News Alert!! TRA kutaifisha mali za wakwepa kodi ya majengo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema wamiliki wa majengo nchini watakaoshindwa au kukaidi kulipa kodi ya majengo kwa wakati, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini ya Sh 75,000 au mali kutaifishwa.


Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema juzi kuwa wamiliki wana wiki tano kuanzia sasa kulipia kodi ya majengo yao vinginevyo watachukuliwa hatua. “Wale ambao hawatalipa kodi hiyo watatozwa faini Sh 75,000 kila mwezi. Wakiendelea kulimbikiza faini, tutawafikisha mahakamani kwa kutumia Sheria ya Kodi ya Mamlaka ya Miji, Sura 289.

Ikitokea wakaendelea kutokulipa, Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 itaamua ambapo TRA itakamata mali zao na kuziuza ili kufidia thamani ya tozo wanalopaswa kulipa,” alisema. Kwa mujibu wa taratibu za kodi ya majengo, TRA imeweka kiwango cha tozo kuwa ni asilimia 0.15 ya thamani ya jengo au nyumba. Kayombo alisema, watakuwa wakitoza asilimia hiyo kila mwaka ambazo zinatakiwa kulipwa Julai mosi mpaka Juni 30 mwaka unaofuata.

TRA ilipewa mamlaka na serikali ya kusimamia na kukusanya kodi ya majengo kuanzia Julai, 2016. Kwa sasa inaendelea kukusanya kodi kwenye majiji manne, manispaa 18 na miji saba. TRA kukusanya kodi ya majengo inatokana na mabadiliko ya sheria tatu zilizo chini ya Sheria za Fedha ya mwaka 2016.

Sheria hizo ni; Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, sura ya 290; Sheria ya Kodi ya Mamlaka ya Miji, sura ya 289 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA), sura ya 399. Kayombo alisema ulipaji kodi kila mwaka hautawagusa wamiliki wa nyumba za ibada (zisizo za biashara), walemavu na wazee wa miaka 60.

Chapisha Maoni

0 Maoni