ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema hana mpango wa kurudi nchini kwa sasa na kwamba taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina ukweli wowote.
Jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilisambaa taarifa kwamba mwanasiasa huyo ambaye aliondoka nchini baada ya kujiweka kando na chama chake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, angewasili leo nchini.
“Dk. Slaa ataingia kesho (leo) nchini na kwamba atazungumza na waandishi wa habari saa tano asubuhi,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kutokana na hilo, MTANZANIA ilimtafuta Dk. Slaa kupitia simu yake ya kiganjani akiwa nchini Canada jana, ambapo alieleza kushangazwa na taarifa hizo akisema watu wakikosa ajenda hubaki kutunga mambo.
“Mmmhh! Ninawashangaa! Unajua watu wakikosa ajenda hubaki kutunga mambo tena yasiyo ya maana…naomba mpuuze,”alisema Dk. Slaa.
Pamoja na hilo, MTANZANIA ilimwuliza ni lini atarejea nchini, alisema kwa kifupi: “Nikiwa tayari nitakujulisha wala usijali lakini hizo taarifa ni za uongo,” alisema.
Mwishoni mwa Machi, mwaka huu, gazeti hili lilifanya mahojiano na Dk. Slaa akiwa Canada ambapo pamoja na mambo mengine, alisema amemaliza masomo yake na baada ya kufanya tafakari atarejea nchini wakati wowote.
“Ni kweli nimemaliza masomo yangu. Bado napima mazingira yaliyonifanya niondoke na familia yangu. Baada ya hapo tutaangalia uwezekano wa kurejea,”alisema Dk. Slaa.
Hata hivyo, Dk. Slaa ambaye alipata kuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu mfululizo, hakuweza kuainisha mazingira yaliyomfanya aondoke nchini na kwenda kuishi ughaibuni.
Septemba, 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Dk. Slaa alijiweka kando na siasa, kwa kile alichokieleza kutofautiana na viongozi wenzake ndani ya chama chake juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
“Sina tabia ya kuyumbishwa…sina chuki na mtu yeyote, sipendi siasa za udanganyifu na propaganda. Nimeachana na siasa tangu Julai 28, 2015, baada ya kuona misingi ya chama nilichoshiriki kukijenga imepotoshwa,”alisema Dk. Slaa siku alipotangaza kuachana na siasa.
Alisema sharti la kwanza ambalo alitaka Chadema izingatie ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya Serikali ya CCM, kujisafisha dhidi ya tuhuma ya kashfa ya sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond aliyohusishwa nayo akiwa Waziri Mkuu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA