hizo.
Baada ya uchunguzi wa wizara, uongozi wa shule ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat ya Dar es Salaam (ambao ni wamiliki wa shule za Al-Muntazir), uliandikiwa barua yenye Kumb. Na. JA.259/287/07911 ya Februari 18, 2015 ikizuia mafundisho hayo, chini ya kichwa cha habari kisemacho; Yah: Utaratibu wa Ufundishaji wa Somo la Dini. Kisha barua hiyo ikaendelea kusomeka:
Tafadhali rejea somo la barua hii.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imepokea barua ya maalalamiko toka kwa wazazi wenye wanafunzi wa Kiislam wa Kisunni wanaosoma katika shule yako. Malalamiko hayo yanahusu ufundishaji wa Elimu ya Dini kwa mtaala ulioandaliwa na shule bila kushirikisha wazazi/walezi wa wanafunzi hao.
Imebainika kuwa shule yako imeanadaa Mtaala wa Elimu ya Dini ya Kiislam ambao unatumika kufundishia wanafunzi wote wa Kiislam. Hata hivyo, unatakiwa kuelewa kuwa, kuna Waislam wa madhehebu tofauti wenye imani zinazotofautiana na maudhui yaliyomo ndani ya Mtaala ulioandaa ambao kwa njia moja ama nyingine wazazi/walezi wa wanafunzi hawakushirikishwa katika kuuandaa.
Somo la dini ni miongoni mwa masomo yaliyomo katika vipindi vinavyotakiwa kufundishwa katika shule za Msingi na limo ndani ya ratiba ya shule. Hivyo, somo la dini linatakiwa kufundishwa kwa kuzingatia imani za wazazi/walezi wa wanafunzi. Kwa mantiki hiyo, kama una wanafunzi wa Kikristo wapewe nafasi ya kuadubu kwa imani yao.
Kinachotakiwa wanafunzi waabudu kulingana na madhehebu yao. Kulazimisha mwanafunzi kusoma dini inayopingana na imani yake ni kukiuka utaratibu na sheria ya usajili wa shule na hasa ikizingatiwa kuwa shule yako ilisajiliwa kama ya Msingi inayofuata Mtaala wa Tanzania na kufundisha kwa lugha ya Kiingereza na si shule ya seminari, hivyo, inasajili wanafunzi wa madhehebu yote. Rejea vyeti vya kusajili No. DSS.01/7/026 na DS.01/7/003.
Kwa barua hii na kwa kuzingatia malalamiko yaliyotolewa na wazazi wa wanafunzi wanaosoma shuleni kwako unasisitizwa kuzingatia utaratibu wa kufundisha dini kwa kuzingatia tofauti za madhehebu ili kuepusha mgogoro usiokuwa na lazima kwa kutoa nafasi kwa kila dhehebu kusoma masomo ya dini wakati wa kipindi cha dini kulinangana na imani husika. Kushindwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na utaratibu wa usajili wa shule. Aidha, wizara itaendelea kulifuatilia suala hili.
Nakutakia utekelezaji mwema.
Prof. E. P. Bhalalusesa
Kamishna wa Elimu
Barua hiyo ilitolewa nakala kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shule (K), Kanda ya Dar es Salaam, S. L. P. 5429, Dar es Salaam, Afisa Elimu Mkoa, S. L. P. 5429, Dar es Salaam, Mkaguzi Mkuu wa Shule, Manispaa ya Ilala, S. L. P. 7467, Dar es Salaam na Mwenyekiti, Wazazi wa Watoto – Al-Muntazir Boys & Girls Primary School, Dar es Salaam.
Mwalimu Mkuu Mzaidizi Zacharia alipoulizwa juu ya suala la mtaala unaokiuka maadili ya kiimani na Kitanzania, alisema: “Baada ya maelekezo ya wizara tumeupeleka Mtaala BAKWATA, na BAKWATA wamepitia na kuturudishia. Sasa tunatumia Mtaala mpya hakuna malalamiko tena.”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA