Madereva wazembe kulowekwa selo baada ya kulipa faini


JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini limesema litachukua hatua kali kwa kuweka mahabusu madereva watakaokiuka sheria za usalama barabarani katika kipindi hiki cha sikukuu badala ya kulipa faini kama ilivyozoeleka.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi wa Kikosi hicho, Mohammed Mpinga, alipozungumza na vyombo vya habari akisema kutoza faini kumekuwa hakuwafanyi madereva kuacha kuvunja sheria.

“Kitendo cha kutoza faini, kimekuwa kikiwafanya madereva kuvunja sheria kwa makusudi, wakijua wakikamatwa watalipa faini na kuachwa,” alisema Mpinga.

Mpinga alisema katika kipindi hiki, watu wengi hupenda kusafiri kwenda maeneo mbalimbali na hivyo kuongeza matumizi ya vyombo vya moto barabarani ambapo pia huambatana na starehe nyingi ikiwa ni pamoja na ulevi kwa madereva.

Alieleza kutokana na hali hiyo ya starehe na ulevi, madereva wengi hupoteza umakini na kushindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hatimaye kusababisha ajali ambazo hugharimu maisha ya watu wengi.

Alifafanua, kwamba kipindi hiki madereva huwa na haraka na huendesha kwa mwendo kasi, hunywa pombe, hupenda kupita magari ambayo ya mbele yao bila hadhari na hufanya makosa ya kizembe yanayohatarisha maisha.

Kamanda Mpinga alisema kwa kutambua hilo, wamejipanga ili kuwatia mbaroni madereva hao na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, alisema katika kipindi cha kuelekea mwishoni na mwanzoni mwa mwaka mpya, wamekuwa wakifanya operesheni katika barabara zote, stendi za mabasi ili kukagua ubora wa mabasi, mikanda, kupima ulevi madereva, uzidishaji abiria na nauli.

Alisema katika operesheni hii inayoendelea mikoani kwa kipindi kifupi madereva wa mabasi ya abiria wamekamatwa kwa mwendo kasi wa zaidi ya kilometa 90 kwa saa, ambapo katika mikoa tofauti jumla ya madereva 277 walifikishwa mahakamani wakitokea mahabusu na kulipa faini ya kati ya Sh. 300,000 na Sh 600,000

Chapisha Maoni

0 Maoni