Katika kudumisha haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeendelea kufanya uangalizi wa utendaji kazi wa serikali ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake bila kukiuka misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.
Mnamo Machi 7, 2018 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilipata taarifa za kushtusha za kutokuonekana kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) Ndugu Abdul Nondo na kufarijika baada ya kupata taarifa za kupatikana kwake mapema.
Hata hivyo taarifa za shutuma zilizoelekezwa kwa Abdul Nondo kutoka kwa jeshi la Polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kujisalimisha kwa Jeshi la Polisi huko Iringa zimekishitua Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na kuona ni vyema kufanya kumbushi ya kisheria kwa jeshi la polisi na viongozi hao kwa kukiuka sheria kama inavyofafanuliwa;
Dhana ya Kutokuwa na Hatia (Presumption of Innocence)
Kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura No.2 kama ilivofanyiwa marejeo mwaka 2002:-
“Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.”
Ni kosa kumhukumu mtu yeyote bila ya chombo chenye mamlaka hayo kuthibitisha kuwa mtu huyo amefanya kosa hilo. Viongozi wa kisiasa na serikali kuzungumza baadhi ya masuala kama maamuzi ya mwisho na kuingilia muhimili wa mahakama na kuwaita watu wahalifu na kusahau dhana pana ya kutokuwa na hatia hadi imethibitishwa ni ukiukwaji wa Katiba.
Kuingiliwa kwa muhimili wa Mahakama
Mahakama ndio chombo chenye mamlaka ya juu zaidi katika utoaji haki kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977:-
“Mamalaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mahakama.”
Viongozi wa serikali na jeshi la polisi watafanya kosa kumshutumu mtu yeyote yule na kuingilia uhuru na kazi ya mhimili wa Mahakama kinyume cha Katiba walioapa kuilinda.
Ukiukwaji wa Haki ya Kupata Dhamana
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzanaia imetoa haki ya mtu kupata dhamana pale ambapo suala lake lipo katika vyombo vya utaoji wa haki. Ibara ya 13 (6) (a) inaeleza:-
“Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote inapohitajika kufanyiwa maamuzi na mahakama au chombo kingine chochote kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kiukamilifu, na pia haki ya kukata rufani au kupata nafuu nyingine.”
Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi lilipaswa kutoa dhamana kwa Abdul Nondo. Mahakama imeweza kutangaza vipengele vya sheria vinanvyokinzana na Katiba katika kumnyima mtuhumiwa kupata dhamana pale ambapo shauri lake linapokuwa linasikilizwa au anapokuwa chini ya upelelezi wa Jeshi la Polisi.
Tumeshuhudia hivi karibuni Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mtobesya, ambapo Mahakama imetangaza kifungu namba 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura No. 20 kuwa batili kwani kinampa mamalaka Mkurugenzi wa Mashtaka mtuhumiwa haki ya kupata dhamana. Si sahihi kumuweka mtu kizuizini bila dhamana au kufikishwa mahakamani kwa zaidi ya siku saba wakati sheria imeweka masaa 24 .
Haki ya kupata Uwakilishi
Mtu anapokuwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi kama mtuhumiwa anayo haki ya kupata mwanasheria ili aweze kumwakilisha mahakamani wakati wa kusikiliza kesi. Ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeeleza kwamba wakati haki na wajibu wa mtu yeyote inapohitajika kufanyiwa maamuzi na mahakama au chombo kingine chochote basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kiukamilifu na kuweza kupata nafuu au nafuu nyingine ya kisheria.
Mahakama zimetoa tafsiri juu ya Haki ya Uwakilishi kwa mtuhumiwa yeyote. Mtuhumiwa anapaswa kuelekezwa kuwa ana haki ya kupata haki ya uwakilishi toka kwa Wakili haya yalisemwa katika kesi ya Thomasi Mjengi & Wenzake dhidi ya Jamhuri 1992 TLR 157, ambapo Jaji Mwalusanya enzi za uhai wake alisema:-
“Haki ya uwakilishi inahusisha pia haki ya mtuhumiwa kuambiwa kuwa ana haki ya kupata uwakilishi na hayo yasipofuatwa basi maamuzi ya awali yaliyotolewa huwa batili.”
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu hakiafiki kitendo cha Polisi chini ya kitengo cha Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), kuwakatalia Mawakili kuweza kumwona mtuhumiwa Abdul Nondo na kuweza kupata haki ya uwakilishi mbele ya vyombo vya utoaji haki.
Msimamo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Ili kudumisha utawala wa sheria na haki za binadamu nchini, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinawataka viongozi wa serikali na vyombo vya dola kufuata sheria na kuheshimu haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) kutumia mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa sheria kuwachukulia hatua viongozi wanaokiuka misingi ya haki za binadamu na utawala bora.
Imetolewa Machi 15, 2018 na,
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji
0 Maoni
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA