Siku
tatu baada ya Rais John Magufuli kueleza bayana kwamba suala la Katiba
Mpya si kipaumbele chake kwa sasa akitaka aachwe ili ainyooshe nchi
kwanza, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu amesema kiongozi huyo
hawezi kunyoosha nchi bila kuwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya
wananchi.
Wakati Lissu akisema hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Jaji mstaafu Damiani Lubuva amesema atatolea ufafanuzi suala hilo
siku za karibuni.
Lubuva na Lissu walieleza hayo walipotakiwa kuzungumzia kauli ya Rais
Magufuli kwamba kipaumbele chake ni kuchapa kazi ili kuinyoosha nchi na
mengine yafuate ikiwamo Katiba Mpya.
Magufuli alitoa kauli hiyo Novemba nne, alipozungumza na Wahariri wa
vyombo mbalimbali vya habari siku moja kabla ya kutimiza mwaka mmoja
tangu aingie madarakani.
Lakini, Lissu alisema nchi haiwezi kunyooka bila kunyoosha kwanza Katiba
inayoiongoza ambapo alipendekeza uwepo wa Katiba Mpya badala ya
kuifanyia marekebisho iliyopo sasa.
“Tulishaondoka kwenye mjadala wa kuziba viraka kwenye Katiba,
tumeshakubaliana kwamba tunahitaji mabadiliko ya Katiba yote si sehemu
tu. Rais asidhani mtu akikalia kiti hicho basi neno lake ni sheria ya
nchi. Haiwezekani,” alisema.
Alisema mchakato wa Katiba Mpya hautakiwi kuendelea ulipoishia kwa maelezo kuwa ikiwa hivyo nchi haiwezi kufika popote.
“Katiba Inayopendekezwa ni kama imepakwa rangi ya Katiba ya sasa.
Inaonekana mpya lakini misingi yake ni ya Katiba ya sasa…, kama Rais
Magufuli anataka kunyoosha nchi, anapaswa kuirejea Rasimu ya Jaji
Warioba. Tuanzie hapo, zaidi ya hivyo atajidanganya na kuwadanganya
Watanzania,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema nchi haiwezi
kuongozwa kwa matamko ya kiongozi mkuu pekee bila kuangalia matatizo ya
kisheria.
“Anafikiri akiamua yeye kama Rais unafuata utekelezaji? Kuna matatizo
mengine ya kikatiba…, hayawezi kubadilika bila kufanyika kwa mabadiliko
ya Katiba. Kuna mambo ili yanyooke ni lazima uwe na Katiba nzuri.
Usipoyashughulikia hayo mengine yote hayatawezekana,” alisema Lissu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Lubuva alipoulizwa
kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na kauli ya Rais Magufuli alisema suala
hilo linahitaji kukaa na kulizungumza vizuri.
“Naomba upokee kuwa nimekuelewa ila kwa sasa ninachoweza kusema nitatoa
ufafanuzi mzuri kuhusu suala hilo kwani ni jukumu la ofisi yangu,”
alisema.
Alisema ni kweli baada ya Katiba Inayopendekezwa kupigiwa kura na Bunge
hatua iliyokuwa inafuata ilikuwa ni kuitisha Kura ya Maoni, lakini
ilishindikana kutokana na kuingiliana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kabla ya Rais Magufuli kutoa kauli yake kuhusu Katiba Mpya, siku za
karibuni NEC iliwahi kueleza kwamba ipo katika hatua mbalimbali za
kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa sheria.
Katika kauli yake ya Novemba nne, Rais Magufuli alisema wakati anaomba
kura hakuweza kuzungumzia Katiba hivyo kwa sasa kilichopo mbele yake ni
kunyoosha nchi kwanza na Katiba mpya itakuja baadaye.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA