Wanafamilia wakiwa wamelizunguka kaburi la marehemu Ngaga aliyezikwa kaburi moja na kondoo pamoja na kuku mweusi jana kwenye kitongoji cha Mkawaganga kijiji cha Mbigili wilaya ya Kilolo mkoani Iringa
Mganga wa kienyeji Galasiano Nyenza (kulia) akiwa na mtoto wa marehemu Andrea Ngaga ,Kurugenzi Ngaga kushoto baada ya kufanyika kwa mazishi ya kimila katika kijiji cha Mbigili Kilolo kwa marehemu kuzikwa kaburi moja na kondoo na kuku mweusi
Mganga Nyenza aliyeongoza mazishi hayo katikati akiwa na baadhi ya ndugu kando ya kaburi
Waombolezaji wakitoka kuzika
Marehemu enzi za uhai wake
Nyumbani kwa marehemu waombolezaji wakiwa kwenye foleni- Picha zote kwa hisani ya MatukiodaimaBlog
MAMIA ya wakazi wa kijiji cha Mbigili na mji wa Ilula katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wamefurika katika mazishi ya aina yake yaliyofanyika katika kitongoji cha Mkawaganga kijiji cha Mbigili wilaya ya Kilolo kushuhudia mazishi hayo ya kihistoria baada ya mzee mmoja aliyefariki dunia ghafla kuzikwa kaburi moja na kondoo pamoja na kuku mweusi.
Tukio hilo limetokea jana wakati wa mazishi ya mzee Andrea Ngaga (90) mkazi wa kitongoji cha Mkawaganga aliyekuwa akijishughulisha na kazi za uganga wa kienyeji kijijini hapo enzi za uhai wake .
Baadhi ya wananchi waliofika katika mazishi hayo walisema walilazimika kusitisha shughuli zao za shamba na biashara na kufika kushuhudia mazishi hayo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika katika kijiji hicho.
Mmoja wa wananchi hao John Mfaligoha alisema kuwa kabla ya kifo marehemu huyo alipata kuwaeleza aina ya mazishi yake yatakavyokuwa.
Hivyo alisema wananchi walio wengi walifika kutaka kushuhudia tukio hilo la mazishi na ndio sababu iliyopelekea wananchi kusukumana msibani wakati wa mazishi kwa kila mmoja kutaka kushuhudia tukio hilo la kihistoria katika kijiji hicho.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mbigili Ibrahim Rashid (46) alisema amezaliwa katika kijiji hicho tukio hilo ni la kwanza kufanyika hajapata kushuhudia mazishi ya aina hiyo zaidi ya kusikia katika vyombo vya habari kutoka nje ya kijiji chake na kuwa mazishi hayo yamefanyika kimila zaidi na kimsingi huwa marehemu anachagua mtu wa kuzikwa nae kabla ya kifo .
Ila hakuweza kuacha maagizo zaidi ya kuomba pindi atakapokufa kuzikwa kimila na ndiyo sababu aliyeongoza mazishi hayo ni mganga wa kienyeji kutoka Ifunda wilaya ya Iringa Galasiano Mfaume Nyeza ambaye ni baba mdogo na marehemu huyo .
Mtendaji wa serikali ya kijiji hicho cha Mbigili Thabith Kalolo alisema kuwa kimsingi hakuna kosa lolote familia ambalo wamelifanya kwa kufanya mazishi ya aina hiyo kwani serikali haiingilii uhuru wa wananchi wake kuamini masuala ya mila na kuwa iwapo mazishi hayo yangekiuka haki za binadamu mwingine mfano kama wangekata kumzika marehemu na binadamu mwingine aliyehai hapa isingewezekana ila kwa kumzika na kondoo na kuku mweusi hakuna shida .
Hata hivyo alisema tofauti ya rekodi ya misiba iliyopata kutokea katika kijiji hicho ,msiba wa mganga huyo umevunja rekodi kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu na kuwa msiba uliovunja rekodi kwa michango ni huo pekee kwani misiba mingine fedha za rambi rambi huwa ni kati ya Tsh 300000 hadi 500000 mwisho ila msiba huo rambi rambi ni zaidi ya Tsh milioni 1.3
Mtoto wa marehemu Kurugenzi Ngaga alisema kuwa babake alifariki dunia juzi Desemba 20 majira ya saa 6 usiku mwakla huu kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo ya chembe ya Moyo na kuwa ameacha wajane wawili na watoto 19.
Kurugenzi alisema kimila kama ingekuwa zamani marehemu angezikwa na mjukuu wake aliyemteua kushika mikoba yake ila kutokana na mambo ya mila kwa sasa kupewa kisogo waliona ni vyema wakamzika na kondoo na kuku huyo mweusi.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA