Yanga: Tunasajili mchezaji yoyote tunayemtaka



Klabu ya Soka ya Yamga imetamba kwamba hakuna mchezaji anayehitajika na Klabu hiyo ikashindwa kumpata wala hakuna mchezaji anayeweza kuondoka yanga kama anahitajika.


hayo yamebainishwa na Kaimu  Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Clement Sanga  kwamba kila kitu kinakwenda sawa Yanga SC na hakuna mchezaji wanayemtaka ataondoka na wote wanaowahitaji kuboresha kikosi chao watawapata.

Katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online jana usiku, Sanga alisema kwamba baada ya kumaliza msimu, viongozi wamegawana majukumu katika kutekeleza masuala mbalimbali ya ustawi wa klabu kuelekea msimu ujao.

Sanga amesema kwamba Kamati ya Mashindano imejikita kwenye suala la usajili kwa sasa na mchakato unaendelea vizuri, wakati Kamati nyingine zinaendelea na majukumu yake mengine pia.

“Nataka nikuhakikishie, kila kitu kinakwenda sawa Yanga na wachezaji wote tunaowahitaji wabaki, watabaki, hakuna atakayeondoka. Na ambao hatutaki, basi wataondoka,”alisema.

Sanga pia amethibitisha kocha Mkuu, George Lwandamina kutoka Zambia ataendelea na kazi kwa msimu mwingine wa pili.

Na kuhusu habari zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mkataba wa udhamini wa SportPesa una kasoro kubwa, Sanga amesema si kweli.

“Mkataba unaozunguka si mkataba ambao upo mikononi mwa Yanga, kama kuna mtu ambaye ni mwanachama anaweza kupita makao makuu ya klabu (Jangwani, Dar es Salaam) kwa Katibu (Charles Boniface Mkwasa) nimemwagiza awaruhusu watu kuuona ukiwa pale,”alisema.

Pamoja na hayo, Sanga amesema kwamba klabu inahitaji utulivu sana kipindi hiki, wakati viongozi wanaendelea kuweka mambo mengi sawa.
Na akasema Mwenyekiti Manji amejiuzulu kwa wema tu na hata kinyongo na mtu yeyote wala klabu.

Chapisha Maoni

0 Maoni