HATIMAYE Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imeanza rasmi utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kutowapangia vyuo vya kujiunga wanafunzi na badala yake kuwaacha waombe moja kwa moja kwa utashi wao.
Kwa mujibu wa tangazo lililopo kwenye tovuti ya TCU, sasa wanafunzi wanatakiwa kuomba nafasi za masomo kwa mwaka 2017/18 katika vyuo husika na siyo kwa kutumia mfumo uliokuwa ukitumika awali kupitia kwao (TCU).
Aprili 15, mwaka huu, Rais Magufuli alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika utekelezaji wa ahadi yake Juni mwaka jana, alisema utaratibu wa sasa unawachanganya wanafunzi.
“Ninaamini kama wanafunzi wangepewe nafasi ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya serikali kama vile UDSM, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,” alisema.
Rais Magufuli alisema TCU imekuwa ikiwachagulia wanafunzi vyuo visivyo na sifa na ambavyo havina makazi ya wanafunzi hivyo kusababisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu na wanapomaliza masomo yao kukosa ajira kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na sifa.
Aidha, Rais aliitaka TCU kubaki na udhibiti, ikiwamo kuhimiza ubadilishaji wa maarifa/elimu kwa njia ya kuunganisha kimtandao vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu, uthibitishaji wa program za kitaaluma, uthibitishaji na uratibu wa udahili wa wanafunzi.
Mengine ni ufuatiliaji na udhibiti wa elimu bora Vyuo Vikuu na Vyuo Vya Vyuo Vikuu, ukusanyaji na usambazaji wa taarifa/data kuhusu elimu ya juu.
Katika tovuti hiyo, TCU imeainisha sifa za wanafunzi wanaopaswa kuomba kujiunga na masomo ya vyuo vikuu, na kwamba maombi yataanza rasmi Julai 22 hadi Agosti 13, mwaka huu, na masomo yataanza rasmi Oktoba 30, mwaka huu.
Kabla ya mfumo wa sasa, TCU ilioyoanzishwa Julai Mosi mwaka 2005, pamoja na majukumu mengine, ilikuwa na kazi ya kudahili wanafunzi kupitia mfumo uitwao Central Admission System (CAS).
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA