WALIOKUWA
wafanyakazi wa msimu takribani 500 wa Kampuni ya Kusindika Tumbaku
(TTPL) iliyopo mkoani Morogoro, wameandamana hadi ofisi ya Mfuko wa
Pensheni wa PPF Kanda ya Mashariki kushinikiza kupata ufafanuzi kuhusu
fao lao la kujitoa baada ya mikataba ya kazi na mwajiri wao kufikia
ukomo Oktoba 31, 2016.
Hatua hiyo ya kuandamana hadi katika Ofisi za Mfuko wa Pesheni wa PPF
Kanda ya Mashariki ilikuja baada ya kushindwa kupatiwa fomu za kujaza
kwa fao la kujitoa kutokana na barua yenye kumbukumbu PPF/GE/ECZ.
71/242/11 ya Oktoba 18, 2016 kwenda kwa Meneja wa Utumishi wa TTPL
iliyotolewa na PPF.
Barua hiyo ilisainiwa na Meneja wa PPF Kanda ya Mashariki, Michael
Christian ambayo ilieleza kwamba, Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa PPF
imezuia malipo ya fao la kujitoa kwa wanachama kuanzia Mei 12, 2016.
Hata hivyo alipoombwa na waandishi wa habari waliofika ofisini mwake ili
kuzungumzia sakata hilo, Christian alidai kuwa yeye si msemaji
isipokuwa msemaji ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, licha ya yeye
kuandika barua hiyo kwenda kwa Meneja Utumishi wa TTPL kuhusu fao la
kujitoa.
Kutokana na shinikizo hilo, uongozi wa PPF Kanda ya Mashariki ,
uliwaomba wateue wawakilishi watano kwenda kufanya mazungumzo na Meneja
wa kanda hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nje ya jengo la ofisi za Mfuko wa PPF
Kanda ya Mashariki mjini hapa, wafanyakazi hao wameulalamikia mfuko huo
kushindwa kutoa fomu za kujaza fao la kujitoa.
Walishangazwa na uongozi wa mfuko huo kuwasilisha barua kwa Meneja
Utumishi ikielezea kwamba Bodi ya Wadhamini imezuia malipo yao, jambo
linalokwenda kinyume cha kile walichokuwa wamefahamishwa kabla ya
kujiunga na mfuko huo.
Walidai kuwa PPF inafanya tofauti na mifuko mingine ambayo imeridhia kujitoa kwao na nakala za barua za kuridhia kujitoa wanazo.
Paulo Mhaku na Respicia Kalori, walisema kutokana na shughuli za kampuni
kupungua na hivyo kuelekea mwisho wa msimu wa 2016/2017, kampuni hiyo
iliwapatia barua kuwafahamisha kwamba mikataba yao itafikia ukomo Oktoba
31, 2016.
Walidai kampuni iliwafahamisha kuwa ujazaji wa mafao yao utatolewa kwa
njia ya matangazo Novemba mosi mwaka huu, ambapo ilitoa utaratibu wa
ujazaji wa fomu za madai.
Wafanyakazi hao walimwomba, Waziri mwenye dhamana pamoja na Mamkala ya
Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA) kuingilia kati jambo hilo
ili kupata haki zao kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine za kiuchumi
na si kusubiri kufikisha umri wa miaka 60 kama mfuko huo unavyohitaji.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya
Hifadhi za Jamii nchini (SSRA), Irene Isaka alisema marekebisho ya
Sheria Namba 5 ya mwaka 2012 yalikwishafuta vipengele vya kujitoa kwenye
baadhi ya mifuko ya jamii.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA