Mavugo Amsainisha Ndikumana Simba Sc,,Hivi Ndivyo Mchezo Ulivyokuwa.


SIMBA inahitaji huduma ya beki Mrundi wa Mbao FC, Yusuf Ndikumana, katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na sasa imeamua kumpa dili hilo Mrundi mwenzake, Laudit Mavugo ili alikamilishe.

Ndikumana ameonyesha kiwango kizuri akiwa katika kikosi cha Mbao FC ambayo ilipandishwa daraja kucheza msimu huu Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutokea upangaji wa matokeo kwa timu za Geita Gold na Polisi ya Tabora.

Beki huyo ambaye yuko katika rada za timu tatu hapa nchini Simba, Yanga na Kagera Sugar ambapo nao wanahitaji huduma ya mchezaji huyo, amedaiwa kuwa ameamua kuzipiga chini timu mbili na kukubali kutua Msimbazi.

Uongozi wa Simba umemtumia straika wao, Mavugo baada ya kubaini ukaribu uliopo kati yake na Mrundi huyo mwenzake na mambo yanaenda vizuri.

Ndikumana kwa sasa ni mchezaji huru mara baada ya kumaliza mkataba wake wa kukitumikia kikosi cha Wauza Mbao  mkoani Mwanza.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu ya Simba, zinaeleza kwamba mchakato wa kumpata beki huyo mwenye uwezo wa kucheza kama kiungo ulianzia baada ya kumalizika kwa fainali ya michuano ya Kombe la FA, mjini Dodoma.

Alisema Simba wameridhika na kiwango kilichoonyeshwa na mchezaji huyo, hali iliyopelekea kupendekeza jina lake katika usajili.

“Mchakato unaendelea vizuri, kwa upande wa mchezaji huyo haina shida kwani tayari maelekezo amepewa Mavugo ili msimu ujao awepo katika kikosi cha timu yetu,” alisema.

Alisema mara baada ya jina hilo kufika mezani, viongozi walifuatilia rekodi za mchezaji huyo kwa kujiridhisha  ambapo mchakato wake sasa umefika katika hatua nzuri ya makubaliano ya kusaini miaka miwili.

DIMBA lilikuwa shuhuda wakati Ndikumana na Mavugo walipokaa pembeni na kuzungumza mara baada ya kumalizika kwa fainali, lakini pia mmoja wa wachezaji hao aliomba mawasiliano ya simu.

Ndikumana alipoulizwa juu ya hilo, hakutaka kuweka wazi na kusisitiza kwamba kwa sasa hajafanya mazungumzo na timu yoyote na kuhusu Mavugo alidai ni mtu  wanayefahamiana kwa muda mrefu.

“Mavugo ni rafiki yangu tulikuwa wote timu ya Taifa ya Burundi, suala la Simba kama wapo tayari  kutoa kiwango cha fedha anachotaka, nitajiunga nao,” alisema.

Chapisha Maoni

0 Maoni