Kijo-Bisimba aikubali serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli, anena haya.


MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo- Bisimba amesema, serikali ya awamu ya tano imefanya mabadiliko ya msingi katika kupunguza rushwa na ubadhirifu.



Dk Kijo-Bisimba amesema jana wakati wa uzinduzi wa taarifa yake ya Haki za Kisiasa na Kiraia ambayo ni ya kwanza na ya aina yake nchini Tanzania iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya siku ya haki za binadamu ulimwenguni.


Amesema pia katika serikali ya awamu ya tano kumekuwa na muelekeo chanya katika ulinzi wa wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi, japo matukio ya kujichukulia sheria mikononi yamekithiri na kuhatarisha haki ya kuishi nchini.


“Suala hili limepewa mtazamo wa kitaifa likitolewa matamko na viongozi wakuu wa serikali, akiwemo Waziri Mkuu,” amesema Bisimba.


Amesema serikali kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na asasi za kiraia zinapaswa kuchukua hatua kutoa elimu na kuongeza uelewa wa haki za kiraia na kisiasa kwa jamii.


Katika hatua nyingine, Dk. Kijo-Bisimba alisema utafiti huo wa mtazamo wa haki za kisiasa na kiraia ni njia mpya ya kuweka kumbukumbu na kukusanya mitazamo ya watu katika ngazi ya jamii kuhusu ulinzi wa haki za kiasia na kiraia kama sehemu ya msingi ya kupata matokeo ya utafiti huo.


Amesema ripoti hiyo ni zao la utafiti unaofanywa kila mwaka na LHRC pamoja na wadau wao katika kuangalia mwenendo wa hali ya haki za kiraia na kisiasa.


“Ripoti hii imejikiti katika masuala sita ya haki za kiraia na kisiasa ambayo ni uhuru wa kujieleza, haki ya kupiga kura, uhuru wa kukusanyika, haki ya kuishi kwa upande wa mauaji na ukatili mikononi mwa vyombo vya dola, kujichukulia sheria mkononi na mauaji yanayotokana na imani za kishirikina,” amesema.

Chapisha Maoni

0 Maoni