IVAN Ssemwanga amekwenda lakini huku nyuma ameacha kimbembe kufuatia baadhi ya ndugu zake kumlipua aliyekuwa mkewe, Zarinah Hassan ‘Zari’ na kudai kuwa, anatakiwa akae mbali na mali za ndugu yao kwa kuwa alimtenda vibaya enzi za uhai wake.
Ndugu hao mara tu baada ya mazishi walionekana kumzodoa Zari na kuviambia vyombo vya habari vya nchini Uganda kuwa, wameshangazwa na ukaribu wake kwa ndugu yao kipindi alipokuwa anaumwa wakati huko nyuma alikuwa kamtosa.
Mtandao mmoja wa nchini Uganda uliandika kuwa, Zari amekuwa hana amani kufuatia maneno ya baadhi ya ndugu wa Ivan wanaodhani ukaribu wake ni ili apate sehemu ya mali za marehemu.
“Wanamsema sana na yote hii ni kwa sababu ya mali ila busara inatakiwa itumike katika kipindi hiki kwa kuwa Zari ana watoto wa marehemu.
“Mawifi wamekuwa mstari wa mbele kumsakama lakini kibaya zaidi ni lile tamko la msemaji wa familia kusema kifo cha mtoto wao kimesababishwa na Zari,” uliandika mtandao huo.
Kiongozi wa familia aliyetambulishwa kama baba mlezi wa Ivan, Herbert Luyinda alikaririwa na gazeti la Uganda liitwalo Bukedde akisema: “Kama familia, hatuna shaka kwamba Zari ndiyo chanzo cha kuumwa kwa Ivan na hatimaye kufariki dunia.
Tangu wametengana, Ivan hakawahi kuwa vizuri. Mtoto wetu alimpenda sana na akamjali kwa hali zote lakini akamtosa. Hili lilimchanganya sana na kusumbua afya yake. “Aidha, Zari siyo mjane wa marehemu, tunayemjua sisi ni mwanamke wa Afrika Kusini aitwaye Ddudu ambaye ni mjamzito.”
Maneno hayo ndiyo yalizidisha kasi ya Zari kushambuliwa, lakini kwa ujasiri wake amekuwa imara na mara nyingi ameonekana akiwa na watoto wake aliozaa na Ivan wakifarijiana. Kufuatia yote yanayosemwa, juzikati Zari aliposti mtandaoni maneno haya: “Katika maisha kuna wakati utajua nani ni muhimu kwako na nani siyo.
Kuna watakaokuwa wanajifanya wako upande wako kumbe ni uongo. Lakini katika ulimwengu huu kilichopo katika mlango wangu ipo siku kitakuja kukugongea kwenye mlango wako.”
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA