Kisa na mkasa mzima mkurugenzi mkuu NIMR kutenguliwa, soma hapa

[​IMG]

EVANS MAGEGE NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM



RAIS Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela.

Uteuzi huo umetenguliwa ikiwa ni siku moja tu baada ya Dk. Mwele kutangaza matokeo ya utafiti wa homa ya zika aliosema ulifanywa na NIMR kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Bugando (Cuhas) hivi karibuni.

Katika matokeo hayo aliyoyatangaza Alhamisi wiki hii, Dk. Mwele, alisema asilimia 43.8 ya watoto wachanga 80 kati ya watu 533 ambao walichukuliwa sampuli na kupimwa, wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya zika.

Alisema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando hivi karibuni, umethibitishwa kuwapo tatizo hilo.

“Tulipima sampuli za damu kutoka kwa watu 533. Kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya waliopimwa asilimia 15.6 waligundulika wameambukizwa virusi vya zika.

“Kati ya wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, asilimia 43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya zika. Utafiti unaendelea kujua ukubwa wa tatizo hili,” alisema.

Matokeo hayo yaliibua mkanganyiko serikalini na juzi ilimlazimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ya kumuita Dk. Mwele ofisini kwake ili atoe ufafanuzi wa utafiti huo.

Baada ya Ummy kupewa ufafanuzi katika kikao chao cha ndani, pia alizungumza na waandishi wa habari na kuwataka Watanzania kutokuwa na hofu, kwa sababu haijathibitishwa kuwapo kwa virusi vya zika hapa nchini.

Alisisitiza kuwa matokeo yaliyotangazwa na Dk. Mwele ni utafiti wa awali na wizara yake ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza matokeo hayo baada ya kupimwa tena kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika mkutano huo wa waandishi wa habari ulioitishwa na Ummy huku akiwa na Naibu wake, Dk. Hamis Kigwangalla na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi, Dk. Mwele naye alizungumza kwa kusema huenda taarifa yake haikueleweka kwa wanahabari.

Dk. Mwele alisema matokeo ya awali ya utafiti wao walioufanya yalionyesha kuwapo kwa virusi hivyo, lakini watu waliokutwa navyo hawakuonyesha dalili wala madhara yanayohusiana na zika, huku wakiwa hawana mamlaka ya kutangaza kama homa hiyo ipo bali wizara ndiyo huthibitisha kwa utaratibu maalumu uliowekwa.

Licha ya kutoa ufafanuzi wa matokeo ya utafiti huo katika kikao cha ndani, lakini saa tano usiku wa juzi, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, alituma taarifa kwa vyombo vya habari iliyohusu Magufuli kutengua uteuzi wa Dk. Mwele.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Ikulu haikufafanua sababu za kutenguliwa kwa uteuzi wa Dk. Mwele, lakini kumekuwa na hisia kwamba pengine taarifa ya utafiti wa zika ndiyo iliyogharimu nafasi yake, huku wengine wakimtetea kuwa yeye hakutangaza kuwapo kwa homa hiyo bali alitangaza matokeo ya utafiti wao.

MTANZANIA Jumapili lilipomuuliza Msigwa kwa simu, sababu za Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Dk. Mwele, alijibu kwamba hajui sababu kwa kuwa rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua na kutengua.

“Mimi ni mtu wa kupewa taarifa na kuiwasilisha kwenu, kwahiyo siwezi kujua sababu na sina uwezo wa kuingilia uamuzi wa rais, nadhani utakuwa umenielewa,” alisema Msigwa.

Baada ya Dk. Mwele kutenguliwa, Msigwa alituma tena taarifa ya uteuzi kwa vyombo vya habari jana kuwa Rais Magufuli amemteua Profesa Yunus Mgaya kuziba nafasi hiyo.



MAJIBU YA DK. MWELE

Baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa nafasi yake, Dk. Mwele, alijibu maoni na pole alizopewa kupitia ukurasa wake katika mtandao wa jamii wa Twitter.

Kupitia ukurasa huo, Dk. Mwele aliwashukuru wachangiaji waliompa pole ya uteuzi wake kutenguliwa na alisema atasonga mbele kwa msaada wa Mungu.

Alisema kuwa alipewa dhamana kaitumikia na anamshukuru Mungu kwa nafasi ya kuwatumikia Watanzania.

Kutenguliwa kwa uteuzi wake, kunaleta pigo la pili katika familia yao baada ya mama yake, Anne Kilango Malecela.

Anne Kilango aliyekuwa Mbunge wa Same Mashariki kabla ya kuangushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, lakini Aprili 11, mwaka huu Rais Magufuli alitengua uteuzi wake.

Rais Magufuli alitengua uteuzi wake baada ya kupewa taarifa zisizo sahihi kuwa mkoa huo hauna watumishi hewa, lakini baadaye alibaini kuwapo watumishi hewa 45 baada ya kutuma timu iliyokwenda kufanya uchunguzi.

Katika hatua nyingine, Profesa Kambi, alisisitiza tena jana kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa hata mmoja aliyeripotiwa kuwa na virusi vya zika.

Alisema kama nchi, upo utaratibu wa kupata taarifa za magonjwa kama hayo na kupitia utaratibu huo hakuna taarifa waliyopokea kwamba kuna mgonjwa wa zika.

“Tanzania ina wajibu wa kutoa taarifa kwa magonjwa haya kwa kufuata utaratibu kwa sababu ni ya kimataifa,” alisema na kuongeza:

“Taarifa hizo lazima zifike wizarani, zikaguliwe, tuwasiliane na WHO na zinatolewa na mratibu wa masuala haya ya kutoa taarifa, kupitia utaratibu huo hatujapata taarifa kwamba kuna tatizo la zika nchini.

“Nawahasa wataalamu, wanasayansi na watafiti wenzangu, wanapotaka kutoa taarifa zinazohusu masuala yoyote yale ni lazima wajihakikishie usahihi wa hizo taarifa kabla ya kuzitoa, wajue kuna taratibu za kutoa taarifa za magonjwa yanayotakiwa kutolewa kimataifa.

“Na tunapowasiliana na jamii zetu wajue kwamba sisi wanasayansi lazima tuzitoe katika lugha ambayo itakuwa rahisi kueleweka na hazitatoa mkanganyiko katika jamii zetu.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa WHO hapa nchini, Dk. Grace Suguti, alisema hawajapokea taarifa yoyote toka wizarani inayoeleza kuwapo kwa mgonjwa mwenye zika.

“Tupo hapa nchini kufanya kazi na wizara katika ufuatiliaji wa magonjwa, ambao unafanyika kila siku katika maeneo ya afya na katika jamii, taarifa huletwa wizarani na wao wanatutaarifu na sisi tunaishirikisha WHO na kwenye tovuti zetu, hatujapokea taarifa yoyote kwamba kuna mgonjwa wa zika Tanzania katika ofisi zetu zilizopo hapa Tanzania,” alisema Dk. Suguti.

MWELE NI NANI?

Dk. Mwele mwenye umri wa miaka 53, ni mtoto wa Waziri Mkuu mstaafu, Samwel Malecela.

Ni mwanamke wa kwanza kutumikia nafasi ya ukurugenzi mkuu wa NIMR na amefanya kazi katika ofisi hiyo kwa miaka 24, huku ikielezwa kuwa alianza katika nafasi za chini za utendaji.

Mwaka jana alikuwa ni mmoja kati ya makada 42 wa CCM waliochukua fomu za kutia nia ya kugombea urais, lakini hakuingia tano bora ya mchakato wa ndani wa chama hicho.

Elimu yake ya juu kuanzia shahada ya kwanza aliipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na baadaye Shahada ya Uzamivu aliipata katika Chuo Kikuu Cha London, Uingereza na alijikita katika masomo ya afya ya binadamu na dawa za kitropiki.

Pia ni Mwenyekiti wa Muungano wa Watafiti wa Masuala ya Afya (MRCC) hapa nchini na mshauri wa bodi ya juhudi za ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika nyanja ya afya hapa nchini (IPPPH).

Dk. Mwele ni mjumbe wa mipango mikakati ya WHO katika masuala ya magonjwa ya kitropiki.

Pia ni mjumbe wa kimataifa wa Bodi ya ‘Grand Challenges Canada’ na mjumbe wa Taasisi ya Sayansi ya Afya ya Chuo cha Morehouse ya Marekani.

Chanzo: Mtanzania

Chapisha Maoni

0 Maoni