STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, huenda msimu ujao asionekane katika kikosi cha timu hiyo kutokana na kutojua hatima yake ndani ya klabu hiyo mpaka sasa.
Tambwe ambaye ameongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo tangu alipojiunga nayo msimu wa 2014/15 akitokea Simba, ameliambia Championi Ijumaa kuwa kwa jinsi mambo yanavyoenda inawezekana asiitumike timu hiyo msimu ujao.
Alidai kuwa mpaka sasa hakuna chochote kinachoendelea kati yake na uongozi, hivyo kama hali hiyo itaendelea mpaka mwezi Julai, basi atachukua uamuzi wa kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine katika timu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kusajili za hapa nchini na nje ya nchi.
Kwa sasa Tambwe ameifungia Yanga mabao 46 katika michuano ya ligi kuu tangu alipojiunga nayo, yupo kwao nchini Burundi kwa ajili ya mapumziko na hajui lini atarejea nchini.
“Kwa hiyo, kutokana na hali hiyo sijui nitarejea lini nchini, lakini ninachoweza kusema ni kwamba bado ninaipenda Yanga na ndiyo maana nimeamua kusitisha mipango yangu mingine mpaka niwasikilize wao kwanza.
“Lakini wakiendelea kuwa kimya mpaka Julai basi nitachukua uamuzi mwingine kwa sababu soka ndiyo kazi yangu, naweza kujiunga na timu yoyote hapo nchini au nje ya nchi ambazo tangu zamani zimekuwa zikinihitaji,” alisema Tambwe ambaye mkataba wake na Yanga tayari umeshamalizika.
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA