KUNA mfumko mkubwa wa kilimo cha bangi nchini; na sasa baadhi ya watu wanaendesha kilimo cha dawa hizo za kulevya kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji.
Wengine wanalima bangi katikati ya hifadhi za misitu ya taifa na juu ya milima, ambako ni vigumu kwa usafiri wa gari au pikipiki.
Wakati kilimo cha bangi kinashamiri, pia kumekuwepo na ongezeko la watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na dawa zingine za kulevya kama mirungi, kokeni na heroin. Ongezeko hilo linatokana na kazi inayofanywa na kikosi kazi, kinachoundwa na taasisi mbalimbali kuzidisha msako.
Kikosi kazi hicho kinaundwa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Wananchi, Magereza na Takukuru.
Kikosi kazi hicho kinapambana na watuhumiwa wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza jana, Kamanda wa Kikosi cha Dawa za Kulevya nchini, Mihayo Msikhela alisema mwaka huu zimekamatwa kilo 84.183.6 za dawa za kulevya, ukilinganisha na kilo 35,373 zilizokamatwa mwaka jana. Idadi ya watuhumiwa pia imeongezeka kutoka 14,339 mwaka jana hadi kufikia watuhumiwa 18,893 waliokamatwa mwaka huu.
Kilimo cha bangi Akizungumzia kilimo cha bangi, Msikhela alisema kikosi kazi hicho, kimebaini kulimwa zao hilo kwa wingi katika safu za milima mbalimbali nchini, ambako kutokana na jiografia ya huko ni vigumu kufika kwa usafiri wa gari au pikipiki.
“Bangi ni janga la taifa, watu wamegeukia kilimo cha bangi na kuacha kulima mazao mengine katika maeneo mengi nchini. Walimaji wanalima katika maeneo ambako ni ngumu kuyafikia kwa usafiri wa magari au pikipiki,” alisema Msikhela.
Alisema kutokana na msako mkali wa kikosi kazi hiyo, mwaka huu kumekuwa na kesi nyingi na kiasi kikubwa cha bangi iliyokamatwa ukilinganishwa na mwaka jana.
Alisema mwaka huu kumekuwa na kesi 8,159 zilizohusu bangi wakati mwaka jana kulikuwa na kesi 6,752. Ongezeko la kesi za bangi ni 1,407. Kiasi cha bangi ambacho kimekamawa mwaka huu ni kilo 65,804, tofauti na mwaka jana ambako bangi iliyokamatwa ilikuwa ni kilo 20,066.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA