Baada ya vuta nikuvute iliyochukua sura mpya nchini Kongo na kupelekea zaidi ya watu 40 kupoteza maisha hivi karibuni katika maandamano ya kutaka Rais Kabila aondoke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo tokea mwaka 2001, hatimaye serikali na upinzani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
zimefikia muafaka, ambapo Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo amekubali kung’atuka uongozini mwishoni mwa mwaka ujao 2017.
zimefikia muafaka, ambapo Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo amekubali kung’atuka uongozini mwishoni mwa mwaka ujao 2017.
Muafaka huo ni matunda ya mazungumzo baina ya wawakilishi wa serikali na vyama vya upinzani chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki yaliyofanyika mjini Kinshasa mapema jana, siku moja baada ya wapatanishi hao kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Kabila pamoja na kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo Etienne Tshisekedi kuhusiana na mgogoro huo wa kisiasa.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano hayo, Kabila hatabadilisha katiba kwa lengo la kushiriki katika uchaguzi mkuu mwaka ujao huku utawala wake wa mihula miwili ambao ulimalizika Desemba 19 mwaka huu ukiongezwa hadi mwishoni mwa mwaka ujao na wala sio Aprili 2018 kama ilivyopendekezwa awali.
Marcel Utembi, Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo amesema Rais Kabila ataondoka madarakani mwishoni mwa mwaka ujao, ili kupisha uchaguzi mkuu ambao utafanyika kabla ya kumalizika mwaka huo, mbali na kuteua Waziri Mkuu kutoka muungano mkuu wa upinzani unaoongozwa na Tshisekedi.
Muafaka huo unatazamiwa kutiwa saini rasmi hii leo ingawaje inaarifiwa kuwa Rais Kabila na Tshisekedi hawatatia sahihi wenyewe, na badala yake kazi hiyo itafanywa na wajumbe wao; jambo ambalo linawatia wasiwasi wadadisi wa mambo ambao wanahisi huenda makubaliano hayo yasiheshimiwe wala kuchukuliwa kwa uzito.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA