Mbunge Alia Kisa Wabunge wa Upinzani kuitwa Mabwege


Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Ester Matiko juzi jioni alikerwa na ujumbe unaodaiwa kuandikwa na Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu uliowataka wapinzani waache mambo ya kibwege.

Matiko ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, aliomba mwongozo wa Spika mara baada ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo.

Matiko aliomba mwongozo huo akitaka kupata ufafanuzi wa utaratibu unaotumika kuwachagua wabunge watakaohoji wakati Bunge linapokaa kama kamati.

Alisema katika Bunge la 11 umekuwa utaratibu wa kiti cha Spika kuchagua wabunge wengi wa CCM kuchangia hoja na hivyo muda kumalizika bila wapinzani kupata nafasi.

Mbunge huyo alisema jambo hilo limekuwa tofauti na mabunge mengine ambayo Bunge limekuwa likienda hadi saa nne usiku ili kuwapa nafasi wabunge kujadili bajeti kwa kina.

“Tukikulalamikia matokeo yake unatutumia kikaratasi kimeandikwa maneno, mambo yenu ya kibwege bwege. Yaani unawaambia wananchi wa Tarime wamechagua bwege?” alihoji Matiko.

Akijibu mwongozo huo, Zungu alisema kanuni zinatoa fursa ya kuingia katika kupitisha vifungu kwa utaratibu wa fungu. Alisema kanuni hiyo pia inatoa fursa ya vyama kupeleka majina ya wachangiaji katika kila kamati ya matumizi inapokaa kupitia bajeti.

Aliwataja waliowasishwa kwa ajili ya bajeti hiyo kuwa ni ni Matiko, Chacha Rioba (Serengeti) na mbunge mwingine wa tatu ambaye hakumtaja jina. “Unasema sijui kuna karatasi mimi nimesema, hiyo karatasi iangalie vizuri imetoka wapi? Sasa wewe unaweza ukaichukua hiyo karatasi ukaipeleka kwa katibu ili ifanyiwe kazi,” alisema Zungu.

Majibu hayo yalisababisha minong’ono miongoni mwa wabunge, lakini Zungu alisema kuwa mwongozo ni huo na kuliahirisha Bunge.

Akizungumza jana kuhusu suala hilo, Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya alisema inapofika Bunge linapokaa kama kamati ya matumizi kila chama kimekuwa kikitakiwa kupeleka majina ya wachangiaji.

Alisema kuna wakati hoja moja wanapewa wabunge hata 10 kuchangia na kwamba hata kama ni uamuzi wa kiti lakini ni lazima busara itumike.

“Wanafanya hivyo ili kuhakikisha kuwa upinzani unakosa nafasi na hiyo tumekuwa tukilalamika hata kwa Zungu,” alisema.   

Chapisha Maoni

0 Maoni