JPM kutikisa tena baraza la mawaziri, hawa hapa watajwa kumrithi Prof. Muhongo


UAMUZI wa Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa rafiki yake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ni wa tatu tangu aunde Serikali, sasa analazimika kukuna kichwa kuteua waziri mwingine kushika nafasi hiyo.

Wakati hilo likisubiriwa, wanasiasa na wasomi wameeleza kuwa hakuna waziri atakayeteuliwa na kusalimika katika wizara hiyo, kwa madai kwamba inazungukwa na rushwa kubwa za kimataifa, mikataba mibovu na kuingiliwa uamuzi na Ikulu.

“Ndiyo maana tumekuwa tukipendekeza kugawanywa kwa wizara hii kwa maana ya kuwa na wizara mbili; ya Nishati na ya Madini,” alisema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema.

Mei 20 mwaka jana, kwa mara ya kwanza Rais alitengua uteuzi wa rafiki yake mwingine wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga na nafasi yake kuzibwa na Mwigulu Nchemba, ambaye awali alikuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, huku Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba akiteuliwa kuchukua mikoba ya Mwigulu.

Mabadiliko ya pili ya Baraza la Mawaziri yalifanyika Machi 23, baada ya mkuu huyo wa nchi kumteua Dk Harrison Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuchukua nafasi na Nape Nnauye ambaye aliachwa.

Katika mabadiliko hayo, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye awali aliteuliwa na Rais kuwa mbunge, alipewa Wizara ya Katiba na Sheria ambayo kabla ya mabadiliko hayo ilikuwa ikiongozwa na Dk Mwakyembe.

Rais hakusubiri Profesa Muhongo ajitathmini, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa sakata la kiwango cha madini kwenye kontena, alikiri kuwa na urafiki na Mbunge huyo wa Musoma Vijijini na hilo halikumfanya asite kumwajibisha, kwani baada ya kuisoma ripoti hiyo, Ikulu ilituma taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuwa Rais ametengua uteuzi wa mtaalamu huyo wa miamba.

Mara zote mbili alizofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli amekuwa na utaratibu wa kuhamisha mawaziri kutoka wizara moja kwenda nyingine au kuteua wabunge na kuwapa wizara.

Katika mabadiliko hayo mawili aliyofanya, ni Dk Tizeba pekee ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka miongoni mwa wabunge wa majimbo.

Iwapo Rais Magufuli atazingatia utaratibu wa mtangulizi wake Jakaya Kikwete kuteua waziri kutoka mkoa ambao waziri aliyeondoka anatoka, huenda nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Muhongo ikajazwa na wabunge kutoka mkoa wa Mara.

Baadhi ya wabunge wa CCM kutoka mkoani Mara ni Boniface Getere (Bunda Vijijini), Nimrod Mkono (Butiama), Vedastus Mathayo (Musoma Mjini), Kangi Lugola (Mwibara) na Lameck Airo (Rorya).

Pia, kauli ya CCM jana kwamba imechoshwa na mauaji yanayotokea kila uchwao mkoani Pwani, ni sawa na kutuma ujumbe kwa Rais Magufuli kwamba kuna tatizo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuchochea ukubwa wa mabadiliko.

Utaratibu

Miongoni mwa wateule wake ni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson. Novemba mwaka 2015 Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani alichukua fomu za kuwania uspika kupitia CCM kabla ya kujitoa dakika za lala salama kisha akateuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge wa viti maalumu.

Baada ya kujitoa, alijitosa kuwania unaibu Spika ambapo wabunge 250 walimpigia kura ya ndiyo.

Wengine walioteuliwa kuwa wabunge na akawapa wizara ni; Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustino Mahiga, Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Philip Mpango (Fedha) na Dk Abdallah Posi  ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu.

Hata hivyo, Posi aliteuliwa kuwa balozi kufuatia dosari ya kikatiba katika uteuzi wa wabunge 10 wa kuteuliwa na Rais ambapo Ibara ya 66 (1)(e) inaeleza katika nafasi hizo,  wabunge watano au zaidi wanapaswa kuwa wanawake. Baada ya kuondolewa Posi, Rais alimteua Anne Kilango kuwa Mbunge.

Hivi karibuni, Rais alimteua Salma Kikwete kuwa mbunge na kufanya idadi ya wabunge wanawake wa kuteuliwa na Rais kuwa wanne, kubaki nafasi moja ya uteuzi ambayo ni lazima awe mwanamke.

Mwingine aliyeteuliwa na Rais kuwa mbunge ni Abdlallah Bulembo na kufanya idadi ya wabunge walioteuliwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi bila kupewa uwaziri kuwa watatu.

Kwa mantiki hiyo, kama Rais Magufuli atazingatia utaratibu wake wa kuteua mbunge na kumpa wizara, safari hii atalazimika kuteua mbunge mwingine mwanamke.

Iwapo hatateua na kuamua kubadili utaratibu wake, huenda Salma na Kilango wakakumbukwa, huku kukiwa na kila dalili ya baadhi ya mawaziri kuhamishiwa Wizara ya Nishati na Madini.

Wanasiasa, wasomi

Katika maelezo yake, Mbowe alisema madini yanahusisha mafuta, gesi na vito hivyo vikichanganywa na nishati ni mzigo mkubwa.

Alibainisha kuwa wizara hiyo inakabiliwa na vishawishi vingi kutokana na fedha zinazopatikana kwa wawekezaji, jambo ambalo huwa ni mtego kwa mawaziri.

Huku akikosoa mikataba ambayo Serikali imeingia na wawekezaji wa sekta ya nishati na madini, Mbowe alisema ikifuatiliwa kwa undani hakuna atakayebaki salama.

“Yupo Waziri Mkuu mmoja aliondoka kwa kashfa ya wizara hii. Kusema nani atatosha ni ngumu sana kwa wizara hii,” alisisitiza Mbowe.

Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda aliitaja wizara hiyo na ya Maliasili na Utalii, kukiri kuwa ni ngumu kuziongoza.

Alidai kuwa mambo mengi yanayoikumba nchi kwa sasa ni matokeo ya nchi kuingia mikataba mibovu, hasa katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

“Tunachopaswa kufanya ni kuangalia mfumo na mikataba iliyoingiwa. Imetawaliwa na nguvu ya pesa, hakuna waziri atakayekuwa salama,” alisema Akitanda.

Kwa upande wake, kada wa Chadema na mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema:”Madini na nishati ni rasilimali zinazoongozwa kwa rushwa duniani, ni ngumu kutulia.”

Kafulila alisema nchi kadhaa duniani zinapigana kwa sababu ya nishati na madini, jambo alilodai kuwa linaakisi nchini.

Rais wa zamani wa Chama kilichofutwa cha APPT-Maendeleo, Peter Mziray alisema, “Kama Mkapa angeona mbali haya mambo yasingetokea hivi sasa. Alishiriki ubinafsishaji ambao umenufaisha wageni.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Frank Tilly alisema kinachoikumba wizara hiyo ni matokeo ya nchi kukosa muundo madhubuti wa uongozi, kusababisha viongozi kufanya mambo wanavyojisikia.

Chapisha Maoni

0 Maoni