BODI ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema hakuna malalamiko yaliyowasilishwa kwao kutoka timu yoyote juu ya Simba kuwachezesha 'visivyo halali' wachezaji wake wawili wa kigeni.
Baada ya ushindi wa Simba wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda kwenye mchezo wa Jumapili iliyopita, zilizagaa taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii zikieleza kuwa licha ya Simba kushinda mchezo huo, Yanga inapaswa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kutokana na Simba kuwachezesha Daniel Agyei na James Kotei (wote kutoka Ghana) bila ya kuwa na vibali vya kufanya kazi nchini pamoja na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Hamad Yahya akizungumza jana kwenye kituo kimoja cha radio jijini Dar es Salaam, alisema taarifa zilizozagaa mitaani hazina mantiki kwa kuwa hawajapokea barua yoyote ya timu ikiilalamikia Simba.
“Hakuna kesi au malalamiko yoyote yaliyofika mezani kwetu zaidi tumesikia timu ya Ndanda ikiilalamikia Simba kwa kuchezesha wachezaji wasiokuwa na kibali.
“Kanuni zetu ziko wazi, hivyo hatuwezi kuzungumza mengi kama wataleta malalamiko rasmi basi tutaangalia kanuni zinasemaje kwani sisi mpaka sasa hatujaruhusu wachezaji wasiokuwa na leseni kucheza mechi,” alisema Yahya.
Aidha, alisema suala la vibali vya kufanyia kazi nchini hayo ni mambo ya taratibu za nchi na watu wa Uhamiaji ndio wanaohusika navyo.
"Siwezi kulizungumzia sana hili kwa sababu halipo upande wangu," alisema Yahya.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alisema taarifa za kutokuwapo kwa vibali kwa wachezaji hao zinaenezwa na wapinzani wao ambao walitegemea Simba ingepoteza mchezo wao dhidi ya Ndanda.
“Niseme hizo taarifa ni za uzushi ambazo zimeletwa na wapinzani kwenye ligi ambao waliamini kwamba tutapoteza ule mchezo ili wao waendelee kuwa juu ya msimamo wa ligi kwa hiyo ushindi wetu haujawapendaza ndio maana wameamua kuendesha vita ya maneno ya uongo na uchochezi.
"Simba imekamilisha taratibu zote za usajili ambazo zipo ndani ya kanuni zetu za VPL, baada ya kukidhi mahitaji yote, wachezaji husika walipewa leseni na TFF na ndio ambazo zilitumiwa siku ya mchezo kwa hiyo vijana wetu walikuwa na vigezo vyote vya kucheza dhidi ya Ndanda kulingana na kanuni,” alisema Kaburu.
Simba ambayo Jumamosi itashuka Uwanja wa Uhuru kucheza na JKT Ruvu, inaongoza ligi baada ya kufikisha pointi 38 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 36 huku Azam wakishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 26 baada ya Jumapili iliyopita kushindwa kufungana na African Lyon.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA