SHEKHE Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salim, amewaomba wafanyabiashara wasipandishe bei ya bidhaa katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Alitoa maombi hayo jana kutokana na alichosema ni tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa zao wakati wa Mfungo huo ili kujinufaisha binafsi.
“Vyakula vinapanda katika kipindi cha Mfungo na kuwasababishia baadhi ya wafungaji kutomudu hali hiyo, vitu vinakuwa na bei kubwa kuliko miezi ya kawaida,” alisema Salim.
Alisema ni vema Waislamu kujianda katika kipindi cha kuikaribisha Ramadhan kwa kutenda yaliyo mema na kuacha mabaya yasiyompendeza Mungu.
“Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni wa kila Mwislamu, kila mmoja anatakiwa kutii kwa kufunga na wala si jambo la hiyari ni lazima, kwa kila mwumini mwenye uwezo na vigezo vya kufunga,” alisema Alhad.
Aliwataka Waislamu kuwasaidia wasiojiweza kama kukaa na yatima na kuwalisha vyakula akisema hali hiyo itawajengea misingi bora katika kumsaidia asiye na kitu.
Katika hatua nyingine, aliwataka Waislamu kuliombea amani Taifa na watu wa mkoa wa Pwani waliokabiliwa na matukio ya mauaji ya kutumia silaha akisema:
“Nawaomba Waislamu tuiombee nchi yetu ya Tanzania amani hasa wenzetu wa mkoa wa Pwani kwa majanga yaliyotokea na tuombee vyombo vyetu vya ulinzi kuimarika ili kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu.”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA