KLABU ya Azam FC imesema kwamba ipo kwenye mazungumzo na wachezaji wake wawili wanaohusishwa na mpango wa kutaka kuhamia Azam FC, kipa Aishi Manula na beki, Shomary Kapombe.
Wawili hao wote wanamaliza mikataba yao mwezi huu na imekuwa ikiripotiwa kwamba wako kwenye mipango ya kujiunga na Simba SC.
Lakini juzi, Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi alisema kwamba mazungumzo yanaendelea vizuri na wote wawili ili kuongeza mikataba.
“Napenda niwahakikishie, mazungumzo yanaendelea vizuri na wote wawili, Aishi pamoja na Kapombe ili waongeze mikataba, nataka niwatoe wasiwasi kabisa wapenzi wa Azam kwamba, wachezaji wote hao hawataondoka,”amesema.
Pamoja na hayo, Azam FC ambayo imewaacha wachezaji wake, kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’ na washambuliaji Ame Ali na John Bocco ‘Adebayor’ imepandisha wachezaji sita kutoka kikosi chake cha timu ya vijana.
Waliopandioshwa ni mabeki Abdul Hajji, Godfrey Elias na Ramadhani Mohammed, viungo
Stanslaus Lwakatare, Abbas Kapombe, ambaye ni mpwa wa Shomary Kapombe na mshambuliaji
Yahya Zaidi.
Jaffar Iddi alisema zoezi la usajili wa wachezaji wa ndani linaendelea, ili kuboresha kikosi kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya Julai 3, mwaka huu.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA