BY ZITTO KABWE:
Buriani BABU: Nimjuavyo Samwel John Sitta
Alfajiri ya leo, Novemba 7, 2016 imekuwa siku ya huzuni na majonzi
makubwa kwa Taifa. Tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha juu ya
kifo cha Mzee wetu Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Mzee Sitta alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo,
lakini bado tulikuwa na matumaini kuwa afya yake ingetengamaa na
kuendelea kuwa nasi.
Habari hizi za kufariki dunia kwake zilizosambaa kwa kasi kubwa kupitia
mitandao ya kijamii zimetushtusha mno. Hatimaye taarifa rasmi ikatoka
kuthibitisha habari hizo. Kuwa Mzee watu amefariki dunia akiwa kwenye
matibabu nchini Ujerumani.
Samwel John Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu
mkubwa sana. Si hivyo tu, sisi wengine pia kwa kiasi flani Hata kukua
kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu
alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika
tanzia hii ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa namna nilivyofungamana naye
binafsi na namna nilivyomshuhudia katika kazi zake mbalimbali za
uongozi.
Samwel Sitta ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa Babu yangu.
Tukiwa Bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo 'babu' kwa
mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa. Labda siku
za usoni 'vinote' (vimemo) hivi vinaweza kuchapishwa pindi watafiti
watakapokuwa wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu. Hivyo siku
zote za maisha yetu nilimuita babu.
Disemba 29, 2005 mzee Sitta aliniapisha kiapo cha ubunge tarehe. Maneno
ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi
niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyo hiyo jioni.
Baada ya kula kiapo cha Utii na cha uaminifu kawaida Wabunge hupewa
mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi.
Kwangu haikuwa hivyo, Mzee Sitta alinikumbatia na kuniambia "Utakuwa
Kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future (unayo
kesho njema)". Maneno haya hayajawahi kunitoka katika kumbukumbu zangu,
ni maneno ya faraja na msukumo wa kunitaka kwenda mbele kila ninapopata
misukosuko ya kisiasa. Mara kadhaa yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na
kunikumbusha juu ya maneno yake haya na kunitia moyo.
Babu Sitta alikuwa Mlezi wa wanasiasa vijana, binafsi amenilea na
kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Tano (Form
Five) katika Shule ya Sekondari ya Galanos ya jijini Tanga, nikisomea
mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE). Hali ya hewa ya jiji la
Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa mara kwa mara. Lakini pia
sikupenda kusoma HGE, nilitaka kusoma Hisabati badala ya Historia.
Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda
Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo
la Hisabati kidato cha Tano na Sita. Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa
kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, ndugu Ndeki alisoma
pamoja na Samwel Sitta.
Kipindi hicho Mzee Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion
Centre (IPC) mara kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments
Centre (TIC) mara baada ya kuwa mbunge wa Urambo kwa miaka 20 (1975 -
1995). Nikaenda Ofisi za IPC, zilizokuwa mahala ambapo leo ni Benki ya
CRDB Tawi la Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama
nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona.
Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu hata kwa akika chache
tu. Akaniruhusu.
Nilipofika Mzee Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa.
Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya
Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo. Alipoyasoma
akaniambia, "wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo
yako unaweza kusoma shule yeyote nchini ya chaguo lako". Akainua simu
akampigia ndugu Ndeki kumuomba anihamishe.
Kisha akaniandikia kikaratasi niende Wizarani muda ule ule. Nilipofika
Wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo. Nilipotoka
nje ya Wizara nikakutana na kijana mwengine, Godfrey Hiluka, anaomba
uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga Iringa.
Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo
ni mbaya sana.
Nikarudi kwa Mkurugenzi. Mtumishi aliyenijazia fomu za Uhamisho (Mzee wa
Makamo) aliponiona narudi na kumwambia sitaki kwenda Mazengo, akachukua
fomu zangu za uhamisho na akachukua 'kifuta - wino' (whiteout) akafuta
Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira "nyie watoto wa
wakubwa bwana!"Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga kusoma Uchumi,
Jiografia na Hisabati (EGM).
Samwel John Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni, mpaka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent nchini
Ujerumani. Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya
Kimataifa mwaka 2004 nilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua
kuunganisha makampuni ya Kijerumani na makampuni ya Tanzania kwa
kuandika mradi wa kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na
kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.
Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Mzee Sitta
akawa mstari mbele kuhakikisha Mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa
umakini kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo. Mafungamano yetu
hayakuishia hapo, mwaka mmoja baadaye tukakutana na Mzee Sitta Bungeni,
yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa
Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake kwangu ukaendelea mpaka mauti
yalipomkuta leo mapema asubuhi. Taifa limepoteza Kiongozi mzalendo,
lakini mimi nimepoteza pia 'babu Mlezi'.
Samwel John Sitta alikuwa Mwanamageuzi (Reformer), na kupitia
uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa
shughuli za Bunge akiwa Spika wa Bunge kwa miaka mitano. Sisi
tuliohudumu kwenye Bunge la tisa chini yake, tukimwita Spika wa Viwango
na Kasi, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi
yake ya Kikatiba.
Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Wabunge yanakuwa yanayolingana na
hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawa
sawa. Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana
kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu Edward Lowasa katika kuleta
mabadiliko hayo.
Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta
ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo badala yake.
Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile.
Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Edward Lowasa ataweza kusemea
hili siku za usoni.
Samwel Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa
ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na
kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge, hususan Kamati za Usimamizi
wa Serikali, zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu
wa Kanuni.
Wakati wa Bunge la 8 chini ya mzee Pius Msekwa, Taarifa za CAG
hazikuwahi kusomwa hata mara moja bungeni. Ni kutokana na mabadiliko
haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC ) ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi
ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya Wabunge wazee.
Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi nyengine ya
namna ya malezi ya kiuongozi yalifanywa na Spika Sitta. Sikuwa nimejaza
fomu kuomba hata ujumbe wa Kamati ya POAC. Wakati huo ulikuwa ni wakati
wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa na Waziri wa
Nishati Hotelini nchini Uingereza kwa siri).
Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani (Kamati
iliyoundwa na Rais kuchunguza mikataba na sheria za madini) nikiwa na
Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia simu,
akaniambia "Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge. Nimekuteua
Kamati ya POAC ambayo ni Kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya
Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa Kamati hii, lakini nahitaji damu
changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge. Naomba unikubalie na kesho
uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana
nimeshafanya kazi yangu".
Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa mjumbe wa
Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya marehemu Abdallah Kigoda, ama Kamati
ya Nishati na Madini chini ya Mzee William Shelukindo. Lakini ombi la
Mzee ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na kuwa mmoja wa washauri wakuu
wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya Mzee John Momose Cheyo
na Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dkt. Willibrod Peter Slaa. Ilikuwa ni
Bunge lenye meno kweli kweli.
Spika Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya maamuzi ambayo
wakati mwengine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni
masuala ya 'Hoja Binafsi ya Buzwagi' na 'Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu
(EPA)'. Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa Wabunge wenye hoja hizo,
yaani mimi na Dkt. Wilbroad Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa
kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja
hizi na hivyo Waziri Mkuu Edward Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu
sana wa kuegemea upande wa Serikali.
Hoja ya dkt Slaa akaitupa kuwa 'Ni makaratasi ya kuokoteza'. Hoja yangu
akaiingiza Bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu Bungeni baada ya
kuwasilisha hoja hiyo. Wananchi walimkasirikia sana. Siku moja usiku,
nikiwa nyumbani kwa ndugu Freeman Mbowe Mikocheni, Spika Sitta
akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa ujumbe wa
simu (sms), akanitaka niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na
uwezo huo. Nchi ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba 2007. Samwel Sitta
alijua namna ya kuisoma nchi, na akamua kuwapa wananchi watakacho,
wakati mwengine.
Mwezi Novemba, katika kujibu kiu ya wananchi kuhusu uwajibikaji na
kufuta makosa ya Buzwagi na EPA, Spika alisimamia kuundwa kwa Kamati
Teule kuchunguza suala la Mkataba wa Richmond. Yaliyofuata yalikuwa
historia. Taarifa ya Kamati Teule husika ilipelekea kuanguka kwa
Serikali kwa mara ya kwanza katika hsitoria ya Tanzania. Waziri Mkuu
Edward Lowasa alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, Baraza la Mawaziri
likavunjika na Serikali mpya kuundwa chini ya Waziri Mkuu mpya, ndugu
Mizengo Pinda. Spika Samwel Sitta akawa ni Spika wa pili wa nchi yetu
aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya uspika
wake.
Mzee Msekwa yeye alikaa kwenye Uspika kwa miaka 13. Miaka 10 na Waziri
Mkuu mmoja, ndugu Sumaye. Akianzia Uspika Mwaka 1993. Mwaka mmoja mbele
akishuhudia mabadiliko ya Mawaziri Wakuu, kutoka mzee John Malecela
kwenda kwa mzee Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Samwel
Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa Viwango mpaka
alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Sifa nyengine ya Spika Sitta ni Uungwana, alikuwa mwepesi mno wa kuomba
msamaha pale alipokosea. Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza
Bungeni Mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo Mzee Cheyo hakufanya.
Baadhi yetu tukakasirishwa sana na kitendo kile. Nikaenda kumwona Mzee
Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile.
Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi John Cheyo. Tukiwa kwenye
Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu, Mzee Sitta
akamwomba radhi Mzee Cheyo.
Nikikumbuka kisa hiki hutabasamu, maana Jaji Werema, aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu? Mzee
Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati tukiwa
tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema "John, naomba radhi kwa tukio
lililotokea Bungeni wiki iliyopita. Sijui nilikuwa nina nini siku
hiyo?, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka
kunitoa, nisamehe Mzee mwenzangu".
Kicheko ukumbi mzima na mzee John Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye
akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja Kitabu
"Bunge lenye Meno".
Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika wa Kasi na Viwango
Samwel John Sitta? Mwanasiasa Shupavu, Jasiri, Mwenye Ngozi Ngumu,
Mbabe, Mnyenyekevu inapobidi na mwenye Uthubutu. Tangulia Babu. Tangulia
Mjukuu wa Fundikira. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta.
Ingawa umeondoka duniani, bado unaishi kupitia kazi zako za Kizalendo
kwa Nchi yetu.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 7, 2016
Dodoma
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA