Dar es Salaam.
Kauli ya Rais John Magufuli kwamba hawezi kuyafukua makaburi yote,
imetafsiriwa na wachambuzi wa duru za kisiasa kuwa pengine alilenga
kashfa nzito za kifisadi zilizowahusisha vigogo katika Serikali
zilizopita.
Rais alitoa kauli hiyo Ijumaa katika mkutano na waandishi wa habari
uliolenga kutathmini mwaka mmoja wa utawala wake tangu aapishwe Novemba 5
mwaka jana.
Rais Magufuli, ambaye amejipambanua kuwa ni mtu anayepambana na ufisadi
bila ya kuogopa mtu, alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa
kituo cha televisheni cha TBCI, Anna Kwambaza aliyetaka kufahamu
kiongozi huyo wa nchi anaona tofauti gani katika matarajio aliyokuwa
nayo kabla ya kuingia Ikulu na hali halisi aliyoikuta.
“Siwezi kuyafukua makaburi yote kwa sababu kuna mengine nitashindwa
kuyafunika. Ninachofanya ni kutekeleza katika kipindi changu yale ambayo
nilitakiwa kuyatekeleza kwa ajili ya wananchi, ndiyo maana naomba
tushikamane,” alisema.
Kauli hiyo imekuja wakati Rais akiwa ameshachukua hatua kadhaa dhidi ya
watendaji wanaotuhumiwa kuhusika katika ufisadi uliofanywa wakati wa
utawala wa Serikali zilizopita na sasa amefanikisha kuanzishwa kwa
Mahakama ya mafisadi kufanikisha juhudi zake.
Kauli za wachambuzi
Lakini kauli kwamba hataweza kufukua baadhi ya makaburi kwa kuwa anaweza
asifanikiwe kuyafunika, imepokelewa kwa hisia tofauti na wachambuzi
waliofuatwa na Mwananchi kutoa maoni yao.
Wachambuzi hao walitaja kashfa kama za uchotaji wa fedha kutoka akaunti
ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu, ununuzi wa Rada,
mkataba wa ufuaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond, uchotaji
fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, Meremeta, Kagoda na hata fedha
zilizolenga kusaidia wananchi, maarufu kama “mabilioni ya JK”.
“Ili awe na uhusiano na viongozi waliomtangulia, hawezi kuyafukua
(baadhi ya makaburi), au yeye mwenyewe kuonekana alihusika wakati akiwa
waziri katika uongozi uliopita,” alisema Richard Mbunda kutoka Idara ya
Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Nadhani mazingira hayo ndiyo yanachangia asiweze kuyafukua.”
Mbunda alisema makaburi kama hayo yanatengeneza mazingira ya kumgusa
moja kwa moja na mengine kumchonganisha na viongozi waliomtangulia.
Maoni kama hayo yalitolewa na Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya
Sayansi ya Siasa ya UDSM aliyesema makaburi yanatokana na changamoto ya
kimfumo.
“Au inawezekana waliohusika walimsaidia hata kisiasa hadi hapo alipofika
ndani ya chama chake. Labda angekuwa upinzani ndiyo angeweza
kuyafukua,” alisema.
Hata hivyo, katika mtazamo mwingine alisema ni kawaida kwa kiongozi
anapoingia madarakani kutojihusisha zaidi na mambo yaliyofanyika katika
kipindi kilichopita licha ya kufanyia mwendelezo wa mambo ya msingi kama
vita dhidi ya rushwa.
Mwanaharakati wa haki za binadamu na mtetezi wa masuala ya kijinsia
nchini kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali alisema
kwa kuwa Rais ameshajipambanua kupambana na udhaifu, hatakiwi kuacha
baadhi ya makaburi.
Alisema kufanya hivyo kunaweza kuathiri watu wanaoendelea kutuhumiwa kuhusika na kashfa hizo.
“Tafsiri ya makaburi hayo ni kwamba nchi ilikuwa imekufa, imejaa wafu,
sera za nchi zimezikwa, sheria hazifanyi kazi na nchi iliendeshwa
kiholela. Sasa kama amekuwa akilaani mikataba mibovu ya madini, na yeye
ameshajipambanua kuwasaidia Watanzania, anawezaje kuacha makaburi hayo?”
alihoji.
Rada
Miongoni mwa kashfa zilizotajwa kuwa ni makaburi ambayo Rais Magufuli
hawezi kuyafukua ni ununuzi wa Rada ya kuongoza ndege kutoka Kampuni ya
Bae System Uingereza. Rada ilinunuliwa kwa gharama kubwa zaidi ya
uhalisia.
Uingereza ndiyo iliyobaini mchezo mchafu na kufanya uchunguzi
uliosababisha Tanzania irejeshewe dola 29.5 milioni za Kimarekani (Sh73
bilioni) Novemba 2013, lakini waliohusika hawajachukuliwa hatua yoyote.
Tanzania ilinunua rada hiyo kwa dola 40 milioni za Kimarekani (Sh54 bilioni).
Aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Andrew Chenge
alijiuzuru kutokana na ununuzi huo kufanywa wakati akiwa Mwanasheria
Mkuu.
Escrow
Pia, sakata la uchotwaji fedha kutoka akaunti ya Escrow limetajwa kama
moja ya makaburi hayo. Katika sakata hilo lililoibuka bungeni mwaka
2014, Sh306 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow iliyofunguliwa
kusubiri mgogoro wa kimkataba baina ya Tanesco na kampuni ya ufuaji
umeme ya IPTL kumalizika, zilichotwa katika mazingira yasiyoeleweka.
Fedha hizo zilichotwa ziliingizwa benki za Mkombozi na Stanbic na
baadaye kuonekana kugawiwa kwa wanasiasa, wakiwemo mawaziri, majaji,
viongozi wa dini na watumishi wa Serikali.
Hata hivyo, waliofahamika ni wale walioingiziwa mgawo kwenye akaunti
zilizokuwa benki ya Mkombozi, lakini waliopewa fedha taslimu baada ya
mabilioni kuchotwa Stanbic, hawajafahamika wala kuchukuliwa hatua.
Mei mwaka huu, Kambi ya upinzani iliibua sakata hilo bungeni huku
ikihoji sababu za Rais John Magufuli kutotekeleza maazimio ya Bunge ya
kumwajibisha Profesa Sospeter Muhongo, aliyejiuzulu kutokana na kashfa
hiyo na badala yake kumteua tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Richmond
Licha ya Dk Harrison Mwakyembe kusema wakati wa kampeni Agosti mwaka
jana akiwa jimboni kwake Kyela kuwa moto wa kashfa ya Richmond
haujazimika, hadi sasa hakuna hatua zinazoonekana kuchukuliwa.
Dk Mwakyembe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza
sakata la kuipa Richmond zabuni ya kufua umeme wa dharura mwaka 2008,
aliliambia Bunge wakati wa majumuisho ya mjadala kuwa kamati yake
haikusoma taarifa kamili ya suala hilo kwa hofu kuwa Serikali nzima
ingeondolewa na kuomba uchunguzi mpya ufanyike ili yaibuliwe mengi
zaidi.
Sakata hilo lililotokea mwaka 2008 baada ya Tanzania kukumbwa na
upungufu mkubwa wa umeme mwaka 2006 na Serikali iliingia mkataba na
Richmond Development Company LLC wa Sh172 bilioni. Edward Lowassa,
aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, alijiuzulu na amekuwa akisema kuwa
ushiriki wake ulitokana na maagizo kutoka juu.
Sakata la EPA
Wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2005 wafanyabiashara wakubwa
wakidaiwa kushirikiana na vigogo wa Serikali, walidaiwa kuwa kuchota
Sh133 bilioni kutoka akaunti ya EPA.
Hatua zilichukuliwa kwa baadhi ya maofisa wa Benki Kuu na
wafanyabiashara wadogo ambao baadhi wamefungwa, lakini watuhumiwa
wengine waliofanikisha ukwapuaji fedha hizo ama wameshinda kesi zao au
wanaendelea na maisha uraiani baada ya kutakiwa na Rais Jakaya Kikwete
kurejesha fedha hizo.
Kupitia sakata hilo, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali
alifukuzwa kazi na Rais Kikwete na akarudi Marekani ambako alikuwa na
uraia wa nchi hiyo na baadaye akafariki dunia na kuzikwa huko.
Mabilioni JK
Mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2005, Rais Kikwete alikuja na mpango
maarufu wa mabilioni ya JK alizoahidi kwenye kampeni. Sh50 bilioni
ziliwekwa benki ya NMB kwa ajili ya kukopesha wafanyabiashara wa kati
ili kuendeleza biashara zao, lakini sehemu ya fedha hizo hazikurejeshwa
na hakuna hatua zilizochukuliwa.
Taarifa ya Dk Mary Nagu, Waziri wa Uwezekezaji na Uwezeshaji aliyoitoa
mwaka 2012, ilisema ni Sh43 bilioni tu kati ya Sh50bilioni
zilizorejeshwa serikalini na wafanyabiashara waliokopa.
Aprili 24, mwaka huu, Takukuru ilinukuliwa na vyombo vya habari ikieleza kuanza kuchunguza fedha ambazo hazikurejeshwa.
Kashfa ya Kagoda
Katika sehemu ya Wizi wa EPA ulibainika wizi wa Sh40 bilioni
uliofanikishwa na kampuni ya Kagoda Agriculture kwa kisingizio cha
kufanya kazi za usalama.
Sh40 bilioni zilizokwapuliwa zilitoka BoT.
Sakata la Meremeta
Mwaka 2011 ulifanyika uchunguzi wa Bunge kuhusu ufisadi wa zaidi ya
Sh205.9 bilioni unaodaiwa kufanywa kupitia kampuni ya Meremeta iliyokuwa
ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hoja inayotakiwa kufanyiwa kazi na Kamati ya Bunge ni kuchunguza uhalali
wa malipo ya dola milioni 132 za Kimarekani (wastani wa Sh205.9 bilioni
kwa viwango cha sasa vya kubadilishia fedha vya wakati huo) ambazo
zilitoka BoT kwenda Ned Bank ya Afrika Kusini, ikiwa ni malipo ya mkopo
wa dola 10 milioni za Kimarekani, uliokuwa umechukuliwa na Kampuni ya
Meremeta Ltd, lakini hadi bunge linamaliza muda wake hakukuwa na taarifa
juu ya kilichobainika na baadaye ilielezwa kuwa masuala hayo ni ya
kijeshi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA