Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo mchana na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
“Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,” amesema.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Profesa Maghembe amesema hadi kufikia Desemba 2015 wakati Faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya kuwalinda tembo na faru. Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu, Iddi Mfunda; Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Freddy Manongi; Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Simon Mduma; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Alexander Songorwa na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Nollasco Ngowe.
Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.
Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA